WATU 788 WAANZISHIWA DAWA ZA ARV KITETO

Bw. Mavanza wa Africare akizungumza na wananchi siku  ya Ukimwi kata ya Engusero Kiteto Manyara TZ
 
Watu 788 Kiteto waanzishiwa dawa za ARV

Na.Mohamed Hamad Manyara
JUMLA ya watu 788 wilayani Kiteto mkoani Manyara wameazishiwa dawa za kurefusha maisha (ARV) huku wengine 640 wakisubirishwa kuanza dawa hizo kutokana na CD4 zao kuwa juu ya kiwango cha kuanza dawa

Kwa mujibu wa Abubakar Omari muhudumu wa wagonjwa majumbani (HBC) wilayani hapo akizungumza na Jambo leo amesema idadi hiyo imetokana na elimu kuendelea kutolewa na watu kupata uelewa wa kutumia dawa

“Mwanzo ilikuwa ni vigumu sana mtu kujitangaza kuwa anaishi na virusi vya Ukimwi hali iliyofanya wengi wao kupoteza maisha kutokana na hofu mbalimbali zikiwemo kunyanyapaliwa na jamii lakini sasa wengi wao wamekubali kuwa wahamasishaji”

“Tunavyo vikundi vya watu wanaoishi na VVU Ukimwi ambavyo kazi yao ni kuhamasisha jamii juu ya janga la Ukimwi namna ya kukabiliana nalo lakini pia kuwataka waache tabia ya kuwanyanyapaa watu wanaoishi na VVU Ukimwi”alisema Abubakar

Alisema kati ya idadi hiyo wa walioanza dawa wengi wao walishindwa hata kutembea na kujikuta wakilala lakini baada ya kufikiwa na wahudumu wa wagonjwa majumbani akiwemo yeye wengi wao wameanza hata kufanya biashara zao ndogondogo

Alitaja kazi za (HBC) kuwa ni pamoja na kuwabaini wagonjwa wanaoishi na VVU Ukimwi na kuwapeleka hospitali kupima,kuwasaidia kufua nguo zao pamoja na kuwapikia,kutoa elimu ya kuwasaidia waishi kwa kujiamini

Hata hivyo Abubakari alitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili WAVIU wilayani humo kuwa ni pamoja uhaba wa lishe, kunyanyapaliwa ndani ya jamii pamoja na hali duni ya wanajamii hivyo kutowathamini ndani ya jamii

Katika hatua hiyo amepongeza na kuzishukuru baadhi ya taasisi na mashirika ya umma ambayo yamekuwa mstari wa mbele kutoa misaada mbalimbali kwa WAVIU na kuyaomba yaendelee na jitihada hizo kwani wengi wao walikata tama ya kuishi kwa kukosa dawa na hata lishe

Ametaja baadhi ya wadau wanaowasaidia WAVIU kuwa ni pamoja na Africare,na Halmashauri ya Wilaya kwa kiwango flani kusaidia vikundi hivyo pesa za miradi ikiwemo ya ufugaji wa kuku mbuzi na biashara ndogondogo za sokoni

MWISHO





Maoni