CHADEMA
yatoa siku 10 za kufanya uchaguzi Kiteto.
- · Uongozi wa vijana wavunjwa,waundwa upya.
- · Kutoshiriki uchaguzi mkuu 2015 wasipofuata masharti.
Na. Mohamed Hamad Manyara.
CHAMA cha Demokrasia na
maendeleo CHADEMA Taifa kimetoa siku kumi kwa uongozi wa chama hicho Kiteto kufanya
uchaguzi ngazi ya chini (Chadema ni msingi) hadi wilaya ili waweze kupata
tiketi ya kushiriki uchaguzi mkuu wa 2015.
Mkuu wa itikadi na uenezi Taifa
Waitara Mwita akizungumza na kamati ya utendaji wa chama hicho Wilayani Kiteto
jana (juzi) alisema ushiriki wa chama hicho uchaguzi mkuu 2015 utategemea
kukamilika kwa uchaguzi ngazi ya chini.
“Hatutaivumilia wilaya
yoyote ishiriki uchaguzi mkuu mwakani kama hawatafanya uchakuzi ndani ya chama
na hili tutalisimamia kikamilifu na wala hatutaona haya kulisemea na mahali
popote nchini”alisema Mwita.
Wakati huo kwa mujibu wa
katiba ya CHADEMA kiongozi huyo ameufuta uongozi wa vijana wilaya baada ya
kuonekana wana umri mkubwa na
kuchaguliwa Abubakari Kidevu kuwa mwenyekiti huku katibu akiwa Athumani Ismail.
Mbali na hatua hiyo pia kura
zililazimika kupigwa kuhusu kuvunja kamati ya utendaji ama kutovunjwa kutokana
na kuonekana kushindwa kuwajibika ipasavyo ambapo walilazimika kuongezewa
wajumbe wengine ili kusukuma mbele shuhuli za chama.
“Hali haikuwa shwari kwenye
kikao, kwani hata kamati ya utendaji ilitakiwa kuvunjwa kutokana na sababu
mbalimbali zikiwemo za kutowajibika ipasavyo hali ilisababisha kudorora kwa chama
kipindi chote”alisema Ole Loilole Leng’isya katibu wa Wilaya.
Aidha katibu huyo alisema
chama kilitakiwa kufanya uchaguzi huo mwisho june 30 mwaka huu na kwamba kutokana
na sababu mbalimbali zilichangia kutofanyika.
Alitaja baadhi ya sababu
hizo kuwa ni pamoja na kukosekana kwa amani katika maeneo mengi ya wilaya ya
kiteto juu ya migogoro ya ardhi ambayo inaendelea hadi sasa na kusababisha
madhara yakiwemo mauaji.
Alisema hali hiyo imekuwa
tishio kwa wananchi na hata viongozi wa kisiasa na Serikali kwa ujumla
kuendelea kufanya kazi katika mazingira hayo kutokana na kitendo cha mauaji ya
kila mara huku kukiwa hakuna jitihada za maksudi kukabiliana na tatizo hilo.
Hata hivyo CHADEMA kwa
pamoja wamelaani mauaji yanayoendelea kujitokeza kwa jamii ya wakulima na
wafugaji wilayani humo na kuitaka Serikali kuzuia ili kuwapa wananchi waweze
kufanya kazi ya ujenzi wa Taifa.
Mwisho.
Maoni
Chapisha Maoni