MAFUTA AINA YA DIESEL YABAINIKA KWENYE VISIMA VYA MAJI MKOANI SONGWE


MAFUTA AINA YA DIESEL YABAINIKA KWENYE VISIMA VYA MAJI MKOANI SONGWE

Waziri wa Mazingira na Muungano Ofisi wa Makamu wa Rais, Mhe January Makamba (Mb) ameendelea na ziara yake mahsusi ya kimazingira ya siku 16 katika mikoa 10 kukagua na kutambua hali ya Mazingira nchini.

Waziri Makamba amefika katika mkoa wa Songwe na kupokea taarifa  ya mazingira ya  Mkoa ambayo imebainisha tatizo la uwepo wa mafuta ya Dizeli katika visima vya maji huku akielezwa kuwa mafuta hayo siyo mafuta ghafi yanayotakiwa kupatikana ardhini. Vilevile taarifa imeeleza uvamizi wa binadamu katika vyanzo vya maji hali inayotishia uhai wa vyanzo hivyo.


Kutokana na taarifa hiyo Waziri Makamba mwenye dhamana ya Mazingira ameahidi kusaidia upatikanaji wa wataalamu ili kuweza kutambua chanzo cha tatizo la uwepo wa mafuta katika maji na ili kutambua njia sahihi za kukabiliana na tatizo hilo.


Vilevile Waziri Makamba amefika katika Wilaya ya Ileje ambapo pia amepokea taarifa ya Mazingira ya Wilaya na

kupongeza juhudi kubwa za wilaya ya Ileje katika utunzaji wa mazingira hasa  eneo kubwa la misitu kuliko katika lililopo katika Wilaya hiyo. Ameahidi pia kuzisaidia Halmashauri za Wilaya na Vijiji namna sahihi na bora zaidi ya kuandaa sheria ndogo za mazingira ili kukabiliana na changamoto za uharibifu wa Mazingira.

Akiwa Wilaya ya Ileje Waziri Makamba pia alifika katika kijiji cha Lubanda ambapo alipata wasaa wa kuzungumza na wananchi wa kijiji hicho  juu ya njia sahihi na namna bora ya utunzaji mazingira huku akiwasisitiza kuacha ukataji miti hovyo na kulima katika vyanzo vya maji huku akisisitiza kilimo cha matuta (kontua) katika miteremko ya milima ili kuepusha udongo na rutuba kupelekwa na maji na kufanya ardhi kuzalisha kwa kipindi kifupi.

Katika kusisitiza utunzaji wa mito na vyanzo vya maji Waziri Makamba amewataka wananchi kuacha kuchepusha maji toka katika mito inayopita katika milima iliyopo katika Wilaya hiyo.
 
"Nikiwa njiani nimeona kuna uchepushaji wa maji, hii ni dhambi kubwa sana ya kimazingira na hatuna budi kuiacha na kufuata taratibu zilizowekwa kisheria za matumizi sahihi ya maji" alisisitiza Waziri Makamba

Waziri Makamba amemaliza ziara yake katika Mikoa ya Morogoro, Iringa, Njombe, Mbeya na Songwe huku akitarajiwa kuendelea katika mikoa ya Rukwa, Katavi, Kigoma, Tabora na kumalizia mkoani Dodoma




Maoni