Dk. John Magufuli
Wafuatiliaji na wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini wanaamini
kuwa Waziri Mkuu ajaye atatoa picha kamili ya dhamira ya Rais mpya,
Magufuli, katika utekelezaji wa ahadi zake alizotoa wakati wa kampeni za
kuwania urais wakati wa Uchaguzi Mkuu.
Maeneo 10 ambayo Magufuli amepania kushughulikia akiingia
madarakani ni pamoja kubana matumizi ya serikali, kuongeza mapato ya
serikali kuboresha mfumo wa utendaji na ufanisi na kupitia kodi na
ushuru unaowaumiza wakulima, wafugaji na wavuvi.
Pia kupitia sheria za kubadilishwa, kuorodhesha kero za wananchi,
kuunda serikali ndogo, kumaliza kero za watumishi wa umma, utekelezaji
wa ilani ya CCM na kupendekeza muundo wa kitaasisi ili kutekeleza ahadi
ya kutoa Sh. milioni 50 kwa kila kijiji.
Waliowahi kuwa mawaziri wakuu ni pamoja na Julius Nyerere (1961-1962), Rashid Kawawa (1962 na 1972-1977)
Edward Sokoine (1977-1980, 1983-1984), Cleopa Msuya (1980-1983,
1994-1995), Salim Ahmed Salim (1984-1985), Joseph Sinde Warioba
(1985-1990), John Malecela (1990-1994), Frederick Sumaye (1995-2005),
Edward Lowassa (2005-2008) na Mizengo Pinda (2008-2015).
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa baada ya Dk. Magufuli
kuapishwa jijini Dar es Salaam Alhamisi (Novemba 5, 2015), jina la yule
atakayemteua kuwa Waziri Mkuu wake na kuliwasilisha bungeni ili lipigiwe
kura, litahusisha mtu mwenye sifa walau tisa zitakazoendana na
matarajio ya serikali yake.
UADILIFU
Ili Dk. Magufuli atekeleze ahadi zake na hasa ile ya kupambana na
ufisadi na rushwa, ni lazima awe na Waziri Mkuu asiyekuwa na chembe ya
kashfa, hasa zinazohusiana na rushwa.
Katika miaka ya hivi karibuni, ikiwamo ya awamu ya nne ya uongozi
wa nchi hii, kuliibuka kashfa kadhaa za ufisadi na rushwa kiasi cha
kuitikisa serikali ya Rais Jakaya Kikwete anayemaliza muda wake.
Kashfa hizo ni pamoja na ile ya uchotwaji fedha katika akaunti ya
Benki Kuu ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), ukodishwaji wa mitambo ya
umeme ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond, ripoti chafu ya Msimamizi
na Mkaguzi wa Fedha za Serikali (CAG) na ile ya ufisadi wa fedha za
akaunti ya Tegeta Escrow kwenye Benki Kuu (BoT).
Lowassa aliwajibika kufuatia kashfa ya Richmond mwaka 2008 wakati
Pinda alinusurika kwenye kashfa ya Escrow baada ya kusafishwa na Bunge.
Hali hiyo inafanya sifa mojawapo kubwa ya Waziri Mkuu ajaye kuwa ni
uadilifu na usafi wa kiwango cha juu, tena usiotiliwa shaka na yeyote.
UKANDA
Kwa kuwa Dk. Magufuli anatoka mkoa wa Geita, ambao uko Kanda ya
Ziwa, bila shaka Waziri Mkuu ajaye atakuwa na uwezekano mdogo wa
kuteuliwa kutoka katika kanda hiyo au zile za jirani.
Pamoja na ukweli kuwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi duniani ambazo
zimefanikiwa kupiga vita ukabila, lakini bado suala hilo limekuwa
likichukuliwa kwa tahadhari kubwa.
Wafuatiliaji wa masual ya siasa nchini, wanaamini Rais mteule, Dk.
Magufuli, ataangalia jiografia ya nchi na kuhakikisha kuwa msaidizi
wake mkuu wa shuguhuli za serikali anatoka sehemu nyingine ya nchi. Na
pia anatarajiwa, walau, kutotoka sehemu moja na Makamu wa Rais, Samia
Suluhu Hassan, ambaye anatokea Zanzibar.
