DED Kiteto aanika madudu hospitali ya wilaya.

Mkurugenzi wa Kiteto, Tamimu Kambona akifafanua jambo..

Na, MOHAMED HAMAD.
MKURUGENZI mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kiteto, mkoani
Manyara, Tamimu Kambona, amesema hospitali ya Wilaya ya Kiteto
inakabiliwa na uhaba wa dawa kitokana na kitengo cha manunuzi kutokuwa
waadilifu katika manunuzi ya dawa hizo.

Akizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dr. Joel Nkaya Bendera,
aliyetembelea hospitali hiyo, Mkurugenzi huyo alisema, awali alikuta
hospitali ikiwa na mzabuni mmoja anayetumia majina mawili
kujishindanisha mwenyewe ili kupata kazi ambaye ni Magoma na mangaka.

Alisema  kwa kuona hali hiyo baada ya kumchunguza bei za dawa
waligundua kuwa dawa hizo zilikuwa zinauzwa mara mbili ya bei tajwa,
hivyo kusababisha wananchi kulalamika kutokana na uhaba wa dawa, huku
wakitakiwa kwenda kununua maduka ya watu binafsi.

Kufuatia hali hiyo Mkurugenzi huyo aliagiza mzabuni kusimama kuendelea
kusambaza dawa hizo katika hospitali hiyo, na kuanza utaratibu mpya wa
kupata dawa kwa utaratibu unaonufaisha wananchi bila kubughuliwa
kwenda kununua dawa maduka ya watu binafsi.

Katibu tawala wa mkoa wa Manyara, Eliakimu Maswi, aliagiza uongozi wa
hospitali hiyo kuwa makini kuhudumia wananchi huku akisema, wilaya ya
Kiteto imepata fedha mwezi januari mil 600 na kuwataka kununua
madawa,huku akiagiza kuondolewa mhasimu mmoja kati ya wawili waliokuwa
wakifanya kazi katika idara hiyo.

“Hatuwezi kulalamikiwa Serikali kutokana na uzembe wa watu wachache
humu, kwani hawa wahasibu wawili wanakazi gani kama wanashindwa hata
kuwalipa fedha madaktari wanaoitwa kwa dharura kufanya kazi pamoja na
madai mbalimbali ya watumishi humu”alisema Maswi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dr. Joel Nkaya Bendera,
akizungumza baada ya ukaguzi huo alisema wamebaini kuwepo kwa uzembe
wa uongozi wa hospitali hiyo na kuwapa onyo na kumtaka mkurugenzi
kuhakikisha dawa zinanunuliwa ili wananchi wapate huduma hiyo.

Alisema Serikali ya awamu ya tano haicheleweshi kumtumbua mtu
anaposhindwa kuwajibika, na kusema kwa eneo la Kiteto watumishi wa
Sereikali wabadilike na kuendana na kasi ya Rais John Pombe Magufuli
anayesisitiza kuwa wananchi wasibughuziwe wala kucheleweshwa katika
huduma.

Akizungumza baada ya ziara hiyo, mganga mkuu wa hospitali ya wilaya ya
Kiteto Dr. Lupembe alisema kuwa amepokea maagizo na maelekezo ya
serikali katika kuwahudumia wananchi huku akiahidi kupatikana huduma
bora za afya katika hospitali hiyo.

Awali akiwasilisha malalamiko kwa uongozi wa Wilaya kuhusu kero katika
hospitali hiyo Veronica Mollel mkazi wa Kibaya, alisema, wananchi
wanalazimika kwenda maduka ya watu binafsi kununua dawa baridi
wanapougua kutokana na kauli chafu za watumishi kwa wagonjwa pamoja na
madai ya hospitali kutokuwa na dawa  zinazohitajika kwa wagonjwa.

mwisho

Maoni