Wananchi Hanang kunufaika na SUMAJKT

Wananchi Hanang kunufaika na SUMAJKT

Na, MOHAMED HAMAD HANANG

WANANCHI wilayani Hanang mkoani Manyara, wanakusudiwa kunufaika na uwekezaji mkubwa utakaofanywa na shirika la uzalishaji mali la jeshi la kujenga Taifa SUMAJKT.

Mkurugenzi mtendaji wa SUMAJKT, Brigadia Jenerali Charo Yateri, ametaja miradi itakayonufaisha wananchi hao kuwa ni ujenzi wa Hoteli ya hadhi tano (five star).

Ujenzi wa karakana ya zana za kilimo, maduka makubwa ya bidhaa (shopping center) karakana za matrekta, kituo cha mafuta cha uhakika na uwekezaji wa kilimo.

Akizungumza hayo baada ya kuwekeana mkataba wa makabidhiano ya maeneo hayo mkurugenzi huyo alisema, lengo la uwekezaji huo ni kuunga mkono Jitihada za Serikali ya awamu ya tano ya Rais Dr. John Pombe Magufuli kuifanya Tanzania kuwa ya viwanda sambamba na kutengeneza nafasi za ajira kwa wananchi.

Alisema katika utekelezaji wa uwekezaji huo waataanza na ujenzi wa maduka makubwa na hoteli ya ngazi tano (five star) ambayo pia itatumiwa na viongozi wakubwa wa Kitaifa watakaofika wilayani hapo.  

Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi ya SUMAJKT, Meja Generali (msaafu) Mohamed Farah alisema kazi hiyo itaanza baada ya kukamilishwa michoro kisha watatoa ajira kwa wananchi kufanya shughuli mbalimbali katika maeneo hayo.

Mkuu wa Wilaya ya Hanang Bi. Sarah Msafiri aliwahakikishia uongozi wa SUMAJKT kuwa ataharakisha wanakamilisha taratibu za kisheria ili shughuli hizo zianze mara moja.

“Napata faraja kupata uwekezaji mkubwa, wananchi watanufaika kwa mambo mbalimbali kwakuwa tuna miundombinu bora ya barabara ya lami hivyo moja kati ya vitu muhimu katika uwekezaji ni kuwa na miundombinu mizuri.

“Nitoe wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli hizo kwani wao ndio wanufaika kwakubwa, na ambao wanatakiwa kutoa nguvu kazi kubwa katika miradi hiyo adhimu”alisema DC Msafiri.

Kabla ya kuwekeana makubaliano ya uwekezaji huo, pande hizo zilienda kuona eneo la ekari mbili kati ya nne zilizokuwa zimeombwa kwaajili ya ujenzi wa hoteli kubwa na maduka ya kisasa pamoja na shamba la ekari 1000 kwaajili ya kilimo eneo la Bassotu.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Hanang, Geoge Bajuta aliuomba uongozi wa SUMAJKT kuwa ajira zitakazotolewa na SUMAJKT, kipaombele kiwe kwa wananchi wa Hanang.

Alisema kwa sasa wananchi wako tayari kushirikiana na SUMAJKT kikamilifu kufanikisha miradi yote akidai kamwe hawatawaangusha katika uwekezaji huo ili uwe wenye tija kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

MWISHO.

Maoni