KUJIAMINI, MTU WA MAAMUZI MAGUMU
Mtu anayetarajiwa kuwa Waziri Mkuu katika serikali itakayoongozwa
na Rais Dk. Magufuli anatakiwa kuwa na sifa ya kujiamini na uwezo mkubwa
wa kutoa maamuzi magumu pale inapobidi.
Kutokana na unyeti wa kazi yenyewe na changamoto zinazokabili taifa
kwa sasa, bila shaka Waziri Mkuu ajaye anapaswa kuwa mtu asiyeyumba.
Mathalani, umahiri wake unapaswa kudhihirika kwenye kipindi cha
maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu kwenye bunge na pale serikali
itakapokuwa na hoja za kujibu.
Kadhalika, kwa kuwa Waziri Mkuu ndiyo mtendaji mkuu wa serikali,
anatakiwa kutoa maamuzi magumu, hasa pale nchi itakapokuwa na masuala
nyeti yanayohitaji uamuzi makini na wa haraka.
ASIYEMZIDI RAIS MAGUFULI KWA UMAARUFU
Uzoefu unaonyesha kuwa watu wengi waliowahi kushika wadhifa wa
Waziri Mkuu ni wale wanaosifika kwa utekelezaji zaidi. Watu hawa
hutakiwa kutekeleza wajibu wao kwa weledi na umakini mkubwa, lakini bila
ya kumzidi Rais aliyeko madarakani kwa sifa au umaarufu.
Rekodi za nyuma zinaonyesha kwa mfano, nyota ya siasa ya Mwalimu
Nyerere ilikuwa juu kisiasa licha ya kufanya kazi na mawaziri wakuu
tofauti waliokuwa wachapakazi kwelikweli kama Kawawa, Sokoine, Msuya na
Salim.
Hata Warioba na Malecela waliposhika wadhifa huo kwenye awamu ya
pili chini ya Rais Mwinyi au Sumaye alipofanya kazi kwa miaka 10 na
Mkapa, bado nyota za marais wao zilikuwa juu.
UWEZO KUSIMAMIA UTEKELEZAJI
Sifa mojawapo ya Waziri Mkuu mpya chini ya Dk. Magufuli ni uwezo wa kusimamia na utelekezaji wa dhati wa mipango ya serikali.
Kwa mujibu wa Dk. Magufuli, yeye hana nafasi na mawaziri
wanaoendekeza kauli za ‘mchakato’, ‘tuko mbioni’ wala ‘tuko katika hatua
nzuri’, bali anachotaka ni vitendo zaidi katika utekelezaji. Siyo
blaablaa, na mwenyewe Magufuli amedhihirisha hilo katika utendaji wake
kwenye wizara mbalimbali alizowahi kuongoza, ikiwamo anayomaliza nayo
sasa ya Ujenzi.
Dk. Magufuli alijizolea sifa kubwa kutokana na utendaji wake, hasa
katika kusimamia ujenzi wa barabara sehemu mbalimbali nchini na bila
kusahau alipokuwa Wizara ya Ardhi na ile ya Mifugo na Uvuvi.
Waziri Mkuu mpya bila shaka atatakiwa angalau kufanana au kumzidi
Magufuli kutokana na ukweli katika serikali ijayo kuna mengi ya
kutekeleza.
Pia anatakiwa kuwa mtendaji mzuri kwani ana kazi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
KINARA WA KWELI SHUGHULI ZA SERIKALI BUNGENI
Tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania, miongoni mwa
viongozi wanaokumbana na changamoto kali za wapinzani bungeni ni
mawaziri wakuu.
Hawa ndio wamekuwa na kibarua cha kuwa vinara katika kukabili
shinikizo kutoka kwa wapinzani, hasa katika kufafanua masuala ya
utendaji.
Pia kuna kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu bungeni, ambacho pia ni aina nyingine ya ‘kitimoto’ kwa viongozi hawa.
Bila kusahau kumekuwa na kashfa na tuhuma nyingi zikiibuliwa dhidi
ya serikali, na hapo ndipo umahiri wa Waziri Mkuu huhitajika maradufu.
