MTENDAJI KITETO ASTAAFU KUHOFU KUTUMBULIWA

Tokeo la picha la Tamimu Kambona Mkurugenzi mtendaji wa Kiteto Tamimu Kambona katika moja ya vikao vya kazi

NA. MOHAMED HAMAD
MTENDAJI wa Kijiji cha Namelock, Kata ya Partimbo, Wilayani Kiteto,
Mkoani Manyara, Ally Zuberi Panjapi, ameomba kustaafu kwa hiyari
nafasi yake, kufuatia kasi ya Rais John Pombe Magufuli, ya hapa kazi
tu, kuhofia kutumbuliwa.

Akizungumza baada ya kuandika barua ya kuacha kazi kwa hiyari,
Mtendaji huyo alisema, ametumikia Taifa kwa muda mrefu, akiwa
mzalendo, anatamani kuwa huru na kuachia nafasi akiwa timamu akilenga
kupata mafao yake.

“Kwa hii kasi ya Rais wetu, nafasi hizi hazitabiriki, ukiona mtu
karudu nyumbani salama, shukuru Mungu kwani kuna changamoto nyingi
ambazo zinaweza kumsababishia mtu akafukuzwa kazi na kukosa mafao yake
aliyotumikia nchi kwa muda mrefu”.

Alisema hakuna anayekataa kufanya kazi, isipokuwa umri aliofikia ni wa
kustaafu kwa hiyari, akidai haoni sababu ya kuhatarisha kazi yake
kutokana na kasi hiyo ambayo imekuwa tishio kwa wafanyakazi wengi hapa
nchini.

Awali mtendaji huyo amedai kufanya kazi katika maeneo mbalimbali
Wilayani Kiteto, akisema amekumbana na changamoto nyingi, ambazo
zimemfanya aone kuwa sasa basi kazi hiyo ili afanye na kazi zake
binafsi.

Taarifa za uhakika kutoka Ofisi ya Utumishi, katika Halmashauri ya
Wilaya ya Kiteto ni kwamba, barua ya mtumishi huyo imepokelewa na
hatua za kisheria zinaendelea, ili aweze kupata haki yake kama
alivyokusudia.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmshauri ya Wilaya ya Kiteto Tamimu Kambona,
amekiri kupokea taarifa hiyo ya kimaandishi na kuwataka watumishi
wengine kufanya kazi kwa uadilifu hadi watakapostaafu kabla ya kupata
matatizo kwa uzembe kazini.

Mwisho.

Maoni