RPC Manyara, azima mapigano ya Kiteto, Kilindi


Kamanda wa polisi wa mkoa wa Manyara Francis Massawe kulia, akiwa mstari wa mbele, kuwasaka wahalifu kutoka kijiji cha Mafisa wilayani Kilindi wakiwa pori la kijiji cha Lembapuli, Kiteto Manyara, waliodaiwa wanaweka mpaka kati ya wilaya ya kiteto na kilindi pamoja na kuchomwa moto gari aina ya Noah..
 Gari aina ya Noah lililochomwa moto na watu wanaodaiwa kutoka kijiji cha mafisa Wilayani Kilindi Mkoani Tanga kufuatia mgogoro wa mpaka kati ya Lembapuli ya Kiteto na Mafisa ya Kilindi..
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Manyara Francis Massawe akionyeshwa mpaka na mkuu wa Polisi  kiteto, uliowekwa na baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mafisa kufuatia mgogoro wa mpaka kati ya Wilaya ya Kilindi na Kiteto Manyara..
Manyara Fracis  Massawe, akitoa maelekezo kwa kikosi cha FFU kufuatia mgogoro wa mpaka kati ya Wilaya y Kiteto na Kilindi..
Kikao cha kamati ya ulinzi na usalama kati ya Wilaya ya Kiteto kilichohudhuriwa na Kamanda wa Polisi wa Manyara Francis Mssawe kilichofanyika Wilayani Kilindi kufuatia mgogoro wa mpaka kati ya kijiji cha Lembapuli na Mafisa..
Tamimu Kambona Mkurugenzi wa Kiteto akiwa katika harakati za kusaka wahalifu waliochoma gari aina ya noah pamoja na kuweka mpaka kati ya Kiteto na Kilindi kinyume cha sheria...

KAMANDA wa Polisi mkoani Manyara, Francis Masawe, amezima mapigano kati ya wananchi wa Kijiji cha Lembapuli  Wilayani Kiteto mkoani Manyara na Kijiji cha Mafisa kilichopo Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, waliokuwa wakigombea mpaka

Gari moja aina ya Noah lenye namba za usajili T 943 CAK, mali ya Saruni Saninyu (32) lilichomwa moto na baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mafisa, Wilayani Kilindi, waliokuwa na silaha za jadi na za moto, wakati wakiweka mpaka wa wilaya ya Kiteto na kilindi, baada ya kukataa uliowekwa na tume ya Waziri Mkuu

Akizungumza kwenye kikao cha kamati ya ulinzi na usalama wa Wilaya ya Kilindi na Kiteto, kilichofanyika Wilayani Kilindi, Mgaya Nyange, katibu Tarafa wa Tarafa wa Kwekivu aliwambia wajumbe hao kuwa, Baraza la madiwani wa Halmashauri ya Kilindi walikataa mipaka iliyowekwa na tume ya Waziri Mkuu

“Kikao cha baraza la madiwani wa Halmashauri ya Kilindi kilichofanyika hivi karibuni, kwa pamoja madiwani walikataa taarifa ya tume ya Waziri Mkuu, waliowasilisha baada ya kufanya kazi ya upimaji wa mipaka ambapo walituma ujumbe wa kumtaka Waziri Mkuu afike kijijini hapo  kusikiliza kilio chao” alisema Katibu Tarafa huyo

Kufuatia hali hiyo wananchi wa Kijiji cha Mafisa waliungana pamoja wakiwa na silaha za jadi na za moto, kwenda kuweka mpaka wao, kisha kuteketeza gari aina ya Noah lililokuwa na wajumbe watu watatu wa Kijiji cha Lembapuli Kiteto, waliofika walifika kuona jinsi mpaka huo unavyowekwa

Akiwa katika Kijiji cha Lembapuli Kiteto, Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Manyara, Fracis Masawe, aliambiwa na uongozi wa Kijiji hicho kuwa, hali si shwari, wananchi wamefunga shule yao ya Lembapuli na kuhamisha familia baada ya kuambiwa muda wowote watavamiwa na watu wa Mafisa wakiwa na Silaha za Jadi na za moto

Kamanda masawe aliwataka wananchi hao kuwa na subra, na wakaa eneo moja wasitawanyike, kisha kuingia porini na kikosi cha Polisi FFU kusaka watu hao waliokuwa wamedaiwa kuwa porini wakiweka mipaka yao kinyume na taratibu ya nchi kati ya Mkoa wa Manyara na Tanga 

Akiwa katika kikao cha kamati ya ulinzi na Usalama, aliwaambia viongozi wa pande hizo kuwa, matatizo hayo yanalelewa na baadhi ya viongozi ambao wanachelewesha kutatua matatizo ya wananchi kwa wakati hivyo wananchi kuamua kufanya watakavyo wakijua hawawezi kufanywa lolote

“Baadhi ya viongozi mmeshindwa kutimiza wajibu wenu.. sasa wananchi wameamua kututumbua.. nilipoambiwa kuwa kuna watu wachache wako porini wanasilaha, viongozi wa Lembapuli wakinisihi nilifike eti watatujeruhi kama sio kutuua.. nikasema hili halijafikia kuwa hivyo kwa nchi yetu ya Tanzania”alisema Masawe


“Haki ya mungu ningewakuta…tungekuwa tunazungumzia mambo mengine hii leo hapa…(DC) Mkuu wa Wilaya ya Kilindi hata wewe unasema kuna hali ya hatari?..nilisikia mlipokuwa mnawasiliana na wenzenu wa Kiteto nikasema mimi Kamanda Masawe narudi Manyama kufanya nini nikaamua kuingia porini mwenyewe” alisema Masawe

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilindi Sauda Salum Mtondoo, alisema suluhisho la mgogoro huo wa mpaka ni kuja kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, aliyeahidi kufika kufuatia migogoro hiyo ambayo siku zote wamekuwa wakimsubiri na sasa wananchi wamechoka na kuamua kufanya uhalifu

Alisema pamoja na jitihada zilizofanywa na tume ya Waziri Mkuu, kubainisha mipaka kati ya Wilaya ya Kilindi na Kiteto, bado kuna tatizo linahitaji ufafanuzi kwa Waziri Mkuu, kwani hata allipofika kuongea na wananchi hao, waliokuwa wanaweka mipaka hiyo, kabla ya kuchoma gari walimhakikishia kuwa hapatakuwa na tatizo

Kwa mujibu wa Tamimu Kambona, Mkurugenzi Mtendaji wa Kiteto, alimweleza kamanda Masawe, mgogoro huo ulisababisha watu wanne kupoteza maisha kwa vipindi tofauti, kufukiwa kisima kirefu cha maji, pamoja na kuchomwa moto mashine ya maji na jana gari moja aina ya Noah kuchomwa moto

Kamati hizo kwa pamoja walikubaliana, wahalifu wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria, mipaka ya kisheria iheshimiwe, mita 100 kutoka kwenye mpaka pasifanyike shughuli mpya ya uandaaji wa mashamba,pamoja na kuheshimu maamuzi ya ngazi za juu yatakayotolewa na viongozi wao

mwisho

Maoni