WAZIRI
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ametoa miezi
mitatu kwa Bodi mpya ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kusuka upya
uongozi uliopo ili kuweza kuleta ufanisi wa utendaji kazi wa Shirika
hilo.
Akizungumza
jijini Dar es salaam mara baada ya kuitambulisha Bodi hiyo, Waziri
Mbarawa amesema kuwa Uteuzi wa Bodi hiyo utasimamia kuleta tija na
ufanisi wa shirika hilo ambalo kwa kipindi kirefu lilikuwa na changamoto
nyingi.
“Nataka
kuona mabadiliko makubwa kuanzia kwenye Menejimenti hadi uongozi wa
chini, hakikisheni mnaweka uongozi amabao utafuata maadili, utakuwa na
ufanisi, ubunifu na kasi katika utendaji kazi” amesema Profesa Mbarawa.
Aidha,
ameitaka Bodi hiyo kusimamia na kuboresha mpango wa kibiashara wa
usafirishaji (Business Plan) katika Shirika hilo ili kuweza kumudu soko
la ushindani na kuweza kuongeza mapato ya Shirika hilo.
“Kama
mnavyojua usafiri wa anga una ushindani mkubwa, hivyo ili Serikali
iweze kupata faida katika biashara hii ni lazima tuboreshe mpango wa
kibiashara unaoendana na wakati”, amesisistiza Waziri Mbarawa.
Profesa
Mbarawa ameitaka Bodi hiyo kuipa ATCL mifumo imara, makini na mahiri
ili kuweza kutatua changamoto zinazoikabili Shirika hilo ikwemo wizi wa
mafuta ya ndege na upotevu wa mapato.
Ili
kupima ufanisi wa utendaji wa Shirika hilo Profesa Mbarawa ameitaka
Bodi hiyo kuandaa mkataba kwa kila mfanyakazi kuanzia ngazi ya juu hadi
chini.
Katika
hatua nyingine Waziri Mbarawa amesema kuwa Serikali ina mpango wa
kununua ndege mbili mpya aina ya Jet ifikapo mwaka 2017 kwa lengo la
kuboresha sekta ya usafirishaji wa anga nchini.
Kwa
Upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin
Ngonyani, ameitaka Bodi hiyo kutumia fursa walioipata katika kufanya
kazi vizuri ili kufufua shirika hilo na kuwapatia watanzania huduma
sahihi na bora za usafirishaji.
Naye,
Mwenyekiti wa Bodi hiyo Mhandisi Emmanuel Korosso, ameahidi
kushirikiana na wajumbe wa bodi yake katika kutekeleza maelekezo ya
Waziri haraka iwezekanavyo ikiwemo kubadilisha menejimenti ya shirika
hilo.
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Maoni
Chapisha Maoni