MCHANGO WA LOWASSA NDANI YA UKAWA BAADA YA KUTIMKIA HUKO
Aliyekuwa mgombea urais wa
Chadema aliyeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward
Lowassa ameupa umoja huo ushindi wa viti 116 vya wabunge katika Bunge la
kumi na moja litakaloanza Novemba 17, Mjini Dodoma.
Idadi
hiyo ya wabunge ndiyo kubwa kuwahi kufikiwa na upinzani tangu
kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 na tangu kufanyika kwa
uchaguzi wa kwanza wa ushindani wa vyama mwaka 1995.
Idadi
ya wabunge wa Ukawa imeongezeka baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC) jana kukamilisha kazi ya kuwateua wabunge wa viti maalumu ambao
orodha yake itawasilishwa kwenye vyama husika.
Katika
uchaguzi wa mwaka huu uliohusisha majimbo 258 kati ya 262, CCM imeshinda
ubunge katika majimbo 188, CUF 35, Chadema 34, NCCR–Mageuzi kiti
kimoja. NLD haikupata kiti wakati ACT – Wazalendo ilipata kiti kimoja.
Idadi wa wabunge wa Ukawa inatokana na jumla ya wabunge wa vyama vinavyounda umoja huo ambavyo ni Chadema, CUF na NCCR.
Akizungumza
na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva alisema
CCM imepata viti maalumu 64, Chadema 36 na CUF 10.
“Vyama
vingine havijapata wabunge wa viti maalumu kwa sababu havikufikisha
asilimia tano ya kura za wabunge kwenye majimbo, kwa mujibu wa Katiba,”
alisema Jaji Lubuva.
Kwa hesabu hiyo, Chadema
imefikisha wabunge 70 kutoka 48 wa mwaka 2010, CUF ina wabunge 45
kutoka 36 wa mwaka 2010 wakati NCCR-Mageuzi imeshuka kutoka wabunge
wanne wa 2010 hadi mmoja na kufanya idadi ya wabunge wa Ukawa kuwa jumla
116. CCM imefikisha wabunge 252.
Lubuva alisema jumla
ya wabunge wa viti maalumu waliopatikana kwenye vyama vyote ni 110 kati
ya 113 wanaotakiwa na watatu wanaosalia watapatikana baada ya kufanyika
uchaguzi ambao uliahirishwa kwenye majimbo manane kutokana na sababu za
vifo vya wagombea sita na kasoro mbalimbali katika majimbo mawili.
Majimbo
ambayo wagombea walifariki dunia ni Masasi, Ludewa, Lushoto, Ulanga
Mashariki, Arusha Mjini na Handeni Mjini wakati majimbo yenye kasoro ni
Lulindi na Kijitoupele.
Jaji Lubuva alisema CCM imepata
idadi hiyo ya wabunge wa viti maalumu baada ya kupata jumla kura
8,333,955 za wabunge, Chadema kura 4,627,923 za wabunge na CUF kura
1,257,955.
Kwa matokeo hayo, vyama 19 kati ya 22
vimeambulia patupu baada ya kupata kura zisizozidi asilimia tano ya kura
zote halali za wabunge.
Jaji Lubuva alisema: “Tumetoa
matokeo ya wabunge wa viti maalumu baada ya kupewa mamlaka kikatiba ya
kutangaza wabunge wa viti maalumu vya wabunge wanawake visivyopungua
asilimia 30 ya wabunge wote.”
Alisema kwa mujibu wa
uamuzi wa Serikali wa mwaka 2010, idadi ya wabunge wanawake wa viti
maalumu iliongezwa na kufikia asilimia 40, ambayo pia imetumika katika
uteuzi wa mwaka huu.
“Haya yote ni kwa mujibu wa Ibara
ya 66 Kifungu cha (1) na (b) na Ibara ya 78 ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano ya Tanzania ya mwaka 1977, ikisomwa kwa pamoja na Kifungu 86A
cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343,” alisema Jaji Lubuva.
Kauli za vyama
Akizungumzia
matokeo hayo, Kiongozi wa ACT - Wazalendo, Zitto Kabwe alisema chama
chake kimefikisha asilimia 4 tu ya kura za wabunge, hivyo hakikutimiza
vigezo vya kupata wabunge wa viti maalumu.
“Napenda
kupongeza vyama vyote vilivyotimiza takwa la kisheria na hivyo kupata
viti vya ubunge. Kwa namna yoyote, ile demokrasia ya Bunge imeimarika
kwa idadi ya wabunge wa upinzani kuongezeka,” alisema na kuongeza:
“Sisi
ACT – Wazalendo tumepata tunachostahili na kazi iliyo mbele yetu sasa
ni kujenga chama kama taasisi imara na kufanya siasa za masuala.
Tutatumia kiti kimoja tulichopata na madiwani 50 tuliopata nchi nzima na
Manispaa ya Kigoma tutakayoongoza kuhakikisha tunaonyesha tofauti yetu
na vyama vingine.”
Maoni
Chapisha Maoni