KIPINDI HIKI CHA UCHAGUZI
NA MWANDISHI WETU WASHINGTON
Serikali ya Tanzania imetakiwa kuhakikisha kuwa amani na usalama
vinakuwepo wakati na baada ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu
utakaofanyika nchini Tanzania tarehe 25 mwezi huu.
Profesa Nicholas Boaz,
Wito huo umetolewa na Mhadhiri wa Mawasiliano na Sera katika Chuo Kikuu
cha Maryland nchini Marekani, Profesa Nicholas Boaz katika mahojiano
maalum na Swahilivilla.
Akizungumza na mwandishi wetu nyumbani kwake, Profesa Boaz ambaye
amerejea nchini Marekani hivi karibuni baada ya ziara yake Tanzania,
alisema kuwa nchini Tanzania kuna joto kali sana na vuguvugu la
mabadiliko."Kuna joto kali sana la uchaguzi. Kwa kweli naona watu wengi
wanaitikia wito wa kutaka mabadiliko", alisistiza profesa Boaz.
Alisema kuwa hali duni za wananchi katika nyanja mbalimbali za maisha
baada ya miaka mingi ya utawala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na miaka
kumi ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete, ndiyo iliyopelekea mwamko wa
vuguvugu la kutaka mabadiliko.
"Baada ya muda mrefu wa CCM kuwa madarakani, na miaka kumi ya Rais
Kikwete, basi watu wamepata mwamko kuwa maisha na maendeleo yao yamekuwa
duni.
Kwa hivyo wanataka wapate mabadiliko ya kiongozi na kimtazamo juu ya
namna ya kuweza kuwasaidia watu hasa katika maswala ya kazi, afya, mamno
ya shule na mambo mengine mengi".
Aliyataja mambo hayo mengine kuwa ni swala la uhuru wa watu kujieleza na kuuliza juu ya kitu ambacho kinawakera.
Akijibu swali iwapo kweli wananchi wa Tanzania wamepata mwamko wa
mabadiliko au wanaimba tu nyimbo za wanasiasa, Bwana Boaz alisema
"Huwezi kuingia akilini mwa watu kuwajua nini wanakitaka.
Lakini ukiona watu wanakusanyika wakasema wanataka mabadiliko, kuna kitu
gani cha kuuliza zaidi ya hicho?" alidadisi msomi huyo na kuongea, "huu
ni ushahidi kuwa watu wanataka mabadiliko ya kweli"
Aidha alisema kuwa wimbi hilo la mabadiliko linatokana na hali ya watu
kukata tamaa na ahadi zinazotolewa na viongozi wa CCM wakati wakitafuta
ridhaa ya wananchi kuingia madarakani na badala yake hali za maisha
kuendelea kuwa duni.
Aliutolea mfano utawala wa Rais Kikwete ambaye aliingia madarakani akiwa
na ari mpya, nguvu mpya na milo mitatu kwa siku, lakini baada ya miaka
kumi ya utawala wake ukuwaji wa uchumi umebakia palepale.
"Kuna takwimu zinaonesha waziwazi, alipoingia Kikwete 2005 kuchukua
madaraka aliukuta uchumi ukiwa ni asilimia 0.7, kwa miaka kumi, huo
uchumi umebakia palepale, na watu hawapati hata nusu mlo", alifafanua
msomi huyo na kusisitiza "Watu wameamka, hawadanganyiki tena na mambo ya
zamani ya kubebwa tu na Chama. Watu sasa hivi wanangalia jinsi ya
kuboresha maisha yao na kulinda mustakbali wa watoto wao"
Mtaalamu huyo aliendelea kufafanua kuwa kumekuweko na takwimu za
kupotosha kuhusu ni chama gani kitashinda uchaguzi, hata hivyo alisema,
"Mimi nikiwa kama Mhadhiri na mtaalamu wa Mawasiliano na Sera, huwa
nayaangalia mambo yanavyokwenda kwa kutumia njia inayoitwa Observational
Research Method"
Alifafanua ibara hiyo ya kitaalamu kwa kusema "Naangalia mikusanyiko ya
watu anapokuwepo Lowassa na anapokuwepo Magufuli. Kwa hiyo, unaweza
kutazama kwa hiyo tu bila hata takwimmu".
