WAFUNGWA MWAKA KWA KUKUTWA NDANI YA HIFADHI KITETO


27 Jela kwa kukutwa ndani ya Hifadhi Kiteto

Na Mohamed Hamad
JUMLA ya watu 27 Wilayani Kiteto Mkoani Manyara wamehukumiwa kwenda Jela mwaka mmoja kwa kosa la kukutwa ndani ya Hifadhi ya Emboley Murtangos iliyoundwa na Vijiji saba kama msitu wa jamii

Idadi hiyo ni kati ya watu 105 waliokamatwa Januari 27 mwaka huu na kufikishwa kwa hakimu mkazi wa Mahakama ya mwanzo Kibaya kwa tuhuma za kukutwa ndani ya Hifadhi hiyo Wilayani humo

Hakimu Bruno Bongole akisoma shitaka moja kwa watu hao 27 alisema watuhumiwa kwa pamoja walikutwa ndani ya Hifadhi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto ya Emboley Murtangos kinyume cha sheria ambayo ilisajiliwa mwaka 2013

Baadhi ya watuhumiwa walikana shitaka hilo na kesi kuanza kusikilizwa ambapo walalamikaji walikuwa ni Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto pamoja na Serikali kuu  ambao waliwakamata na kuwafikisha mahakamani hapo

Kwa upande wa Serikali kuu alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Bi.Martha Umbulla akiwakilishwa na katibu tawala, na Halamshauri alikuwemo mwanasheria wa Halamshauri Cosmas Msemwa,Barhezi Titi, Mariamu Mohamed mafisa misitu

Kwa mujibu wa Hakimu Bongole washitakiwa  wakiongozwa na Fokas Rafael kwa pamoja wametakiwa kwenda Jela mwaka mmoja bila faini kwa madai kuwa ni stahili yao ili iwe fundisho kutokana na jinsi mvuto wa kesi hiyo ilivyo

Kati ya idadi hiyo wapo wazee wawili wa miaka 60,mwananke mmoja mwenye mtoto  na mtoto wa miaka 14 ambapo wao walifungwa kifungo cha nje kutokana na umri na pia mwanamke kuwa na mtoto wa kunyonyesha

Akizungumzia hukumu hiyo Mwenyekiti wa wakulima Bw.Maneno Saidi Mpanda wa Laitime alisema suala hili lina utata mkubwa kutokana a na jinsi lilivyoendeshwa na Uongozi wa Wilaya ya Kiteto ambao wamekiuka maagizo ya Waziri Mkuu

Alisema Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipofika Kiteto alitoa agizo la kuwafumbaza wakulima na kujiona kuwa wangeweza kuendelea kuwepo akisema watu waliopo walindwe,wapatiwa chakula, wakati Serikali inajiridhisha kuhusu mipaka ya eneo hilo

“Waziri Mkuu alisema kuna mtu ana miaka 20 eneo la kwa Mtanzania atampeleka wapi, akisema katembea kwa Hekopta hajaona Hifadhi akisisitiza Uongozi wa Kiteto ukae na kuangalia upya kama nia ya Hifadhi ipo ama haipo” alisema Mwenyekiti huyo

Alisema baada ya agizo hilo siku chache Serikali ya Kiteto ikaanza operesheni ya kuwakamata watu na kuharibu makazi yao huku mashamba yakichungiwa mifugo maeneo ya mlima Itamba wakiendelea kuishi humo kwenye Hifadhi na kuharibu mazao ya wakulima

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Bi Martha Umbulla akizungumza na Nipashe hivi karibuni alisema wanachosimamia ni amri ya Mahakama ya Rufaa ambayo ilitolewa mwaka 2012 kuwa hatakiwi mkulima wala mfugaji kwenye eneo hilo

Mwisho

Maoni