MIGOGORO YA ARDHI 4 WAFARIKI AKIWEMO MTOTO WA MIAKA 6




mmoja wa wanajamii ya kifugaji (mmasai) aliyenusurika kuuawa mjini kibaya hivi karibuni akikimbizwa hospitali kutokana na migogoro ya ardhi  inayoendelea kujitokeza

Wanne wafariki Kiteto akiwemo mtoto wa miaka sita

  • ·        Watuhumiwa watoweka na ngombe zaidi ya 2000

Na Mohamed Hamad Manyara
WATU wanne wa jamii ya kifugaji (wamasai) Wilayani Kiteto Mkoani Manyara wameuawa kikatili katika matukio tofauti akiwemo mtoto wa miaka sita kisha kuporwa mifugo yao (ng’ombe) 2000

Tukio la kwanza limetokea kitongoji cha Engaloji kwa kuuawa watu watatu akiwemo mtoto wa miaka sita ambao kwa pamoja walivamiwa kisha kukatwakatwa na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za miili yao

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa Manyara Deusdeti Nsimeck amewataja marehemu hao kuwa ni pamoja na Makaloti Kitemela (70) Ngobilo Lengashumu (60) na mtoto mdogo Meshaki Ngonyani (6.5)

Kamanda Nsimeck amesema mbali na mauaji hayo wameporwa mifugo zaidi ya elfu mbili kisha kutokomea nayo kusikojulikana ambapo baada ya jitihada kubwa zilizofanywa na jeshi la polisi kwa ushirikiana na wananchi waliweza kuokoa baadhi ya mifugo hiyo


Amedai kuwa jumla ya ng’ombe 2296 ziliporwa na watu hao ambao walielekea katika moja ya chanzo cha maji kisha kupora mifugo mingine zaidi na kutoweka nayo ambapo hata hivyo  mifugo 2040 ilikamatwa katika maeneo mbalimbali ikisafirishwa

Watu 11 wanashikiliwa na Jeshi la polisi Wilayani Kiteto kwa tuhuma za mauaji pamoja na kukutwa na mifugo hiyo ambapo jitihada zaidi za kutafuta mifugo pamoja na watuhumiwa zikiendelea

Amesema Jeshi la polisi Wilayani Kiteto linaendelea na jitihada za kurejesha amani ambayo imetoweka katika maeneo hayo ambapo kila kundi limejiandaa kukabiliana na tukio hilo dhidi ya mwenzake

Tukio linguine la mauaji limetokea katika kijiji cha Dosidosi ambapo mwanaume mmoja aliyefahamika kwa jina la Paremalo Lembogwa (55) mfugaji amekutwa ameuawa karibu na nyumbani kwake na watu wasio julikana

Kwa mujibu wa kamanda huyo alisema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Aug 6 ambapo marehemu aliokotwa baada ya mwili huo kuonekana na wasamaria wema waliokuwa wanapita katika maeneo hayo na kutoa taarifa

Katika hatua hiyo Kamanda Nsimeck ameyataka makundi yanayohasimiana Wilayani Kiteto ambao ni wakulima na wafugaji kuacha mara moja tabia za kujichukulia sheria mkononi akisema kama kuna lalamiko lolote wafuate taratibu za kufikisha malalamiko yao kwenye vyombo vya sheria

Kamanda Nsimek ameliambia gazeti hili kuwa miili mitatu imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kiteto na kwamba mara baada ya upelelezi kukamilika watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zao

Matukio ya mauaji yameendelea kujitokeza mara kwa mara Wilayani Kiteto kutokana na kugombea ardhi jambo ambalo makundi hayo yaliomba Serikali kusaidia kutatua kwa kutengwa maeneo bila mafanikio

Maoni