Mohamed Hamad katika harakati za kupiga picha kikao cha bajeti cha baraza la madiwani Kiteto
Wanafunzi
771 Kiteto waliofaulu hawakuripoti sekondari
Na. Mohamed Hamad Manyara
Jumla ya wanafunzi 771 waliofaulu kujiunga na Sekondari
wilayani Kiteto mkoani Manyara wameshindwa kuripoti sekondari kutokana na
sababu mbalimbali zikiwemo kuolewa pamoja na kukosekana kwa mwamko wa elimu kwa
jamii
Katibu tawala wa wilaya ya Kiteto Nicodemus John
akizungumza kwenye kikao cha Baraza la madiwani leo (jana) alisema idadi hiyo
imetokana na wengi wa wanafunzi hao kuwa na wachumba shuleni na baada ya
kumaliza kuolewa
“Idadi hii ni kubwa na wala haivumiliki kuona kiasi hiki
kikikosa elimu,naagiza kila Katibu Tarafa awe amewabainisha watoto na
kuwafikisha wazazi wao mahakamani mara moja”alisema Nicodemas
Kuhusu agizo la Rais kutaka kujengwa vyumba vitatu vya maabara
katika kila Sekondari Katibu huyo alisema muda uliongezwa kukamilisha ujenzi
huo na kuwataka kila kiongozi wa jamii awajibike katika nafasi yake
Alisema Kiteto inahitaji viongozi wawajibikaji na sio kupiga
midomo kwani agizo hilo la Kiongozi wa Nchi ni sheria na atakaye kaidi sheria
zitamthibitikia zikiwemo adhabu ya kifungo, faini ama vyote kwa pamoja kutokana
na maamuzi ya Hakimu
Kwa upande wake Kidawa Othman Diwani wa kata ya Matui
CHADEMA alishangazwa na baadhi ya kata za jamii ya kifugaji wamasai kama vile
Makame,Ndedo, Namelock,na Partimbo kushindwa kutekeleza agizo la Rais wakati
wana rasilimali nyingi na za kutosha (mifugo)
“Mbona kwenye zoezi la kuwatoa wakulima mashambani
wafugaji na rasilimali zenu mliungana kuchangia madume, kwanini agizo hili la
Rais mnalisusia kwa kugoma kuchanga fedha kwaajili ya maabara”alisema Kidawa
Kutokana na agizo hilo kata ya Namelock, Partimbo na
Makame zimeshindwa kufikia kiwango stahili cha ujenzi ambapo kwa tarafa ya
Makame badala ya kila kata kujenga Sekondari yake wameamua kujenga Sekondari ya
Tarafa tofauti na agizo la Rais
Kwa upande wake Bosco Ndunguru Mkurugenzi Mtendaji wa
Halamshauri ya Wilaya ya Kiteto alizitaka kata hizo kuongeza jitihada akisema
kila kiongozi atawajibika katika nafasi yake muda utakapofika akisisitiza kuwa
kinachotakiwa ni maabara tatu kila Sekondari
“Kila mtu aguswe na maendeleo ya kata yake sioni sababu
ya suala hili kuonekana kukwama kutokana na kuwepo kwa rasilimali nyingi na za
kutosha ndani ya jamii na ikishindikana mabaraza ya kata yatumike kufanikisha
zoezi hili”alisema Ndunguru
Mwisho
Maoni
Chapisha Maoni