Afisa Maendeleo ya Jamii (W)
Ngorongoro, Teresia Irafay (wa pili kushoto) akiitambulisha meza kuu
kabla ya kumkaribisha Katibu Tawala wa Wilaya ya Ngorongoro, Lemuel
Kileo, (wa tatu kulia) kufungua kongamano la viongozi wa mila wa kabila
la wamasai (Laigwanan/Ngaigwanani) na wanawake Mashuhuri yenye lengo la
kushawishi uondoaji wa mila potofu zinazorudisha nyuma maendeleo katika
jamii za wafugaji. Kushoto ni Mtaalamu wa masuala ya vyombo vya habari
vya kijamii na Mkufunzi kutoka (UNESCO), Bi. Rose Haji Mwalimu, Kiongozi
wa Malaiboni wilaya ya Ngorongoro Bw. Sangau Naimodu (wa pili kulia)
pamoja na Katibu wa Baraza Mila (W) Ngorongoro, Laanoi Munge, (kulia),
Mwenyekiti wa Baraza la Malaigwanan wilaya ya Ngorongoro, Joseph
Oletiripai (wa tatu kushoto). (Picha zote na Zainul Mzige wa Modewjiblog).
Na Modewjiblog team
JAMII ya wafugaji imetakiwa kutumia
juhudi zao binafsi kubadilisha mawazo na imani ya jamii kwamba mila na
desturi hazibadiliki ili kutengeneza mfumo bora mpya unaothamini maisha
ya wanawake.
Wito huo umetolewa na Mtaalamu wa masuala
ya vyombo vya habari vya kijamii na Mkufunzi, Bi. Rose Haji Mwalimu
wakati akiwasilisha mada kwenye kongamano la viongozi wa mila wa kabila
la wamasai (Laigwanan/Ngaigwanan), Laiboni na wanawake Mashuhuri yenye
lengo la kushawishi uondoaji wa mila potofu zinazorudisha nyuma
maendeleo katika jamii za wafugaji.
Aliwataka washiriki wa warsha kusimama
kidete na kutumia elimu waliyoipata katika kushawishi jamii kubadilika
na kuachana na mila za ukekeketaji,ndoa za utotoni na pia unyanyasaji
mwingine wa kijinsia unaoonesha ubabe wa wanaume na mfumo dume.
Aliwataka wanajamii hao kutumia njia
mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari, rediojamii, vikao mbalimbali vya
kata na vijiji pamoja na nyumba za ibada kuhimiza watu kubadilika na
kuacha mila hizo za ukeketaji na kuozesha watoto katika umri mdogo.
Aidha Bi. Rose Haji Mwalimu katika
kongamano hilo lililoandaliwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni
la Umoja wa Mataifa, (UNESCO) amewataka wanawake kuvunja ukimya na
kuacha uoga na kuibua vitu vinavyowanyima haki zao za msingi.
KatibuTawala wa Wilaya ya Ngorongoro,
Lemuel Kileo akifungua kongamano la viongozi wa mila
(Laigwanan/Ngaigwanan na Laibon) pamoja wanawake mashuhuri lenye lengo
la kuondoa mila potofu zinazokwamisha maendeleo katika jamii za
wafugaji ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro.
Aliwataka wanawake kujitambua ili kutumia
sheria zinazowalinda kuondokana na unyanyasaji pamoja na ukatili wa
kijinsia unaoendelea katika jamii za kifugaji na kuwaomba viongozi wa
mila washiriki katika kuondoa mfumo dume.
Naye Ofisa Ustawi wa Jamii wa halmashauri
ya wilaya ya Ngorongoro, Benezeth Bwikizo, amesema kama watuw
atajitokeza na kueleza ukweli serikali itachukua hatua hasa ya kulinda
wanawake na watoto kupitia mamlaka iliyokabidhiwa na Katiba ya nchi.
Alisema kwa mujibu wa sheria Serikali ina
mamlaka ya kuhakikisha kwamba haki za watoto zinalindwa kupitia sheria
ya mtoto namba 21 ya mwaka 2009 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
kwamba mtoto lazima alindwe na apate haki zake zote za msingi.
Alisema pamoja na katika na sheria
zilizotungwa, mtoto pia analindwa na mkataba wa kimataifa wa haki za
mtoto wa Novemba 20, 1989 inayotoa ufafanuzi wa kulinda na kuhakikisha
kwamba haki za mtoto zinalindwa na kuheshimiwa.
Aliongeza kuwa pia ulindaji huo wa haki
za mtoto unakwenda sanjari na mkataba wa Umoja wa nchi za Afrika ya
mwaka 1990 unaotoa ufafanuzi juu ya haki za msingi za mtoto na namna
inavyotakiwa kuheshimiwa na kulindwa bila kuathiri haki zao.
