Waziri Mkuu Majaliwa Kassimu Majaliwa..
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa amekerwa na mifuko ya mbolea ya kiwanda cha
Minjingu kuchapishwa anuani ya Kenya wakati inazalishwa Tanzania na
kumtaka mwekezaji kumuomba radhi Rais.
Kutokana
na hilo, Waziri Mkuu amewataka wamiliki wa kiwanda hicho, waandike
barua kwa Rais John Magufuli kabla hajamaliza ziara yake keshokutwa na
apate nakala ya barua hiyo.
Alitoa
agizo hilo baada ya kutembelea kiwanda hicho kilichopo wilaya ya Babati
akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake mkoani Manyara. Waziri Mkuu
amerejea Babati jana akitokea Dar es Salaam ambako alikuwa na ratiba za
kitaifa.
“Nilikuja
kukagua kiwanda baada ya kupokea malalamiko kuwa mbolea hii haikubaliki
huko vijijini. Watafiti wameonyesha kuwa ikitumika inasaidia kutoa
mazao mengi. Lakini wakati niko kiwandani nimekerwa kukuta mifuko ya
kupakia mbolea hii ina anuani ya Nairobi, Kenya wakati mali ghafi
inatoka Tanzania,” alisema.
“Ni
kwa nini mifuko hii ina anuani ya Kenya? Hapa tulipaswa tuone anuani ya
Babati! Je mlipata kibali kutoka serikalini? Tena kuna lebo ya TBS.
Kwanini Tanzania haionekani? Kwani malighafi iko Kenya? haiwezekani, ni
lazima uandike barua na uombe radhi kwa Mheshimiwa Rais Magufuli. Yeye
anahimiza ujenzi wa viwanda ndani ya nchi, halafu ninyi mnafanya hivyo?”
Akitoa
maelezo kuhusu hali hiyo, Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Tosky Hans
alimweleza Waziri Mkuu kwamba wametumia lebo hiyo kutokana na
makubaliano na wanunuzi jibu ambalo Waziri Mkuu hakulikubali na
kusisitiza kuwa anapaswa aombe radhi.
Maoni
Chapisha Maoni