TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
1. Sintofahamu katika chaguzi za kuwapata wenyeviti/makamu wenyeviti wa halmashauri na Mameya/manaibu meya katika maeneo ambayo UKAWA umeshinda.
2. Ukandamizaji wa demokrasia jimboni kwa Waziri Mkuu.
Kumekuwa na kila dalili za uminywaji na ukandamizaji mkubwa wa demokrasia katika maeneo yote ambako vyama vinavyounda UKAWA vimeshinda idadi kubwa ya madiwani na kuwa na uhalali wa kuongoza halmashauri/manispaa au jiji.
Kilichotokea katika uchaguzi wa kumpata Meya wa Jiji la Tanga juzi Jumamosi, Novemba 19, 2015 ni mwendelezo wa njama na hujuma za makusudi zinazopangwa na watawala wakiwatumia wakurugenzi na vyombo vya dola, kwa namna ile walivyofanya wakati wa Uchaguzi Mkuu, kupora haki za raia Watanzania wanyonge walioamua kuchagua UKAWA, wakiamini katika mabadiliko ya kweli dhidi ya maneno tupu ya CCM.
Hujuma za namna hiyo za watawala ndizo zimefanyika maeneo mengine ambayo wananchi wamechagua UKAWA uwaongoze, mf; Kyerwa-Kagera, Kilombero, Ilala, Kinondoni n.k ambako hadi sasa uchaguzi bado uko kwenye sintofahamu kubwa kwa kile ambacho kinaonekana wazi ni kutaka kuibeba CCM kwa nguvu baada ya kuwa imekataliwa na wananchi katika maeneo husika.
Ni suala linalofikirisha sana kwamba hujuma hii dhidi ya demokrasia ambayo kimsingi ni ubabe dhidi ya wananchi waliotumia haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi wanaowataka, inafanyika huku Ofisi ya Rais, ambayo ndiyo inasimamia Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa kupitia Wizara ya TAMISEMI, ikiwa kimya jambo ambalo linaashiria mambo matatu;
1. Kuwa sintofahamu inayosababishwa na hujuma hizo ni matokeo ya maelekezo au ina baraka kutoka ofisi hiyo.
2. Wizara hii tayari imemshinda Rais John Magufuli kiasi cha watendaji walio chini yake, hususan Wakurugenzi kujifanyia mambo kadri wanavyotaka kwa ajili ya kuibeba CCM, jambo ambalo ni kero nyingine kwa wananchi katika maeneo mbalimbali. Vinginevyo ni vigumu kuelewa kwamba mathalani hadi sasa takriban mwezi mzima na zaidi eti Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeshindwa kumpata DED wa Halmashauri ya Kyerwa, Kagera (au DED huyo amegoma) ili tu athibitishe kama kweli CHADEMA ina madiwani wengi kuliko CCM ambayo ina madiwani wachache lakini 'imezawadiwa' na NEC madiwani wengi wa Viti Maalum, kinyume kabisa na utaratibu, ili kuongeza kura za hujuma kisha iongoze Halmashauri ya Kyerwa badala ya CHADEMA ambayo ndiyo yenye madiwani wengi.
3. Mganga hajigangi, hivyo Rais Magufuli ameshindwa kutumbua jipu ambalo liko ofisini kwake. Kushindwa kusimamia shughuli zilizoko chini ya TAMISEMI, tena nyeti kama hiyo ya kuwapata viongozi wa serikali za mitaa watakaosimamia shughuli za maendeleo ya wananchi katika maeneo wanayoishi, ni jipu kubwa linalohitaji mtumbuaji. Tunataka kujua nani atakuwa anatumbua majipu yanayobainika kupewa nafasi ofisini kwa Rais?
2. Uminywaji wa demokrasia jimboni kwa Waziri Mkuu.
Siku ya jana na leo tumepata taarifa kutoka kwa viongozi wa chama katika maeneo ya Jimbo la Ruangwa ambalo anatokea Waziri Mkuu Majaliwa Kasimu Majaliwa, kuwa kumekuwa na operesheni ya kushusha bendera na kuvunja vijiwe (ngazi ya misingi) vya CHADEMA hasa katika maeneo ya Nandagala, Mnacho n.k.
Mbali ya kusikitishwa na jambo hilo, tunalaani vikali hatua hiyo ambayo tumeambiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Mkurugenzi kwenda kwa Watendaji wa Mitaa, Vijiji na Kata, hususan wakati huu ambapo Waziri Mkuu yuko ziarani Mkoa wa Lindi ambayo itamfikisha nyumbani, huko Ruangwa.
Tunawataka watendaji wa Serikali katika eneo hilo kuacha mara moja ukiukwaji huo wa demokrasia hasa kwa kukilenga CHADEMA huku wakiacha CCM ikiendelea kufanya kazi zake za kisiasa.
Tunatoa wito kwa Waziri Mkuu kuona fahari demokrasia ikishamiri katika jimbo lake na yeye akubalike kwa uhalali wa kisiasa kutokana na kukubalika kwake kwa wananchi badala ya vitisho kutumika kuua ushindani wa demokrasia ya vyama vingi kwa kuhujumu chama kinachoonekana kutishia uwepo wa CCM jimboni na hata nyumbani kwake. Tunamuomba asiache kumbukumbu mbaya kama ya aliyemtangulia, Mizengo Pinda, ambaye baada ya kuona CHADEMA ina ushawishi mkubwa katika mtaa wa nyumbani kwake hapa Dar es Salaam na hata kijijini kwao huko Katavi, aliingilia uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka jana ili tu atangazwe Mwenyekiti wa Mtaa anayetokana na chama chake hata kama hakupewa ushindi na wananchi.
Tunaamini kuwa kama demokrasia ni moja ya misingi muhimu kwa maendeleo ya taifa lolote, viongozi wa serikali wanapaswa kuwa watu wa kutiliwa mfano kuiheshimu kwa maslahi mapana ya Watanzania na hawataweka matakwa ya CCM mbele.
Imetolewa leo Jumatatu, Desemba 21, 2015 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA
Maoni
Chapisha Maoni