Kwa mujibu wa utaalamu huo, Profesa Boaz anahisi kuwa upepo mwanana
unapulizia upande wa vyama vinavyojumuika chini ya mwamvuli wa Umoja wa
Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Pia alidokeza kuwa takwimu zenyewe zinabashiria ushindi kwa UKAWA. "Kuna
takwimu kutoka serikalini zinasema kuwa asilimia baina ya 60 hadi 74 ya
wapigakura wote ni vijana wenye umri kati ya miaka 18 hadi 40. Na
katika hao kuna uwezekano mkubwa vijana kuipigia kura UKAWA kuliko CCM",
alifafanua msomi huyo na kuongeza "Kwa hiyo ikiwa mambo yatakwenda
vizuri bila ubabaishaji, basi kuna uwezekano mkubwa kwa UKAWA kuchukua
nchi, lakini tarehe 25 mambo yatakuwa wazi"
Akijibu hoja kuhusu madai ya baadhi ya wadadisi wanaodai kuwa viongozi
wa CCM waliokihama chama hicho na kujiunga na kambi ya upinzani
wanatumiliwa na chama tawala kama vibaraka wa kudhofisha upinzani,
Profesa Boaz aliimabia Swahilivilla "Watu wana uhuru wa kudadisi mambo
au maoni, lakini watu wengine wanaweza kupotosha kitu ambacho
kinaonekana kina ukweli"
Aliitupilia mbali joja hiyo kwa kusema "Hayo ni mambo ambayo watu
wanayazusha na hayaingii hata akilini". Aliendelea kufafanua "Mimi
nimetembelea sehemu mbalimbali Tanzania, mijini na vijijini, na unakuta
kitu watu wanachokizungumzia ni mabadiliko"
Alisisitiza kuwa Watanzania wana kiu ya mabadiliko, na kwamba kati ya
watu kumi wanaozungumza saba wanataka mabadiliko. "Unaweza kuwakuta watu
kumi, labda wawili au watatu wanazungumzia CCM, lakini saba
wanazungumzia mabadiliko na wanasema ni kwa nini wanataka mabadiliko"
Aidha aliusifu mwamko wa wapiga kura kwa kuthamini na kuzilinda shahada
zao za kupigia kura kiasi cha kufikia kuziita "Vichinjio" na kuzionesha
wakati wanapoulizwa mikutanoni.
Aliwatolea changamoto wale wote wanaobeza vuguvugu la mabadiliko kwa
ksema "Tusubiri tuone hiyo tarehe 25 tuone mambo yatakuwaje, je kweli
hayo mabadiliko yanayozungumzwa yatatokea? Nafikiri labda tutazame pale,
lakini joto liko na watu wanataka mabadiliko"
Akijibu swali kuhusu malalamiko ya upinzani dhidi ya uadilifu wa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC), Profesa Boaz aliyapongeza mabadiliko
yaliyofanywa na Tume hiyo likiwemo swala la matokeo yote ya uchaguzi
kubandikwa vituoni tangu ya Udiwani hadi Uraisi, pamoja na vyama vyote
kuruhusiwa kuwa na mawakala wao ndani ya vituo vya kupigia kura.
"Nafikiri hayo ni mambo ambayo yameleta faraja kuwa kuna uwazi, kwa
sababu ukileta demokrasia vitu kama hivyo vinakuwa ni vya lazima,
huwezi kufanya vitu kwa kujificha ficha"
Hata hivyo, alielezea wasiwasi wake juu ya kauli ya Tume ya uchaguzi
kwamba wananchi wakishapiga kura hawaruhusiwi kukaa eneo la vituo vya
kupigia kura umbali wa mita 200, akisistiza kuwa hiyo ni haki ya
wananchi kikatiba. "Lakini katika katiba limo hilo, mwaka 2005 watu
walikaa.
