AGIZO LA PINDA LAPUUZWA KITETO

Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Martha J.Umbulla mwenye miwani akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halamshauri ya Wilaya ya Wilaya ya Kiteto Bi Jane Mutagurwa


Agizo la Pinda lapuuzwa Kiteto

NA.MOHAMED HAMAD
CHAMA cha TLP Kimewashukia Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Martha Umbula pamoja na Mkurugenzi Mtendaji Jane Mutagurwa kwa kuwataka wajiuzulu kwa kushindwa kutekeleza agizo la Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyeagiza wakulima waliochomewa makazi yao wapatiwe chakula

Akizungumza na MTANZANIA  Ramadhani Machaku Mwenyekiti wa TLP Wilayani humo alisema Waziri Mkuu alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Kiteto kuwapatia chakula wahanga waliopatwa na matatizo baada ya kuchomewa makazi yao na wengine kuuawa bila sababu

Alisema toka agizo hilo litolewe Jan 16 mwaka huu wakulima hao hawajapatiwa msaada wowote na badala yake wamekuwa wakipigwa kalenda na kutakiwa kuondoka katika maeneo hayo kwa madai kuwa hawako kisheria

“Namtaka Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Martha Umbula ajiuzulu pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halamshauri ya Wilaya Jane Mutagurwa kwa Kushindwa kutekeleza agizo la Waziri Mkuu kama walivyo agizwa Jan 16 mwaka huu  na Pinda”alisema Machaku

Alisema pamoja na agizo hilo pia walitakiwa watafute mihtasari ya vijiji saba vilivyodaiwa kuunda Hifadhi iliyopewa jina la Emboley Murtangos ambayo kwa sasa imejaa utata wa jinsi ilivyoanzishwa kuwa jamii haikushirikishwa

“Ninachojua na ambacho kinatakiwa kitekelezwe ni lile agizo la Pinda na sio vinginevyo, kwani kama utafika wakati wa viongozi wa ngazi za chini kukaidi agizo la Kiongozi wa Ngazi za juu ina maana hakuna kazi inayoweza kutekelezeka na badala yake kila kukicha wananchi watazidi kulalama”alisisitiza Machaku

Hata hivyo Machaku alisema kazi inayofanywa na kamati ya Ulinzi na usalama pamoja na baadhi ya madiwani sio kuhakiki na kukusanya mihutasari ya vijiji hivyo badala yake ni kuwataka wananchi waliopo maeneo hayo ya Laitimi na kwa Mtanzania waondoka

Hivi karibuni Waziri Mkuu Mizengo Pinda alifika Wilayani Kiteto kwaajili ya kujionea maafa ya zaidi ya watu 16 waliopoteza maisha katika makazi yao baada ya kuvamiwa na kikundi cha watu wachache na kuagizwa Polisi kuwasaka wahalifu mpaka wapatikane

Waziri Mkuu akizungumza na mamia ya wananchi wa Mji wa Kibaya aliwaambia kuwa baada ya kutembelea eneo hilo linalodaiwa kuwa ni hifadhi alichokuta ni mashamba ya wakulima ambapo hapo aliacha agizo kuwa ipatikane mihutasari ya makubaliano ya kuanzisha hifadhi hiyo ili Serikali iweze kutoa tamko

Hata hivyo Mahakama ya Rufaa katika kesi ya msingi kati ya Halmashauri na wakulima iliamuru pasiwepo na shuguli za kibinadamu katika eneo hilo kati ya wakulima na wafufaji na wala watu wasiondolewe kwa nguvu 

Hata hivyo kutokana na agizo hilo jumla ya watu 35 walikamatwa na Polisi, 12 walifikishwa mahakamani na kufunguliwa kesi ya mauaji, 10 wako chini ya uangalizi wa Jeshi la Polisi,7 waliachiwa huru  baada ya Polisi kujiridhisha na wengine 6 wanaendelea kuhojiwa juu ya mauaji ya watu 10 Jan 12 mwaka huu.

Mwisho

Maoni