Ni kwa sababu yeye ndiye kioo cha serikali linapokuja suala la masuala
nyeti.
KUKUBALIKA NDANI, NJE CCM
Dk . Magufuli wakati akiteua Waziri Mkuu mpya, atalazimika kuwa na
mtu mwenye sifa hii ya kukubalika na kuheshimika ndani na nje ya CCM.
Hapaswi kuwa mtu mwenye kuzua maswali kwa jamii kutokana sifa na uzoefu
wake wa uongozi.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema mtu huyo, ndiye pia
atakayetoa taswira ya serikali ya Dk. Magufuli, hasa katika dhamira ya
kutekeleza ahadi zake na pia anatakiwa kulinda maslahi ya chama chake.
Anatakiwa kuwa mtu safi, ambaye jamii itakuwa na imani naye pale atakapochaguliwa kushika wadhifa huo.
MTU ASIYEWAZIA URAIS
Pamoja na dhamira njema ya Rais Kikwete ya kuwatumikia vizuri
Watanzania, lakini moja ya matatizo yaliyomkabili ilikuwa ni kitendo cha
baadhi ya mawaziri kuunda mitandao ya maandalizi ya urais kwa ajili ya
uchaguzi mkuu wa 2015.
Mara baada ya kuingia madarakani mwaka 2005, baadhi ya watendaji wa
serikali na wale wa CCM walianza kazi ya kuandaa mikakati na
kutengeneza mitandao ya kumrithi Rais Kikwete.
Mitandao hiyo ilisababisha kuporomoka kwa utendaji wa baadhi ya
mawaziri na mbaya zaidi, kulitokea kutoelewana na hata kuwapo kwa
migawanyiko ya wazi.
Kufuatia hali hiyo, kulizuka mtindo wa baadhi ya mawaziri kubaki na
kazi moja ya kuchafua wenzao huku wengine wakihangaika kujijenga
kisiasa badala ya kufanya kazi waliyotumwa na rais na matokeo yake
kushuka kwa utendaji katika baadhi ya wizara.
Hali hiyo ilisababisha CCM kuwaomba Rais mstaafu Mwinyi, aliyekuwa
Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Pius Msekwa na Katibu Mkuu wa CCM,
Abdulrahman Kinana, kufanya kazi ya kusuluhisha makundi ndani ya chama
hicho.
Ni dhahiri kuwa Waziri Mkuu wa serikali ya Dk. Magufuli atakuwa ni
mtu asiye na makundi wala asiwe na ndoto za wazi za kuwa mrithi wa Dk.
Magufuli kwa nafasi ya urais.
UZOEFU SERIKALINI
Dk Magufuli wakati anamteua Waziri Mkuu ajaye atapaswa kuangalia mtu mwenye uzoefu na masuala ya uongozi.
Waziri Mkuu kwa kawaida ndiye mtendaji mkuu wa serikali. Na ndiyo
maana ni muhimu akawa na uelewa mpana wa namna serikali inavyofanya kazi
na mifumo yake.
Serikali ina mfumo mpana, ambao bila ya mtu kuufahamu vizuri itakuwa ngumu kuongoza.
Mathalani, Waziri Mkuu anayemaliza muda wake, Mizengo Pinda, kabla
ya kushika wadhifa huo, alikuwa na uzoefu mkubwa wa utumishi serikalini
kwa kufanya kazi kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ikulu na
kuwa Naibu Waziri na waziri kamili wa masuala ya Tamisemi.
Pia mawaziri wakuu waliomtangulia waliwahi kushika nyadhifa
mbalimbali serikalini kabla ya kupata nafasi hiyo. Ni wazi kuwa Rais Dk.
Magufuli atazingatia eneo hili ili kumpata mtu makini atakayetimiza
dhamira ya kuwavusha Watanzania kutoka katika lindi la umaskini.
Kibarua hiki kiko kwa Rais Dk. Magufuli katika kuteua jina la mtu
anayeamini kuwa anamfaa kwa nafasi ya uwaziri mkuu na pia wabunge wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watakaofanya kazi ya kumpigia kura baada
ya kufikishiwa jina hilo katika kikao chao cha kwanza cha Bunge la 11.
Maoni
Chapisha Maoni