NKAMIA APATA MAPOKEZI HAFIFU JIMBONI KWAKE


Nkamia apata mapokezi hafifu Jimboni kwake
·         Awashambulia wapinzani kwa kuimba mashairi
·         Atangaza neema kwa vijana,wazee

NA.MOHAMED HAMAD, CHEMBA
Wakati uteuzi wa mwanahabari Juma Selemani Nkamia kuwa Naibu Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo ukiendelea kuhojiwa hapa nchini, kwa mara ya kwanza amepata mapokezi hafifu Jimboni kwake  alipofika kwenye mkutano wa kampeni za Udiwani Kitongoji cha Kaloleni Kata ya Mrijo Wilayani Chemba

Kutokana na mahudhurio hayo hafifu ya wananchi kumlaki Mbunge wao na Naibu Waziri baadhi ya wananchi wameeleza sababu za wananchi kutohudhuria mkutano wake kuwa ni pamoja na wengi wao kuwa shambani kujitafutia riziki na wengine jana (juzi) ilikuwa siku ya soko

Akizungumza na MTANZANIA mara baada ya kumalizika mkutano huo wa kampeni mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Chemba Alhaji Sahaaban Issa Kilalo kuhusu uchache wa wananchi hao alisema idadi hiyo imetokana na wananchi kuwa wachache kwenye tawi la CCM Songambele

“Wanachama waliofika kwenye mkutano ndio hao waliokusudiwa kulingana na idadi yao, naweza kusema pia walikuwa wengi kwani wengi waliofika ni pamoja na wapinzani kumlaki Naibu Waziri ambaye naweza kusema ni bahati kubwa Wilaya mpya ya Chemba kupata Waziri”alisema Kilalo

Pia tuliona kulingana na ratiba yetu ilikuwa sahihi kufika katika tawi hilo kwakuwa ilikuwa siku ya Kampeni za udiwani na isingewezekana kufanyika mkutano Olboloti ambako kulikuwa na wananchi wengi kwenye soko ambako kila mtu alikuwa anajitafutia kipato chake cha kuendesha maisha yake alisema

Kwa upande wake Ayubu Mjeja (Bingwa wa mayenu) alisema Mkutano huo ulifana kwa kiasi chake kwa kuwa ni wakati wa kilimo kila mtu alikuwa na ratiba zake za shambani tofauti na siku zingine ambazo wengi wao huzagaa mitaani wakiwa hawana kazi za kufanya

“Utampata nani hivi sasa, watu wameenda shambani, naweza kusema hata ule mutano ulifanikiwa sana na kwa uchache huo Naibu Waziri alieleweka alichosema naamini kila mtu atakuwa amepata taarifa juu ya ziara hii na kilichozungumzwa kimeleta matumaini kwa wananchi”

Mjeja alisema zipo changamoto kubwa zinazowakabili wananchi wa Olboloti akitaja kuwa ni maji,migogoro ya ardhi,elimu pamoja na afya akisema kutokana na bahati waliyopata kutoka kwa Mungu ya kuteuliwa Nkamia kuwa Kiongozi wa kwanza Waziri  toka Wilaya ya Chemba na Kondoa anaamnini kuwa zitatatulika

Naye Asia Pipi (mwananchi) alisema kupata madaraka ni jambo moja lingine ni uwajibikaji,akisema nafasi aliyopata Nkamia ina changamoto kubwa kutokana na kutakiwa kutumikia nyazifa mbili kwa wakati mmoja Ubunge na Uwaziri huku wananchi wakitegemea makubwa Jimboni kwao

Akizungumza na wananchi hao Naibu Waziri Nkamia alianza kwa kumshukuru mungu kwa kuteuliwa kwake akisema hizo ni Baraka za wananchi wa Jimbo la Chemba baada ya kugawanyawa Wilaya ya Kondoa na kupatikana Wilaya mpya anayoiongoza hivi sasa ya Chemba

Nkamia alikerwa na wapinzani akisema kamwe CCM haiwezi kuiga taratibu zao zikiwemo za kutembea na Helkopta angani wakidhani wingi wa watu wanaoupata ndio idadi ya kura, akisisitiza kwa kuimba shairi kuwa hana shaka na watu wa Mrijo, dua waliomuombea ndio zilizompa Unaibu Waziri, akisema Cheo hicho sio chake bali ni cha wananchi wa Chemba

Aliwataka wananchi hao kumchagua Hamisi Nayasuka kuwa Diwani wa kata ya Olboloti akisema kuwa anaamini ni mchapakazi na mzoefu wa uongozi hata wananchi wanajua umuhimu wake Kijijini na kuongeza wasihadaike na rushwa za mirungi na viroba wanavyotoa wapinzani

AHADI
Kuhusu ahadi Nkamia alisema kwa kuwa Wilaya ya Chemba ni mpya uongozi wake umejipanga kuhakikisha Kijiji cha Mlongoa kinapata maji safi na salama na kuongeza kuwa umeme utaenda kila Kijiji ukianzia Kijiji cha Jangalo, Mtakuja, Kinkima, Mlongia, Masada, Machiga, Kwamtoro, Farkwa, Dosoo, Bubutore,Gwandi hadi Chemba ambapo mkandarasi amepatikana

Alisema Kondoa wameanza kuchanganyikiwa kwa kuona Chemba inaenda kwa kasi kubwa na kusisitiza wananchi wawe watulivu ambapo kwa kuanza timu zote za michezo zitapata Jezi huku akisisitiza akinamama watakaokuja kwenye mikutano yake watapata themos za chai na viokombe

Kuhusu mikopo Nkamia aliwataka wananchi waendelee kuwa wapole kwani kuna mchanganua unaomalizika kuwa hivi karibuni wananchi wataanza kunufaika nao na kuwataka waachane na mirungi,pamoja na viroba wanavyopewa na wapinzani ili waweze kuwapigia kura

Wakati huo Nkamia aliagiza Jeshi la Polisi kuwakamata watu wanaonunua shahada za kura akisema zipo tetesi kwa wananchi kuwa kuna wanaojihusisha na kazi hiyo akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni kosa na sheria zichukuliwe mara moja kwa wahusika

Hata hivyo baada ya kumaliza mkutano wa kampeni akirejea kwa kwa kupita katika mitaa mbalimbali ya kata ya Olboloti Mbunge Nkamia akiwa kwenye gari la Chama chake alirusha kalamu kwa wananchi wake zilizoandikwa jina lake na Nembo ya chama ambapo wananchi walionekana kugombania

Baadhi ya wananchi walionekana kufurahishwa kupata kalamu hizo ambazo hawakutegemea wakisema zitasaidia watoto wao, lakini wengine walichukizwa na kitendo hicho wakisema ni dharau kwani alikuwa na kila sababi ya kugawa kwa utaratibu na sio kurusha barabarani akitembea kwenye gari

“Kama alilenga kuwasaidia watoto wetu alitakiwa apeleke shuleni wakagawiwe kwa utaratibu elimu katika kata hii ni duni alipaswa kuwa muungwana na sio kama alivyofanya kwani wako watu wazima waliodhalilika kwa kunyanganyana kalama barabarani jambo ambalo sio zuri”alisema mmoja wa wananchi wa Olboloti

Kwa upande wa Wapinzani Abdala Suti (CUF) akizungumzia ziara hiyo alisema ziara ya Nkamia pamoja na kufika akiwa na gari la Serikali alibadilisha gari na kuvaa joho la CCM hali iliyowapa shada wapinzani na wakashindwa ufika kwa madai kuwa aikuja Kichama na sio Kiserikali pamoja na kwamba alitumia kari la Serikali

Mwisho

Maoni