HIFADHI YA EMBOLEY YAPORWA NA SERIKALI






Hifadhi ya Murtangos Kiteto kumilikiwa na Serikali

Na Mohamed Hamad Manyara
Serikali Wilayani Kiteto mkoani Manyara imeamua kupima na kuweka mipaka eneo la Emboley Murtangos linalogombaniwa na wakulima na wafugaji ambalo linasababisha maafa ya kila mara kati ya makundi hayo  na kuwa chini yao

Akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Martha Umbula alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya kukosekana kwa maelewano ya wakulima na wafugaji waliotenga eneo hilo na kufanya uharibifu

Eneo hilo limedaiwa kuwa na ukumbwa wa hekta laki moja na elfu thelathini na tatu ambalo lilitengwa na vijiji saba kama msitu wa jamii ambao utatumika kwa matumizi ya baadaye na hasa kutumia mazao ya msitu wakati wote katika maisha yao

 “Eneo hili ndugu zangu lilitengwa na vijiji saba kama msitu wa jamii na kwamba lengo lilikuwa ni kutaka kutunza msitu wa asili ili wananchi waweze kunufaika nao kama vile kupata mvua na hata  mazao ya msitu kwa kuokota kuni”

Alisema kilichotokea ni wakulima kuvamiwa eneo hilo kwa shuhuli za kilimo na kufanya uharibifu mkubwa hali ambayo vijiji viliomba Halmashauri kuwasaidia kuwatoa jambo ambalo lilifanyika kwa  mara kadha bila mafanikio

“Mvutano huu uliibua mgogoro wa kuuana wakulima na wafugaji ambao ulisababishwa na rushwa,ukabila,pamoja na ukosefu wa uadilifu wa baadhi ya viongozi wa Serikali jambo ambalo sasa Serikali imeliona na kulifanyia kazi”alisema Umbula

Mkuu huyo wa Wilaya alisema tume maalumu ya wataalamu 27 kutoka ofisi ya Waziri mkuu imewasili kwaajili ya kutatua migogoro hiyo ambapo pamoja na mambo mengine wataweka mipaka ya vijiji na hata wilaya na wilaya

Kiteto inakabiliwa na migogoro pande zote nne ambapo kuna mgogoro na wilaya ya Simanjiro,Kilindi,Kongwa,na Chemba ambapo kwa mujibu wa taarifa za tume wamedai wataweka mipaka kuondoa tatizo la kiutawala katika wilaya hizo

Mkuu  huyo wa Wilaya ametoa wito kwa wananchi wilayani humo kutoa ushirikiano kwa wataalamu hao ambao watapita katika maeneo tofauti kufanya kazi hiyo ambapo amedai kuwa tatizo la watu kuuana litamalizika kwa kuwekwa mipaka hiyo

Mainge Lemalali mwenyekiti wa Halamshauri ya Wilaya ya Kiteto katika hatua nyingine alisema migogoro ya ardhi haitamalizwa na wataalamu kama hapatakuwa na maridhiano ya wakulima na wafugaji ambao wao ndio chanzp cha migogoro hiyo

“Migogoro hii itamalizika tu endapo kutakuwa na maridhiano ya pande zote mbili wakulima na wafugaji kwani kinachosumbua hapa ni mvutano kila kundi halitaki kupoteza chochote jambo ambalo katika maridhiano haliwezi kusaidia”

Wakulima tukubali kupunguza maeneo yetu ya kilimo hali kadhalika wafugaji nao wapunguze mifugo na wafuge kulingana na maeneo walionayo haiwezekani mkulima mmoja kumiliki ekari 3000 na mfugaji kumiliki ngombe 3000 huku wakijua kuna changamoto alisema Lemalali

Mwisho

Maoni