Majaliwa ahitimisha migogoro ya wakulima, wafugaji Kiteto






Na, MOHAMED HAMAD

WAZIRI Mkuu Kassimu Kassimu Majaliwa, amehitimisha mgogoro wa ardhi
kati ya wakulima na wafugaji, wilayani Kiteto mkoani Manyara, uliodumu
kwa miaka mingi na kusababisha mauaji kwa kushiriki maombi maalumu na
viongozi wa dini, mila na wananchi kwa pamoja.

Mgogoro huo umesababisha watu zaidi ya 30 kupoteza maisha na wengine
zaidi ya 200 kujeruhiwa kufuatia mapigano ya mara kwa mara yaliyokuwa
yakiibuka wilayani hapo, wakati makundi hayo yakigombea ardhi katika
maeneo mbalimbali wilayani humo.

Akizungumza na mamia ya wananchio hao alisema, amebaini kuwa migogoro
hiyo imesababishwa na watu wachache hasa viongozi wa vijiji kugawa
ardhi kwa upendeleo, kuendekeza rushwa hali iliyoleta madhara na maafa
kwa wananchi huku wao wakijinufaisha.

“ Kimsingi hii migogoro hata mkuu wa wilaya angeweza kuitatua, mimi
nilienda pale mpakani mwa Kiteto na Kilindi  mlipokuwa na mgogoro wa
mpaka, nilichokuta ni kitu cha ajabu sana..nimewauliza maswali sita tu
viongozi huku matatu kule matatu nikamaliza mgogoro..”

Kwa Kiteto mliosema mna migogoro pande zote, naangiza tumieni mipaka
ya ardhi GN ya mwaka 1961, itawasaidia kutatua, acheni kubabaika,  kwa
kufanya hivyo mtaondokana na migogoro ya adha hii ambayo imechelewesha
wananchi kwa muda mrefu kupata maendeleo yao

Akizungumza mbele ya Waziri Mkuu, Mkuu wa mkoa wa Manyara Dr. Joel
Nkaya Bendera, alimhakikishia kuwa baada ya maridhiano hayo ya
viongozi wa mila na makabila manne wanguu, wamasai, wakaguu na wagogo
wilaya itakuwa shwari

Alisema awali waliunda kamati ya maridhiano na kuzunguka maeneo yote
kuhubiri amani na kuwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria
mikononi ambapo hitimisho lake ni mkutano huo wa kuomba dua ya pamoja
kuachana na maiaji ya makundi hayo kugombea ardhi

Kwa upande wake mwenyekiti wa mila Abubakar Mrisho (mguu) na Mbabire
Oleikuukuru wa jamii ya kifugaji maasai waliuhakikishia umma kuwa
amani Kiteto itarejea baada ya kula kiapo kwa makabila hayo kuwa
atakayethubutu kuchonganisha wananchi ama kuchochea  atapata madhara

“Kazi iliyofanyika ni ya kuigwa na nzuri sana, kwa muda wote Kiteto
itabaki kuwa shwari, kama kutakuwa na mtu atakayejeruhiwa labda iwe
uhalifu wa kawaida na sio mapigano ya wakulima na wafugaji..hili sisi
tumeshamaliza”alisema Mrisho

Naye Mbambire Oleikurukuru kiongozi wa mila (mmasai) alimhakikishia
Waziri Mkuu kuwa jamii ya kifugaji Kiteto wamepata ujumbe wa kutangaza
amani, kuwa hawatochukua sheria mkononi na kuleta madhara kwa umma

Mwisho.

Maoni