DC Nzoka apewa cheo cha “laigwanani”Kiteto



NA. MOHAMED HAMAD MANYARA.
MKUU wa wilaya ya Kiteto mkoani Manyara Kanali Samuel Nzoka amekabidhiwa cheo cha (laigwanani) kuwa msemaji wa rika la korianga ndani ya jamii ya kifugaji masai ambapo atakuwa na jukumu la kusimamia masuala mbalimbali yakiwemo usuluhishi

Cheo hicho alikabidhiwa kwenye sherehe iliyoandaliwa na jamii hiyo ya (kimasai) ya kupanda rika iliyofanyika katika kijiji cha Mbigiri kata ya Partimbo ambapo atakuwa na uwezo wa kuzungumza na rika hilo kwa masuala mbalimbali yanayowahusu

“Kundi hili la korianga Kiteto ndilo lililokuwa linajihusisha na uhalifu hapa ukiwepo wa mauaji kati ya wakulima na wafugaji nafasi hii itakuwa mwarubaini wa mauaji kwani kiapo hiki atakayekiuka atapata madhara kwa jamii hii”alisema Kanali Nzoka

Awali Mkuu wa wilaya akizungumza na kiongozi wa mila Mbambire Olkurukuru alimwagiza kuita vikao ndani ya jamii hiyo na kuzungumza na vijana hao wa rika la Korianga kwani lilikuwa tishio kubwa kwa wananchi ambapo sasa amedai hali ni shwari

Agizo hilo lilitekelezwa kwa kufanyika vikao mbalimbali  katika vijiji vya Ndaleta, Kimana na Lalala ambapo jamii hiyo iliweza kuelezwa agizo hilo la Serikali kuwa waache kujiingiza kwenye uhalifu ambao umeleta madhara makuybwa ndani ya wana-Kiteto

Katika sherehe hiyo ya kupanda rika kundi kubwa la vijana hao wa kimasai wakiambatana na makundi mengine ya jamii hiyo walionekana wakiwa na vipande vidogo vya matawi ya miti kama ishara ya kurejesha amani wilayani humo na kufanya mila kwamba atakayekiuka atapata madhara makubwa

Kanali Nzoka alikabidhiwa rungu jeusi maafufu (orkumaa) kama ishara ya kuwa kiongozi wa rika la korianga ambaye atakuwa anaalikwa kwenye vikao mbalimbali na kupata nafasi ya kuongea nao katika masuala mbalimbali yanayowahusu na hata maagizo ya Serikali

Mbambire Oleikurukuru kiongozi wa mila akizungumza na MTANZANIA alisema nafasi hiyo inatolewa kwa watu mwaminifu ndani ya jamii hiyo, hivyo wamemwamini mkuu huyo wa wilaya kama mtu ambaye hawezi kuwasaliti na atashikikishwa mambo mbalimbali ya jamii hiyo

“Wamasai tuna mambo mengi yanayohusu mila zetu…sisi tumemwamini mkuu huyu wa wilaya tutashirikiana naye katika kukemea masuala mablimbali ndani ya jamii yetu ambayo hufanywa na makundi mbalimbali kama vile uhalifu wa wizi wa mifugo,na hata mauaji”alisema

Jamii ya wafufaji masai na wakulima walihasimiana wakigombea ardhi mwanzoni mwa mwaka jana wilayani hapo ambapo zaidi ya watu 38 walipoteza maisha na kuisukuma Serikari kuingilia kati kwa kuweka kambi kurejesha amani iliyokuwa ikisuasua wilayani humo

MWISHO



Maoni