MAHAKAMA NA CHANGAMOTO ZA UTOAJI HAKI MANYARA


Hakimu Elimu Massawe akihutubia wananchi ambao hawapo pichani siku ya sheria nchini ambapo kiwilaya ilifanyikia mjini Kibaya Picha na Mohamed Hamad Manyara


Mahakama na changamoto za utoaji haki Manyara

Na. Mohamed Hamad Manyara
Fursa ya utoaji haki nchini imekuwa na kauli mbiu ya utendaji kazi wa kila siku kwa taasisi zinazojishuhulisha ama kusimamia haki hasa katika nchi za Kidemokrasia zikiwemo za Afrika

Pamoja na hayo haki huendana na wajibu kwa mwenye haki hiyo kutambua fursa na mipaka yake inapoishia ndipo haki ya mtu mwingine inapoanzia kama moja na kigezo kikubwa cha msingi wa haki

Ni kutokana na ukweli kwamba hakuna haki isiyo kuwa na wajibu na wajibu mkubwa zaidi ni kuheshimu na kulinda haki za wengine wakati wote kama ibara ya 29 (1) na 30 (1) ya katiba ya Jamhuri na Muungano wa Tanzania inavyosema

Katiba imetaja haki mbalimbali sambamba na maelekezo kati ya mtu na mtu,ama vyombo na hata Taasisi zinazojihusisa na maisha ya kila siku ya binadamu kuyafanya kuwa endelevu

Ibara ya 107 A ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeunda mahakama zitakazokuwa na kauli za mwisho kwa kuzingatia masharti kuwa mtu ana haki kupata haki mahakamani anapozuiliwa kuipata ama kupokonywa na mtu mwingine

Wajibu wa Serikali

Serikali haina budi kuboresha mahakama na mazingira yake kuwa safi na endelevu kwaajili ya shuhuli za utoaji haki ambapo majaji na mahakimu ndio wenye jukumu la utoaji haki

Hata hivyo bila watumishi wa kada zingine mahakamani hapo kama walinzi,wahudumu,madereva makarani,wahasimu maafisa utumishi,wachumi,wahandisi na wachapaji kazi hiyo haitafana kama katiba ilivyoelekeza kuhusu utoaji wa haki

Akitoa hutuba Elimu Massawe Hakimu mkazi mfawidhi mahakama ya wilaya ya Kiteto na Simanjoro siku ya sheria nchini ambapo ilifanyika katika viwanja vya mahakama ya wilaya Kiteto alisema dosari zilizopo katika upatikanaji wa haki zinachangiwa na changamoto zilizopo

Alisema mazingira ya kazi ni magumu kwa watumishi ambapo Wilaya ya Simanjiro kuna mahakama nne tu za mwanzo kati ya hizo hakuna hata moja yenye jengo zaidi ya kuazimwa chumba kimoja ama viwili ndani ya ofisi ya kijiji ama kata ama mamlaka za maji

“Hivi kuna fursa ya kupata haki katika mazingira ambayo hakuna ofisi,hivi ndani ya chumba kimoja hakimu,karani, na mhudumu kwenye meza moja majalada yanatunzwa wapi?vielelezo udhibiti wake unakuwaje?alihoji Hakimu Massawe

Alisema mazingira haya hayafurahishi watumishi hivyo kuwaondolea ari ya kufanya kazi kwa ufanisi na kutia doa Idara ya mahakama katika kutoa haki kwa wananchi ambao Mahakam zimekuwa kimbilio siku zote la wanyonge kudai haki zao

Pia imeelezwa kuwa wilaya ya Simanjro haina mahakama ya wilaya na kusababisha adha kubwa kwa wananchi wake wakiwemo wa Sukuro na Nyumba ya Mungu ambao wanalazimika kusafiri umbali mrefu kusaka haki kupitia mahakama

“Hebu fikiria kutoaka Orkesmeti hadi Kibaya ni km 160 na kutoa Orkesmeti hadi Shambarai (mererani) ni km 122 kwa umbali huu ni mtanzania yupi atakayeweza kufuata haki yake”alisema Massawe

Alisema bila kuwepo na fursa sawia ya kupata haki hapatakuwepo na utawala wa sheria na Demokrasia ambapo mahakama ndio kimbilio na kwamba  wanaoonewa ama kukanganywa ni wananchi wa hali duni kimaisha

Maeneo ya Sunya, Dongo, Makame yaliyopo wilayani Kiteto ambako ni mbali na makao makuu ya wilaya yanapatia wapi haki zao?na je hali hii haisababishi wananchi kujichukulia sheria mkononi alihoji hakimu Massawe


Hata hivyo Hakimu Massawe alisema kuwa sambamba na changamoto hiyo za miundombinu bado kuna tatizo la maslahi duni ya wafanyakazi jambo ambalo nalo lilmekuwa likiwafanya watumishi hao kushindwa kutimiza wajibu wao

Akichangia hoja hiyo Christopher Parmet (mwananchi) alisema changamoto kwa idara hiyo ya mahakama imechangiwa na Serikkali kujisahau na kuona Mahakama kama mhimili ambao hauwahusu pamoja na kwamba ni chombo pekee na kimbilio la kupata haki kwa wananchi wote

“Mbona tuna ona agizo la Rais akiwataka watanzania kuchanga kwaajili ya maabara ama shule za kata na zinasimama kwanini mhimili wa mahakama unakuwa kama yatima” alihoji Parmet

Kwa upande wake wakili Jemsi Ole Milya alisema iko haja ya Serikali kutafuta mbinu za kuiokoa Idara ya mahakama ambayo kwa sasa imetelekezwa kwa muda mrefu ambayo tena wao wamekuwa mtari wa mbele sana kuitumia ili hali iko katika mazingira duni ya utendaji kazi

“Huwezi kudai haki eneo ambalo watu wake wanaukata wa fedha, majengo mabovu hayatoshi yanashawishi hata rushwa wakati mwingine na ndio maana utasikia mahakama zinalalamikiwa kwa wingi uhusu rushwa”alisema Milya

Mwisho

Maoni