MIGOGORO YA ARDHI 2 WAUAWA 20 WAJERUHIWA KITETO


mmoja wa wakulima katika kijiji cha Ndirigishi kata ya Engusero muda mfupi baada ya kuuawa na watu wanaodaiwa kuwa ni wafugaji Picha na Mohamed Hamad Manyara


Mgogoro wa ardhi Kiteto.

Wakulima 2 wauawa 20 wajeruhiwa

Na Mohamed hamad
Wakulima wawili wamepoteza maisha kwa kukatwa katwa mapanga na wengine ishirini kujeruhiwa  wilayani Kiteto mkoani Manyara baada ya kuvamiwa na wafugaji katika maeneo tofauti kutokana na mgogoro wa ardhi kati yao na wafugaji

Waliouawa ni pamoja na Selemani Chihamilo (30) wa Ndirigishi na Zuberi Rashidi wa kijiji cha Chekanao huku wengine zaidi ya ishirini wakiendelea na matibabu Hospitali ya wilaya ya Kiteto na kituo cha afya cha Enguseri

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Manyara Deusdedit Nsimeki amekiri kutokea matumikio hayo na kwamba kikosi maalumu cha polisi kutoka Manyara kimewasili kwa ajili ya kuzuia mapigano hayo

“Polisi wako eneo la tukio kwa hivi sasa ambapo wengine wako kijiji cha chekanao alikouawa mtu mmoja shambani kwake akikataza mifugo isiingie shambani  na mwingine Kijiji cah Ndirigishi ambapo mkulima mwingine kauawa hivyo tumetawanyika kukabiliana na tukio hilo” alisema

Mauaji hayo ni mwendelezo wa mapigano ya mara kwa mara ambapo mwaka huu Waziri mkuu Mizengo Pinda aliwasili Wilayani humo baada ya kuuawa zaidi wa watu kumi na kuagiza watu hao wakamatwe na kufikishwa mahakamani

Toka agizo hilo litolewa wafugaji na wakulima wameendelea kuhasimiana huku wakiuana kutokana na madai ya kuingiliana kwenye maeneo ya kazi jambo ambalo limedaiwa uongozi wa wilaya umeshindwa kuwakutanisha ili kuondoa tofauti zao

“Mgogoro wa ardhi kiteto umedumi kwa zadi ya miaka kumi kutokana na kutumika kama vyanzo vya mapato ya baadhi ya viongozi ambapo Katibu Mkuu wa CCM Abrahamani Kinana akiwa ziarani hapa alisema ataenda kuongea na Rais juu ya tatizo hili” alisema Bakari Maunganya (mwananchi)

“Kama kweli viongozi wetu hawahusiki tungewaona wakishiriki nasi katika misiba kutoa hata pole kama ilivyo maeneo mengine ya nchi hii,tazama toka maafa haya yatokee juzi hakuna kiongozi yoyote aliyeongea nasi hata kwenye vyombo vya habari”

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Halamshauri ya Wilaya ya Kiteto Minge Lemalali amekiri kuwepo kwa tatizo la uongozi ambapo alisema linachangiwa na baadhi ya viongozi wasiokuwa waadilifu kutoka wilaya na mikoa ya jirani

“Huwezi kuisemea wilaya ya jirani juu ya jambo lolote kwani kila wilaya ina mipaka yake sasa inakuwaje Mbunge wa Kongwa Jobu Ndugai azungumzie wilaya ya Kiteto kuwa kuna mauaji na sio eneo lake huu ni uchochezi”alisema Mwenyekiti wa Halamshauri Mainge Lemalali

Kila kiongozi ana mipaka yake ya kiutawala hivyo kila mtu azungumzie eneo lake namuomba Ndugai aiache Wilaya ya kiteto  asituingilie kabisa na kama anataka eneo la kilimo afuate utaratibu na sio kuvamia kama wanavyovamia watu wake hatukubali

Akiongea kwa njia ya simu Mbunge wa Kongwa Jobu Ndugai alisema Wilaya ya Kiteto ni sehemu ya Tanzania hataacha kuizungumzia kwa kuona kuwa imekuwa eneo hatari kwa watu wanaojihusisha na shughuli za kilimo kuuawa na kuongeza kiongozi mzuri atapimwa na wananchi wake

“Kila raia wa nchi hii ana haki ya kuishi mahali popote ili mradi asivunje sheria sasa kama kuna anayevunja sheria huko Kiteto tuone wakiadhibiwa na mahakama na sio kuuawa kinyama tena eti kwa kuchinjwa”alieleza Ndugai huku akionyesha kukerwa na vitendo hivyo

Alisema Serikali inajua kinachofanyika Kiteto na sio kingine bali ni ubaguzi wa kikabila wa hali ya juu na kuiomba kuharakisha maamuzi yao ambayo yatasaidia kuepusha vifo hivyo ambavyo havina sababu tena kwa nchi hii inayosifika kwa amani duniani

Mwisho

Maoni