HUDUMA YA MAJI KITETO YAGEUKA KUWA BIASHARA


Baadhia ya wananchi wa mji wa Kibaya wakiwa kwenye foleni ya maji ambapo imeelezwa ili kupata maji lazima kuwekwa foleni kwa siku tatu

Huduma ya maji Kiteto yageuka kuwa biashara

Na Mohamed Hamad Manyara
HUDUMA ya maji wilayani Kiteto Mkoani Manyara imegeuka kuwa biashara inayofanywa na taasisi za Serikali (mamlaka za maji wilaya) hali inayosababisha usumbufu kwa wananchi kwa 
kuwachelewesha katika kujiletea maendeleo yao 

Ndoo moja ya maji inauzwa kati ya Tsh 1,000 na 1,500 maeneo ya vijijini hali iliyodaiwa kuwa  wananchi wanalazimika kutumia gharama kubwa ya pesa na muda kusaka maji hayo kuliko kufanya shughuli zingine za maendeleo

Wakizungumza na MTANZANIA wananchi hao wamesema biashara hiyo inafanywa na baadhi ya viongozi wa Serikali kwa kuwatumia baadhi ya vijana wilayani humo kuuza maji kwa kutumia maboza,viberenge na pikipiki maarufu bodaboda

“Huwezi kuamini viongozi wakubwa wananufaika sana na huduma hii ya maji na ndio maana utakuta hakuna ufumbuzi wa dhati katika utatuzi wa maji hali hii inatugharimu sana wananchi, tunaiomba Serikali iingilie kati kwani tunaumia sana,”alisema Ramadhani Machaku (mwananchi)

Alisema kila siku mtu akiamka asubuhi anafikiria namna ya kupata maji na wakati mwingine  wanaweka foleni kwa zaidi ya siku tatu ili wapate maji, na kuongeza huduma hii inawalazimu kutumia muda mwingi kuliko kazi nzingine za maendeleo

Kutokana na adha hiyo wananchi wa mjini wa Kibaya na wale waishio vijijini wameitaka Serikali kuzuia maji kuwa biashara na badala yake iwe huduma kama ilivyokuwa awali kwani kufanya hivyo inawagharimu katika maisha yao

Serikali ya wilaya imedai kuwa watahakikisha kuwa maji yanapatika kwa wingi mijini na vijijini kutokana na mipango ambayo imewekwa kama moja ya jitihada za kuwaokoa wananchi na matatizo yanayowakabili

Akizungumza hayo Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Bi. Martha Umbulla alisema kuwa tatizo la maji ni kubwa wilayani hapo kutokana na uchakavu wa miundombinu ambayo ni ya toka mwaka 1970 wakati wananchi hao wakiwa 12,000

“Vipo visima alivyotuahidi Mhe. Rais wetu wakati wa kampeni na naamini kuwa ahadi hiyo itatekelezwa bila wasiwasi, kwa hivi karibuni savey ilifanyika na kubainii maeneo yatakayochimbwa visima hivyo”alisema Bi. Umbulla

Amewataka wananchi hao kuwa na subra wakati Serikali yao ikiwa katika mchakato wa kuwafanikishia huduma hiyo na kuongeza kuwa kwa kiasi kidogo cha maji yaliyopo kitumike vizuri bila hujma ili yaweze kusaidia

mwisho 

Maoni