NA.MOHAMED HAMAD MANYARA
Jopo la madaktari wa hospitali
ya wilaya ya Kiteto mkoani Manyara limefanikiwa kuokoa maisha ya Bi.Sinyati
Parla (33) kwa upasuaji aliyekaa na mimba ya mtoto wa kiume aliyefia tumboni
kwa miaka mitano
Upasuaji huo ulifanyika
mwishoni mwa wiki katika hospitali ya Kiteto baada ya mwanamke huyo kulazwa na
kufanyiwa uchunguzi na kubainika kuwa alikuwa na uvimbe mkubwa tumboni ambapo
alitolewa mtoto wa kiume tumboni akiwa mfu
Akiongea na UWAZI Dr. Leadry
Malisa aliyefanya upasuaji huo kwa kushirikiana na Dr Madama Hosea alisema walifanikiwa
kutoa maiti hiyo ya mtoto wa kiume iliyokuwa tumboni kwa miaka mitano
“Haikuwa rahisi kama tulivyozoea kufanya
upasuaji wa kawaida, lakini kwa mapenzi ya mungu tulifanikiwa na hali ya
mgonjwa imeimarika naamini atapona na kuendelea na kazi zake za kawaida za kila
siku”alisema Dr Malisa
Hata hivyo jopo hilo la madaktari lilisema
kuwa upasuaji huo ulikuwa ni wa aina yake na wakihistoria wilayani humo ambapo wamedai
haijapata kutokea toka wilaya hiyo izinduliwe mwaka 1974 kutoa kiumbe mfu
kilichokaa kwa miaka mitano tumboni
Uchunguzi uliofanywa na
gazeti hili umebaini kuwa mimba hiyo ilikuwa ni ya nne kwa mwanamke huyo ambapo
awali alijifungua watoto watatu wote wakiwa salama na afya njema
Katika kuhakikisha kuwa uhai
kwa akinamama wajawazito unaimariishwa Dr
Malisa aliwataka wanawake wajawazito kuwa na utamaduni wa kwenda kiliniki mara
wanapopata ujauzito kupata ushauri wa kitaalamu hadi watakapojifungua
Akizungumza akiwa amelazwa
wodi namba mbili katika Hospitali hiyo mwanamke huyo alitaja baadhi ya
Hospitali alizofika kusaka huduma katika kipidi hicho chote kuwa ni pamoja na
Seliani ya Arusha, KCMC Moshi na Mhimbili
Alisema alitumia fedha nyingi
kusafiri pamoja na kugharamia za matibabu
kwa miaka mitano mfululizo ambapo katika Hospitali ya Kiteto aliitwa tu na
ndugu yake aliyempeleka hospitali na kufanyiwa upasuaji huo
“Nawashukuru sana madaktari kwa kazi
nzuri waliyofanya kwani sasa nina matumaini mazuri kuisha naamini kuwa nitapona
kwa hapa nilipofikia kwani nilishakata tamaa ya kuishi”alisema Bi.Sinyati Parla
Mwisho
Maoni
Chapisha Maoni