WAKUNGA WA JADI KITETO WATUMIA MALBORO KUZALISHA


Wakunga wa jadi Kiteto watumia malboro kuzalishia

Na Mohammed Hamad
WAKUNGA wa Jadi Wilayani Kiteto Mkoani Manyara wameendelea kutumia mifuko ya Rambo (malboro) kama gloves wakati wa kuzalisha kwa lengo la kujikinga na VVU Ukimwi baada ya kunyimwa glovs na Idara ya Afya Kiteto kwa madai hawapaswi kufanya kazi hizo wanapokuwa nyumbani

Akizungumza hayo Joseph Tutuba Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kiteto kwenye Semina ya Ukimwi hivi karibuni mjini Kibaya alisema kazi ya wakunga wa Jadi ni kusindikiza wajawazito Hospitali ama kituo cha afya na sio kuzalisha kama wanavyofanya sasa

“Ukiwapa wakunga Gloves utakuwa umewahalalishia kazi hiyo badala ya kuwasaidia kuwapa huduma ya kwanza wakati wa kuwapeleka kwenye vituo vya afya, sasa hili tumeliona na kusema ili watu waje kujifungulia Hospitali lazima tupige marufuku wakunga wa jadi kuzalisha kwa kutowapa gloves”slisema Tutuba

Alisema kitendo cha kutumika kwa malboro kama gloves na hatua ta kunyima kufanya kazi hiyo kwa kutopewa gloves, na kuongeza kwa utaratibu wa Wizara ya Afya wanatakiwa utambuliwa na sio kufanya kazi hizo kama walivyojitokeza kwa wingi Kiteto hivi sasa

Hatua hiyo imetokana na baada ya kuulizwa kuwa Idara ya Afya Kiteto ina mkakati gani kuzuia maambukizi kwa wakunga wa Jadi wanaotumia malboro kama gloves kutokana na kunyimwa kwa maksudi ili wasifanye kazi hiyo

Hata hivyo kutokana na ukubwa wa tatizo hilo Mainge Lemalali Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto aliiagiza kamati ya huduma za jamii kuingilia kati suala hilo akisema kuwa kuna haja ya kutazamwa upya kunusuru maambukizi ya Ukimwi kwa wakunga

“Huwezi kuwatambua wakunga 145 Kiteto na usiwape hata vitendea kazi pale wajawazito wanapoletwa Hospitali wanasaidiwaje, unategemea nini na kwanini maambukizi yasiongezeke kwa wakunga kutaka kuokoa maisha ya mama na mtoto”alisisitiza Mainge

Kwa upande wake Zamzamu Ramadhani Diwani Viti maalumu CHADEMA alisema ni aibu kwa Serikali kuwanyima wakunga gloves akidai utamaduni wa kiafrika wakunga wa jadi hata kama hajaruhusiwa  ilimradi anajua kufanya kazi hiyo hujitokeza kuokoa maisha ya mama na mtoto

Semina hiyo imeandaliwa na Halmashauri ya Wilaya kupitia Idara ya Afya ambapo ililenga kubuni mikakati mipya ya kukabiliana na janga la Ukimwi ambalo linazidi kuwa tishio ndani ya Jamii

Kwa Upande wake Joseph Mwaleba Ofisa Maendeleo ya Jamii Kiteto akiongea kwenye mafunzo hayo pamoja na Jitihada za kukabiliana na VVU Ukimwi kupitia semina na makongamano bado elimu inahitajika kwa wananchi Kiteto.

Mwisho

 

Maoni