Bonde la Ufa lajitokeza Chemba,wataalamu waombwa kuja kuchunguza,hofu yatanda














Bonde la Ufa lajitokeza Chemba  
·        kaya 30 zakosa makazi, nyumba zaanguka
·        Familia 162 zatakiwa kuhama
·        Mamia wamiminika kushuhudia mipasuko hiyo

NA. MOHAMED HAMAD
Bonde la Ufa limejitokeza kitongoji cha Bomba Kijiji cha Olboloti Wilayani Chemba Mkoani Dodoma, na kusababisha taharuki kwa familia 16 kukimbia makazi yao na kuomba hifadhi nje ya eneo hilo baada ya kutokea mipasuko mikubwa kwenye nyumba zao na ardhini 

Jumla ya kaya 162 zinatakiwa kuhama katika eneo hilo ambalo kwa sasa kuna mipasuko mikubwa ambayo inafanya mamia ya wananchi kutoka katika maeneo mbalimbali kushuhudia huku wengine wakisema kuwa ni maajabu yaliyotokea na kuwataka wataalamu kuja kushuhudia

Akizungumza na wananchi wa Kitongoji cha Bomba  Bw.Gabriel Mbogoni wakala wa Jiolojia Tanzania chini ya Wizara ya Nishati na Madini Dodoma alisema utafiti wa awali unaonyesha kuwa eneo hilo liko kwenye ukanda wa Bonde la ufa

Alisema tabia ya bonde la Ufa huwa kuna mipasuko mingi inayojitokeza chini ya ardhi ambapo juu sio rahisi kuiona na mara baada ya kujitokeza ndipo mwonekano wake unajitokeza tena ukiwa na madhara  makubwa kama yalivyojitokeza katika eneo hilo

Alisema moja ya sababu ya mipasuko hiyo ni kushuka kwa kina cha maji, na baada ya mvua kunyesha kwa kiasi kikubwa maji yalipenya na kufuata nyufa kisha kuchukua udongo wa juu na kwenda nao chini ya ardhi ambapo madhara yake ni mipasuko iliojitokeza

“Ningeshauri wananchi mhame katika eneo hili kabla ya madhara hayajajitokeza, tafuteni eneo lingine kwaajili ya makazi yenu, hapa hapafai tena kuishi kwani mko kwenye ukanda wa Bonde la ufa mtazidi kuona mipasuko ikiendelea ambayo itasababisha kamazi yenu kuharibika”

Kwa mujibu wa Abdala Suti Mwenyekiti wa Kijiji cha Olboloti alisema chanzo cha tukio hilo ni kunyesha mvua kubwa siku hiyo kwa masaa matano mfululizo na kusababisha kutuama maji mengi ambapo ghafla yalizama chini na kutokea mipasuko hiyo

Alisema akiwa nyumbani kwake alipata taarifa kwa wananchi waliopata hofu kuona hali hiyo wakimtaka afike na kuwasiliana na mamlaka za Serikali kwaajili ya kufanya uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo ambalo liliibua husia tofauti za watu baada ya kuona mipasuko hiyo

“Nilipofika nilishuhudia mapango makubwa ndani ya ardhi kila aliyeona alibaki kumshukuru Mungu kwani mingine ilijitokeza ndani ya nyumba za watu na hata mtu angetumbukia asingeweza kuonekana kulingana na ukubwa wa mapango hayo”alisema Mwenyekiti huyo

“Ndugu zangu wananchi utata uliokuwa umejitokeza baada ya kuona mipasuko hii kila kona ya maeneo yetu, sasa wataalamu wamefika wameshauri hapafai kuishi ni vyema tukawa wasikivu ili tuepushe maisha yetu”alisema Mwenyekiti Suti

Alisema Serikali ya Kijiji itahakikisha kuwa wananchi wa maeneo hayo wanapatiwa maeneo mengine kwaajili ya makazi, tofauti na maeneo hayo ambayo kwa sasa hayatakiwi kuishi binadamu kutokana na kuibuka kwa mahandaki na mipasuko hiyo

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo alitaja baadhi ya nyumba ambazo wananchi waliridhia kuhamia kwenda kuomba hifadhi kwa ndugu na jamaa zao kuepuka madhila hayo kuwa ni pamoja na Adamu Iddi Ndalo,Aisha Siraji,Habibu Waziri,Salum Manyehe na Godson Loilole

Wengine ni Adamu Cheru,Bakari Mchana, Mtu mmoja aliyejulikana nkwa jina la Turuku,Issa Binge,Henedi Kiberenge,Rama Mrangi,Iddi Ramadhani,na Sarah Adam ambao kwa pamoja wamedaiwa kuwa watapata maeneo mengine kwaajili ya kuanzisha ujenzi upya

