MAJIPU HATARI




jipu hatari 
 

NA CHRISTINA GAULUHANGA, DAR ES SALAAM
SERIKALI imebaini madudu ndani ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) na kuamua kuwasimamisha kazi wakurugenzi wakuu wanne, baada ya kupitia ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2013.

Wakurugenzi hao wameng’olewa kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo uzembe uliosababisha mabilioni ya fedha za bodi hiyo kupotea.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam  jana, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, alisema hatua hiyo imekuja kutokana na ripoti ya uchunguzi uliofanywa mwaka 2013 ambayo ilibani upotevu mkubwa wa fedha na ukosefu wa umakini wa usimamizi.

Aliwataja wakurugenzi hao kuwa ni pamoja na Mkurugenzi Mtendaji aliyestaafu, George Nyatega ambaye
alikuwa akifanya kazi kwa mkataba wa miaka miwili, ambao ungemalizika Agosti 31.

Alisema mkurugenzi huyo mkataba wake umesitishwa rasmi kuanzia jana na atalipwa mshahara wa mwezi mmoja kama notisi kulingana na kifungu cha 50(3)(a) cha kanuni za kudumu.

Wakurugenzi wengine waliotumbuliwa majipu ni Yusuph Kisare (Fedha na Utawala), Juma Chagonja (Urejeshaji Mikopo) na Onesmo Laizer (Upangaji na Utoaji Mikopo).

Profesa Ndalichako alisema ukaguzi wa ndani wa mikopo ya wanafunzi kuanzia mwaka 2013 hadi 2016, ulibaini upungufu kadhaa na aliwaandikia HESLB kujibu tuhuma hizo, lakini walishindwa kutoa maelezo yoyote hadi walipoandikiwa barua na Wizara ya Elimu ya kutaka majibu ya ripoti hiyo.

“Cha kushangaza watendaji wa bodi hii walikabidhi majibu Februari mosi, mwaka huu. Baada ya kujibu tuhuma zinazowakabili wamemtupia lawama Mkaguzi Mkuu wa ndani wa Serikali kwa madai taarifa yake haikukidhi viwango, imejikita katika ‘Operational Audit’, wakati kazi hii hufanywa na mkaguzi wao wa ndani,” alisema Profesa Ndalichako.

Alisema HESLB ilijaribu kutoa ufafanuzi wa baadhi ya udhaifu ulioibuliwa na mkaguzi na kujibu hoja za baadhi ya maeneo.

RIPOTI YA CAG MWAKA 2013
Profesa Ndalichako alisema katika ripoti hiyo, wanafunzi 23 walipata mikopo kupitia vyuo viwili tofauti (havikutajwa) kipindi cha miaka mitatu mfululizo wakilipwa Sh 153,999,590 chuo cha kwanza na Sh 147,541,460 chuo cha pili.

Alisema wanafunzi 169 walipata mikopo kupitia vyuo viwili tofauti kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo, ambapo katika chuo cha kwanza walilipwa Sh 658,047,570 na chuo cha pili walilipwa Sh 665,135,716.

Profesa Ndalichako alisema wanafunzi 343 wasiokuwa na usajili kwenye vyuo husika walilipwa Sh 342,468,500 na wanafunzi 55 walioacha masomo walilipwa Sh 136,232,800.

Aliongeza kuwa jumla ya Sh 159,664,500 zililipwa kwa wanafunzi 306, zaidi ya kiwango kilichoainishwa kwenye vipengele namba 4.3 na 4.3.2 vya miongozo ya upangaji na ukopeshaji ya mwaka 2008/09 na 2009/2010.

“Miongozo mingine ni vipengele namba 4.6 na 4.3.1 vya miongozo ya upangaji na ukopeshaji mikopo ya mwaka 2008/2009 na 2009/2010 hadi 2010/2011, jambo ambalo ni kinyume na sheria,” alisema Profesa Ndalichako.

Alisema wamebaini wanafunzi 77 walipatiwa mikopo kwenye vyuo vya ndani na nje ya nchi kwa wakati mmoja, ambao walitumia Sh 467,620,654 kwa vyuo vya nje na Sh 123,047,119 kwa vyuo vya ndani.

Waziri huyo alisema wanafunzi 19,348 walipata mikopo bila kupitishwa na Kamati ya Mikopo, jambo ambalo ni kinyume na kanuni namba 8 ya Kanuni za Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu.

“Wanafunzi 54,299 walipangiwa mikopo wakati hawakuomba na kiasi cha Sh 207,052,650 hazikuchukuliwa na wanafunzi husika, lakini cha ajabu  hazikurejeshwa kwenye bodi kinyume na Hati ya Makubaliano (MOU) kifungu 3.3.4 (b) na (c),” alisema.

Alisema uzembe mwingine ni wanafunzi 143 kulipwa mikopo kwa miaka mitatu bila kusajiliwa, hali ambayo ilisababisha Sh 173,641,700 kulipwa kinyume na taratibu.

Profesa Ndalichako alisema kutokana na madudu hayo ndani ya wizara yake ambayo amefanya kazi siku 50 tu hadi jana, ameamua kuwasimamisha kazi wakurugenzi wa bodi hiyo waliohusika kwa namna moja ama nyingine.

“Wizara itateua maofisa watakaoshika nafasi hizo kwa muda hadi uchunguzi utakapokamilika na wakurugenzi wa bodi hiyo kuchukuliwa hatua stahiki,” alisema Profesa Ndalichako.

Alisema wizara yake imeridhika na kuona ukweli kuwa kuna utendaji usioridhisha kwenye taasisi hiyo na kusababisha matatizo yanayojirudia kwa wateja wao.

Profesa Ndalichako alisema wizara yake haitawafumbia macho watendaji wote ambao wanashirikiana kwa namna moja au nyingine na watumishi wa HESLB kuchelewesha fedha za wanafunzi, ikiwa ni pamoja na kuzitafuna.

Alisema vipo viashiria vinavyoonyesha tabia za wazi kwa baadhi ya wakuu wa vyuo ambao wamekuwa wakishindwa kulipa mikopo hiyo kwa wakati na mara baada ya wizara kufuatilia, fedha hizo zimekuwa zikilipwa.

Akitolea mfano wa vyuo hivyo na kutoa onyo kali kuwa ni pamoja na Chuo Kikuu cha St. Joseph (Songea), St. Joseph (Arusha), Chuo Kikuu cha Dodoma ambavyo vilifunguliwa  Novemba 2015 na malipo kufanywa Januari 2016 yaani miezi mitatu au miwili baadaye.

Alisema wanafunzi wanaosoma nje ya nchi kama Algeria, Ujerumani na Msumbiji ambao Serikali kupitia HESLB inatakiwa kuchangia baadhi ya gharama, wamekuwa wakiendelea kulipwa licha ya muda wa mkataba kumalizika.

“Hawa wanafunzi wa nje, mfano Algeria wamekuwa wakiendelea kulipwa fedha wakati mkataba wao umekwisha baada ya miaka minne, wameendelea kulipwa hata miaka saba, huku wengine wakiendelea na kozi nyingine tofauti,” alisema Profesa Ndalichako.

Maoni