Sasa hilo ni swali la NEC kulitatua. Kwa sababu ni haki na ndiyo njia ya uwazi kuona kweli kura zetu tumepiga, tunaziona"
Alielezea kuwa raia wa Tanzania ni watu wa amani na wasiopenda fujo, na
kamwe hawawezi kuanzisha jufo, na kwamba iwapo fujo zitatokea, basi wa
kubebeshwa lawama ni mamlaka husika.
"Kama kuna mtu ataanzisha fujo, basi ni askari wenyewe na serikali
yenyewe ya Chama cha Mapinduzi, na mimi siamini kuwa ni watu wenyewe
wataanzisha fujo", alisema Bwana Boaz kwa sauti ya kizalendo, na
kudadisi "Kwani kuna ubaya gani, kuna kitisho gani, au CCM ina
wasiwasi?"
Alifutilia mbali madai hayo ya uwezekanio wa kutokea fujo kwa kusema
kuwa viongozi wa upinzani wamekuwa wakiwahimiza wafuasi wao kutunza
amani na utulivu kwa kusema "viongozi wao hao wa vyama vya upinzani
wamewaambia, mukimaliza kupiga kura kaeni kule pembeni, tulieni"
Aidha, alikariri lawama zake kwa vyombo vya ulinzi na usalama na rais
Kikwete mwenyewe kwa kushindwa kuyakemea mambo hayo na kwenda kinyume na
katiba. "Fujo Tanzania ikianza, kwa kweli itakuwa imeanzishwa na askari
na yeye rais wa Jamhuri ya Tanzania ambaye alitakiwa hivyo vitu
avikemee sana, na kwamba afuate hiyo katiba, hii ndiyo maana ya sheria"
alitoa dukuduku lake na kuwa "Hili ndilo tatizo tulilonalo Tanzania,
sheria zinakuwa hazifuatwi"
Halkadhalika Profesa Boaz alitoa nasaha kwa rais Kikwete kuwaheshimu
wapiga kura ambao ndio waliomwingiza madarakani madala ya kutumia kauli
za vitisho. "Yeye Kikwete muda wake umekwisha, mimi nadhani angekaa
akatulia, aache tena haya mambo ya kusema Polisi watafanya mambo ambayo
watu hawayataki"
Alielezea imani yake kuwa Tume ya uchaguzi itaweza kurekebisha kasoro
zote kabla ya siku ya uchaguzi. "Kwa hiyo mimi naona tusubiri mpaka
Jumamosi, watu watakuwa wamelitatua, kwa sababu watu ni haki yao
kutazama", alisema Bwana Boaz na kuhoji "Kwani kuna ulazima wakake
nyumbani?
Prosesa Boaz alimalizia kwa kutoa nasaha kwa Watanzania wote wenye haki
ya kuoiga kura kujitokeza kwa wingi kupia kura na kumchagua mtu
wanayemtaka kwa njia za amani bila woga ili kuendeleza sifa ya Tanzania
kama nchi ya amani.
"Kwa hiyo mimi nahisi watu wakapige kura kwa amani wachague mtu
wanayemtaka, na siyo kununuliwa na mtu yoyote au kufanya jambo jengine
lolote"
itafaa kukumbusha kuwa kumekuweko na hali ya sintofahamu miongoni mwa
wadau wa kisiasa nchini Tanzania kufuatia kauli iliyotolewa na NEC
pamoja na Rais Jakaya Kikwete kwamba wananchi wakishapiga kura
hawaruhusiwi kukaa eneo la vituo vya kupigia kura umbali wa mita 200.
Hali hiyo imepelekea imepelekea baadhi ya wanasiasa wa upinzani kufungua
kesi mahakamni anaitaka mahakama itamke kama ni halali kwa Rais na Tume
ya Uchaguzi (NEC) kuzuia wananchi kukaa kwa utulivu umbali huo ama la.
Maoni
Chapisha Maoni