Wimbi la ‘kutimka’ kwa makada katika Chama Cha Mapinduzi (CCM)
linazidi kushika kasi baada ya kada mwingine wa chama hicho, Balozi Juma
Mwapachu, kutangaza kujivua uanachama wa chama hicho jana.
Uamuzi wa Mwapachu kujitoa CCM, unakuja siku chache baada ya
aliyekuwa kada mwenye nambari nane wa CCM, Kingunge Ngombale Mwiru
kutangaza kujitoa chama hicho Oktoba 4, mwaka huu.
Katika taarifa yake aliyoitoa jana huku sehemu kubwa akimsifia
Lowassa, Mwapachu ambaye hakutaja anajiunga na chama gani, alisema
kuanzia kesho (leo) yeye siyo tena mwanachama wa CCM na anatarajia
kurudisha kadi yao.
“Nimepata fursa ya kuwa kiongozi ndani ya chama hiki. Lakini
kuanzia kesho (leo) mimi si mwanachama wa CCM tena. Na mimi nakubaliana
na msimamo wa Lowassa na hao waliomfuata kutoka ndani ya CCM.” alisema
Mwapachu.
Alisema alikuwa mwananchama wa CCM tangu mwaka 1967 wakati alipojiunga na Tanu ambacho baadaye kiliungana na ASP na kuzaa CCM .
Alisema tangu alipokuwa mjini Dodoma kwenye mchahakato wa kumpata
mgombea wa urais ndani ya CCM alikuwa akimuunga mkono Edward Lowassa
ambaye hivi sasa ni mgombea urais wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) anayeungwa mkono pia na vyama vingine vinavyounda Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya NCCR-Mageuzi, NLD na Chama cha Wananchi
(CUF).
Alisema Lowassa ndiye chaguo lake katika kampeni za kumpata Rais
mpya wa Tanzania na kueleza kuwa chaguo lake si ndoto wala mlipuko wa
mapenzi juu ya Lowassa.
Mwapachu alisema amemfahamu Lowassa tangu miaka ya 90 akiwa kada wa CCM kwa mahusiano katika majukumu ya kichama.
“Kama marehemu Baba wa Taifa alivyowahi kusema, ‘CCM si mama
yangu’. Hivyo ndugu zangu, kuanzia kesho (leo) mimi si mwana-CCM tena.
Nitarejesha rasmi kadi yangu kupitia ofisi ya CCM ya kata yangu
Mikocheni, Dar-es-Salaam. Kwa sasa sijaamua kujiunga na chama kingine.
Mwenyezi Mungu anilinde,” alisema Mwapachu.
Alisema Lowassa amejaliwa nuru na uwezo wa kuongoza na kupendwa na
watu. Pia ni msikivu na asiyependa ukiritimba na utovu wa nidhamu
kazini, iwe ni kwa upande wa watumishi au kwake mwenyewe.
Aliendelea kusema kuwa, Lowassa ni kiongozi ambaye uchamungu wake
unamsaidia kuwa na uongozi unaojali na kuheshimu utu, ukweli na uwazi.
Mwapachu ambaye aliwahi kushika nafasi mbalimbali serikalini, ndani
ya CCM na pia kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, alisema
kuwa viongozi wanaodhani au kutaharuki kuwa Lowassa ana hulka ya
kulipiza kisasi kwa jambo lolote ni waongo.
“Lowassa ni chaguo la wengi na CCM katika busara yake ya kumuengua
katika mchakato wa kumpata mgombea wa urais, kimedhihirisha kutokuwa
chama kinachoendeshwa kwa misingi ya demokrasia,” alisema Mwapachu.
Alisema dalili za CCM kupoteza lengo la kuwa chama cha watu na kuwa
cha viongozi wachache zilianza siku nyingi na hasa katika kipindi cha
uongozi wa Rais Jakaya Kikwete.
Alisema CCM kimebadilika na kuwa chama cha makundi na migawanyiko
yakupambana si kwa malengo ya itikadi na ujenzi wa chama, bali ya
kumalizana na kutaka kufukuzana.
Mwapachu alieleza kuwa Lowassa angeweza kufukuzwa miaka mingi
iliyopita ila alishinda vita kutokana na kupendwa na idadi kubwa ya
wanachama ndani ya CCM.
Balozi Mwapachu alisema kujivua uanachama kwa Lowassa hivi karibuni
ulikuwa ni uamuzi sahihi kwa sababu CCM si chama tena cha watu na
kimetekwa.
Kadhalika, alisema aliwahi kuandika makala siku za nyuma akinukuu
mshairi kutoka nchini Uingereza aliyeandika 'There comes a time when the
door opens and allows the future in'.
Alisema mlango huo sasa umefunguka usoni kwake na uamuzi wake ni
kukubali kwamba wakati mpya umewadia ambao ni wakati wa mabadiliko.
Alisema kuendelea kujihisi kwamba bado ni mwana-CCM wa kadi ni kukubali kujidanganya mwenyewe.
CHANZO:
NIPASHE
Maoni
Chapisha Maoni