Askari Polisi aporwa SMG Kiteto



                                              IGP Ernest Mangu


·       Ni baada ya kumwokoa mtuhumiwa wa wizi asiuawe

MOHAMED HAMAD KITETO
Askari Polisi namba H.3068 PC Ginwe wa kituo cha Kibaya wilayani Kiteto mkoani Manyara, amenusurika kifo na kuporwa silaha aina ya SMG pamoja na risasi zake  mnada wa Dosidosi uliopo Kijiji cha Dosidosi wilayani humo akituhumiwa  kumtorosha mwizi aliyekuwa auawe na watu wenye hasira kali.

Tukio hilo limetokea majira ya saa saba mchana Kijijini hapo  ambapo mtuhumiwa alidaiwa kumpora mmoja wa wachuuzi wa ng’ombe fedha taslimu tsh laki nane alizouza ngombe kisha kukimba na baadaye kukamatwa na kuanza kushambuliwa kwa silaha za jadi

Wakati mtuhumiwa akishambuliwa na watu wenye hasira kali askari waliokuwepo wakilinda mnada huo walijitokeza na kutaka kumwokoa kwa kupiga risasi za moto juu ili wasiweze kumdhuru bila mafanikio na ndipo  wakatafuta gari aina ya noah na kumpakia haraka na kumkimbiza kwenda Kibaya makao makuu ya wilaya ya Kiteto

Askari PC. Ginue katika mazingira ya kumwokoa aliachwa na gari hilo lililokuwa linamtorosha mtuhumiwa ambapo hapo alianza kushambuliwa na baadhi ya jamii ya kifugaji waliomtuhumu kumtorosha mhalifu waliyetaka kumuua kwa kosa la wizi.

Katika hatua hiyo askari huyo alijeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake kisha kunyang’anywa silaha aina ya SMG na watu ambao hawakujulikana kisha kutokomea nayo kusiko julikana

Kwa mujibu wa Juma Maganga Afisa Mtendaji wa Kata ya Dosidosi alisema jitihada za kuwatafuta watu waliohusika na tukio hilo zinaendelea na kwamba watu watatu akiwemo askari polisi wamejeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya wilaya ya Kiteto kwa matibabu zaidi.

Kwa mujibu wa askari mmoja ambaye hakutaka kutajwa majina yake gazetini alieleza MTANZANIA kuwa
Afisa wa upelelezi wa makosa ya jinai wa mkoa wa Manyara aitwaye Justine Masejo amelazimika kuanza safari kwenda Kiteto kwaajili ya tukio hilo.

Kanali Samuel Nzoka Mkuu wa Wilaya ya Kiteto amekiri kutokea tukio hilo na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano kuwakamata watu waliohusika kupora silaha hiyo ambayo alisema ni kosa la jinai na kwamba wanapaswa kuirejesha silaha hiyo mara moja.

Alisema kitendo cha wananchi kujichukulia  sheria mkononi hakifai, na kuwataka wafuate sheria za nchi kuwa chombo pekee cha kutoa haki ni mahakama na sio kuanza kupigana na kusababisha madhara

“Haifurahishi hata kidogo kusikia raia anamnyang’anya askari silaha kali kama SMG anakwenda nayo wapi kama sio naye ni mhalifu”alisema Kanali Nzoka huku akiapa kuwa lazima silaha ipatikane na wahusika kufikishwa mahakamani

Mwisho.

Maoni