Ofisa Elimu ya Uzazi na UKIMWI kutoka UNESCO, Mathias Herman akizungumzia malengo ya kongamano hilo kwa washiriki.
Bw.Bwikizo, alitaja haki za muhimu kwa
mtoto zinazotakiwa kulindwa na kuheshimiwa ili kuhakikisha mtoto anakua
katika malezi bora ni huduma za afya, chanjo, matibabu, Lishe na malezi
bora kupata haki ya kuishi, haki ya kuendelezwa na haki ya kulindwa.
Akizungumza katika ufunguzi wa kongamano
hilo, KatibuTawala wa Wilaya ya Ngorongoro, Lemuel Kileo, amelishukuru
Shirika la UNESCO kwa kuendesha mafunzo hayo ya kutoa elimu na kujenga
uwezo kwa viongozi wa mila na wanawake mashuhuri ili kuondoa mila potofu
katika jamii ikiwemo Ukeketaji, mimba za Utotoni na ndoa za umri mdogo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya,
Bw. Kileo aliwataka viongozi na washiriki wa warsha hiyo watumie nafasi
hiyo waliyoipata kwenda kufikisha ujumbe kwa jamii ili kupeleka
maendeleo mbele kwa kupunguza vifo vya akinamama na wasichana wenye umri
mdogo, kuondokana na ukeketaji pamoja na mimba za umri mdogo.
Mtaalamu wa masuala ya vyombo vya
habari vya kijamii na Mkufunzi kutoka UNESCO, Bi. Rose Haji Mwalimu
akisisitiza jambo kwa washiriki wa kongamano.
Kwa upande wa mmoja wa wakufunzi wa
warsha hiyo kutoka UNESCO akizungumzia malengo ya warsha hiyo, Ofisa
Elimu ya Uzazi na Ukimwi wa shirika hilo, Mathias Herman, amesema warsha
hiyo ni mwendelezo wa warsha zinazotolewa na UNESCO kwa ajili ya kutoa
elimu ya kuwajengea uwezo na kugawa majukumu kwa viongozi wa kimila
(Laigwanan), wa mama mashuhuri, viongozi wadini, wakunga wa jadi pamoja
na waandishi wa habari kufanya ufuatiliaji wa afya ya uzazi na malezi
bora kwa watoto.
Aliongeza kuwa UNESCO inatarajia mafunzo
hayo kutaleta mabadiliko kupitia nafasi ya viongozi hao mashuhuri katika
jamii kwa kuwa wanaaminika ili kushirikiana na wadau wengine wa
maendeleo wanaotoa mafunzo kuhakikisha kwamba suala la mimba za utotoni,
ndoa za utotoni pamoja na ukeketaji linafika mwisho katika jamiii ya
kifugaji.
Mwenyekiti wa Baraza la Malaigwanan
wilaya ya Ngorongoro, Joseph Oletiripai akisisitiza jambo kwa
Malaigwanan pamoja na wakina mama mashuhuri ambapo aliwataka watumie
nafasi waliyopewa na jamii na fursa ya elimu waliyopata kutoka kwa wadau
wa maendeleo UNESCO kuwa italeta mabadiliko na mpango chanya katika
jamii ya Kimasai.
Ofisa Ustawi wa Jamii wa wilaya ya
Ngorongoro, Benezeth Bwikizo (kuhoto) akizungumzia haki za watoto. Kulia
ni Mkalimani wa lugha ya Kimasaai Mchungaji Mark Murenga.
Mama Mashuhuri kutoka kijiji cha Olopiri, Nolarir Pashuku, akitoa maoni yake kwenye kongamano.
Mmoja wa washiriki katika warsha hiyo ambaye ni Laigwanan , John Olekulinja kutoka kata ya Malambo akizungumzia mafunzo hayo.
Kiongozi wa Malaiboni wilaya ya Ngorongoro Bw. Sangau Naimodu (katikati) akieleza namna inavyofaa kueneza elimu ya mabadiliko.
Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto,
tarafa ya Loliondo (W) Ngorongoro, Bi. Nailejileji Joseph akitoa elimu
ya uzazi wa mpango kwa washiriki wa kongamano hilo.
Pichani juu na chini ni viongozi wa
mila wa kabila la wamasai (Laigwanan/Ngaigwanan), Laiboni na wanawake
Mashuhuri walioshiriki kwenye kongamano hilo yenye lengo la kushawishi
uondoaji wa mila potofu zinazorudisha nyuma maendeleo katika jamii za
wafugaji lilioandaliwa na Shirika la UNESCO.
Maoni
Chapisha Maoni