Kinnapa latumia sh 120 mil kuchimba visima 10


Kinnapa latumia sh 120 mil kuchimba visima 10

Na, MOHAMED HAMAD KITETO.

SHIRIKA lisilo la Kiserikali (KINNAPA) Wilayani Kiteto Mkoani Manyara, linalotoa huduma za jamii, limepunguza adha ya maji kwa wananchi  kwa kuchimba visima 10.
Visima hivyo vimechimbwa Vijiji vya Kimana, Matui, Chapakazi, Lalakir ya Partimbo, Sekii visima viwili, Vumilia,  Msakasaka, Bwagamoyo na Ilera.

Akizungumza na MTANZANIA, Mratibu wa Shirika hilo, Abraham Akilimali leo (jana) alisema jumla ya sh 120 mil zimetumika kuchimbwa visima hivyo ambavyo vitakuwa vinatumia pamp za mkono.

“Muda mrefu wananchi hawa walikuwa wakitumia gharama kubwa na muda kupata maji, hivyo kwa kuona ukubwa wa tatizo hili, Shirika la KINNAPA tumesikia kilio chao kwa kuwachimbia visima hivyo”alisema Akilimali.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, Tamimu Mahmmoud Kambona, alikiri kuwepo kwa adha ya maji akisema awali wananchi vijijini walipata maji safi na salama kwa 37%.

“Serikali tumejipanga kuhakikisha tunapandisha asilimia hizi, kwani mbali na visima hivyo kwa miezi 18 toka nimeteuliwa kuwa Mkurugenzi hapa, nimechimba visima vingine zaidi ya 15” alisema Kambona.

Wakizungumza baada ya kuchimbiwa visima hivyo baadhi ya wananchi walisema huduma ya maji ni muhimu kwani kutopatikana kwa wakati walishindwa kufanye maendeleo mengine.

Huwezi amini suala la ujenzi lilitushinda, wanaume na wanawake tulibaki kutafuta maji masika na kiangazi, lakini sasa tunashukuru hizi jitihada za Serikali na Mashirika zimetuokoa, alisema Rajabu Musa (Mwananchi) wa Kijiji cha Matui.

Mwisho.



Maoni