HOFU KWA WANANCHI
Hofu imetanda kwa wananchi wa eneo hilo baada ya kuona mipasuko mingi ikizidi kujitokeza wasijue cha kufanya huku wengine wakianza kuhamisha familia zao kwenda kuhifadhiwa kwa ndugu na jamaa zao wakidai hata kama watalazimishwa kuishi humo hawako tayari

Nilichojionea siwezi kuelezea nendeni kwangu mpasuko uliotokea zaidi ya watu kumi wanaweza kutumbukia na wasionekane na hapo ndipo kulikuwa na kitanda changu kwakuwa nimenusurika basi bora niondeke hapo alisema Adamu Cheru

Naye Godson Loilole aliitaka Serikali ya Kijiji hicho kuwa pamoja na kuwapatia maeneo mapya kwaajili ya kuanzisha ujenzi, huku akisisitiza kuwa eneo hilo lipimwe pasitokee tukio la namna hiyo kwani kwakuwa hakuna aliyepoteza maisha wachukue tahadhari

Alisema mbali na kuahidiwa kupewa maeneo mengine ya makazi utazamwe upya utaratibu wa kuwafidia waathirika kwani wengi wao walijenga nyumba za gharama ambazo kwa sasa hawawezi kuishi humo kutokana na mipasuko hiyo

“Huwezi kusema tu ondokeni na kupewa maeneo mengine nani atalipa gharama tulizotumia kujenga nyumba zetu, kwanini Serikali hamkufanya utafiti wa kina kujua kama eneo hilo halifai kuishi watu?”alihoji huku akidai kuwa atadai haki zake hata mahakamani

Kwa upande wake Juma Kidevu (mwananchi) alisema kuna kila sababu ya kufanyika utafiti wa kina, kupimwa maeneo hayo kuona kama yanafaa kwa makazi ya binadamu ili kuepukana  na changamoto za kimaisha kama hizo zilizojitokeza

Alizitaka mamlaka za Serikali na zisizo za kiserikali kufanya tafiti za kina juu ya tukio hilo kwani madhara kama hayo yaliweza kujitokeza katika meneo mbalimbali lakini hakuna aliyebaini na kusaidia ili wananchi wachukue tahadhari

Kwa upande wake Idi Ibrahimu msuya (mwananchi) alisema akiwa nyumbani kwake siku hiyo aliona maji mengi yakiingia ndani ya nyumba kisha kuitaka familia yake kutoka nje , ambapo hapo aliona kila kaya wakipiga mayowe kuomba msaada kutokana na maji hayo

Alisema ghafla maji hayo yalizama chini ya ardhi, huku nyumba yake ikionekana kuwa na mpasuko ambao ulimpa shaka kisha kwenda kwa majirani ambapo hapo alizidi kushuhudia mipasuko ya nyumba za jirani ikiongezeka na ndio wakajua kumbea eneo hilo lina matatizo

Wadau wa matukio
Naye Gabriel Tuke mdau wa matukio yanayojitokeza ardhini na angani na Mratibu wa shirika lisilo la kiserikali la SWEAT linalofanya kazi ya matumizi bora ya ardhi Kiteto alisema yaliyotokea Ololoti hayapaswi kupuuzwa kwani ndio yanayoendelea kujitokeza nchi zilizoendelea kama Mexico

Alisema wanasayansi kutoka vyuo mbalimbali hapa nchini wanapaswa kuonyesha uwezo wao wa kielimu kupitia tukio hilo kueleza kilichojitokeza na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wananchi ili waweze kujilinda wasiweze kupata madhara zaidi

Kwa upande wa baadhi ya wananchi hao akiwemo Aisha Siraji,Godson Loilole Adamu Cheru na Iddi Ramadhani walisema wako tayari kuondoka kupisha madhara yanayoweza kujitokezana na kuitaka Serikali kufanya uchunguzi wa kina katika maeneo waendako kama yako salama

“Tumejionea haijawahi kutokea uko ndani uasikia maji yanaunguruma chini ya ardhi huku ukishuhudia nyumba inavyopasuka sambamba na ardhi, toka dunia iumbwe haijapata tokea hili ni geni sana katika maeneo haya”alisema Mzee Cheru

Katika hatua hiyo wananchi hao wameitaka Serikali kufanya utafiti wa kina na wakitaalamu kujua juu ya ardhi katika maeneo hayo ambayo inaonekana kuwa na dalili za madini ya aina ya chokaa wakidai yanaweza yakawasaidia kwa siku za usoni

Baadhi ya wananchi waliozungumza na MTANZANIA walisema kwa muda mrefu wamekuwa wakichimba eneo hilo na kutumia udongo huo kama chokaa wasijue na kuitaka Serikali kutuma wataalamu kuja kufanya utafiti huo mwafaka kwa hivi sasa


Mwishi

Maoni