CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM) CHAPOKEA TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA ILANI YA UCHAGUZI KUTOKA TAASISI ZA FEDHA

*CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM) CHAPOKEA TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA ILANI YA UCHAGUZI KUTOKA TAASISI ZA FEDHA ZINAZOWEZESHA WANANCHI NA KURATIBIWA NA SERIKALI KUPITIA BARAZA LA TAIFA LA UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI (NEEC)*

Leo tarehe 20 Mei 2018 Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia kwa Ndg. Humphrey Polepole Katibu wa Itikadi na Uenezi kimepokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 - 2020 kutoka katika Taasisi za kifedha zinazowezesha wananchi na kuratibiwa na Serikali kupitia Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).

Kikao hicho cha upokeaji wa taarifa ya utekelezwaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kimefanyika katika Ofisi Ndogo za Chama Cha Mapinduzi Lumumba Jijini Dar Es Salaam na kuhudhuriwa na jumla ya Mifuko na Taasisi za Kifedha thelathini na sita (36) ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ikiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la uwezeshaji wananchi kiuchumi Dk. John Jingu.

Katika kikao hicho Ndg. Polepole amewaeleza watendaji wa mifuko hiyo kuwa,

*Chama Cha Mapinduzi kimeweka utaratibu wa kufuatilia utekelezaji wa Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2015 hadi 2020. Ilani ya Uchaguzi ya CCM ndio mkataba kati ya CCM na wananchi na hasa wapiga kura. Sasa, tunapoelekea na ifikapo mwaka 2020 tunapaswa kutoa hesabu ya nini tumetekeleza sambamba na tuliyoyaahdi 2015, ikiwemo fursa za uwezeshaji wananchi kiuchumi.*

Aidha Ndg. Polepole ameeleza dhumuni la mkutano huo kuwa ni kupata fursa ya kushirikishana mwelekeo wa Sera za CCM na maelekezo yake kwa Serikali kadri utekelezaji wa Ilani unavyoendelea na mrejesho tunaoupata kutoka kwa wananchi kwa kuzingatia kuwa, katika Ilani ya CCM fungu la 56 hadi 63 inazungumzia uwezeshwaji wa wananchi kiuchumi.

Akipokea taarifa hiyo Ndg. Polepole amesisitiza kwa watendaji hao juu ya umuhimu wa kuongeza ushirikiano baina ya taasisi za uwezeshaji na kusema kuwa,

*Ili kufikia lengo la kuwakwamua wananchi kutoka katika umasikini ni lazima taasisi na mifuko yote iliyo chini ya Serikali iweke utaratibu mzuri wa mawasiliano ya mara kwa mara na kubadilishana uzoefu.. Ni lazima uwekwe utaratibu wa uratibu wa shughuli za mifuko hii kupitia Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi.. Ni lazima yawepo mashirikiano baina ya taasisi na mifuko hii ili kuongeza tija na ufanisi katika kuwawezesha wananchi kiuchumi.*

Kikao hicho ni sehemu ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (2015-2020), ambapo CCM imeahidi kuwawezesha wananchi kiuchumi ikiwemo kuwapatia mikopo ya masharti nafuu wakina mama, vijana, watu wenye ulemavu, wajasiriamali pamoja na wakulima wadogo wadogo na wakati.

Imetolewa na,

*IDARA YA ITIKADI NA UENEZI*
*CHAMA CHA MAPINZUZI (CCM)*

*OND - LUMUMBA*

Maoni