RC Manyara, awang’akia viongozi Kiteto

                                           Mkuu wa Mkoa wa Manyara Dr. Joel Nkaya Bendera


Na, MOHAMED HAMAD.
MKUU wa mkoa wa Manyara, Dr. Joel Nkaya Bendera, ameonya baadhi ya viongozi wilayani Kiteto kuwa chanzo cha migogoro ya ardhi akisema, wameligharimu Taifa kutumia fedha nyingi kuitatua pamoja na kucheleweshewa maendeleo.

Akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani Mkuu huyo wa Mkuu huyo wa mkoa alisema, migogoro ya ardhi Kiteto, imekwisha kwa kufanyika maridhiano ya wananchi na Waziri Mkuu Majaliwa Kassimu Majaliwa kuhitimisha.

“Uongozi wa mkoa hatuwezi kuendelea kuwafumbia macho baadhi ya viongozi ambao wamekuwa matatizo kwa wananchi..na tumeanza kazi sasa tutamnyofoa mmoja mmoja ili wananchi wabaki salama”

Alisema katika kukabiliana na tatizo hilo, mkoa umejipanga kufanya ufuatiliaji wa kina huku akimpa siku 14 Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Tumaini Magessa, kuanza uhakiki upya wa mashamba kubaini wanaomiliki mashamba makubwa bila vibali

Akiwa katika ziara wilayani Kiteto Mkuu huyo wa Mkoa wa Manyara alielezwa na wananchi kuwa, kuna baadhi ya wakulima wamejimilikisha mashamba makubwa ekari 1,000 mpaka 3,000 huku wakiwa hawana vibali.

“Nimezungumza na baadhi ya wananchi wakisema, kuna wanaomiliki mashamba makubwa..hawana vibali na mwisho wa vijiji kugawa ardhi ni ekari 50 kwa mtu mmoja, sasa kwa kiteto nimegundua maajabu ya dunia kuwa mtu mmoja ana maekari ya shamba akimiliki isivyo halali”alisema.

Katibu Tawala wa mkoa wa Manyara Eliakimu Maswi, akizungumza mbele ya baraza hilo alisema tayari wameanza kuchukua hatua kwa baadhi ya viongozi wasioadilifu na matokeo yataonekana kwa wananchi kubaki salama.

Alisema serikali ya awamu ya tano haihitaji kusikia wananchi wakilalamika na badala yake viongozi wametakiwa kutatua mara wanaposikia malalamiko, ili waishi kwa kuifurahisha Serikali yao ambayo ni ya hapa kazi tu.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kiteto, Lairumbe Mollel alimhakikishia mkuu huyo wa mkoa kuwa wilaya itatekeleza maelekezo yote waliyopewa na mkoa akisema hayo ndio maamuzi sahihi kumaliza mgogoro huo

Mwisho.

Maoni