MWANAMKE BABATI AKIMBILIA POLISI KUJISALIMISHA


Wasaidizi wa kisheria wakielekea kituo cha polisi Babati baada mwanamke aliyefahamika kwa jina laFausta Marandu kulia kufanyiwa ukatili wa kukatwa  kiganja na hawara yake bila kuchukuliwa hatua za kisheria Picha na Mohamed Hamad Manyara

Mwanamke ajisalimisha Polisi kuhofia kuuawa mumewe

·       Akatwa kiganja cha mkono,atembea nacho
Na. Mohamed Hamad Manyara
VITENDO vya ukatili wa kijinsi vinavyoendelea kujitokeza mkoani Manyara baada ya mwanamke mmoja mkazi wa kijiji cha Mayoka kuomba msaada wa ulinzi  kwa Jeshi la Polisi kuhofia kuuawa  na mumewe

Akiongea mbele ya Mkuu wa Polisi wa kituo cha Babati mwanamke huyo aliyejulikana kwa jina la Fausta Marandu (44) akiwa na wasaidizi wa kisheria alioambatana nao alisema ameamua kukimbilia Polisi kunusuru maisha yake

Awali mwanamke huyo alinusurika kuuawa na mumewe nyakati za usiku kisha kukatwa kiganja cha mkono wa kushoto hadi kikadondoka kwa kile kilichodaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi dhidi ya mume wake

“Hapa nina kiganja changu cha mkono natembea nacho mfukoni nilikausha mwenyewe baada ya kushauriwa niwe nacho kama kielelezo, kwamba ninapohitaji msaada nikionyeshe ili niweze kusaidiwa kwa haraka kupata haki zangu”alisema Fausta Marandu

Alisema awali aliishi na mwanaume huyo aliye mkata ambaye alijulikana kwa jina la Migire Amri (37) miaka mingi iliyopita na ulipofika mwaka 2011 ndipo akafanyiwa ukatili huo ambao alidai kuwa hatausahau maisha yake

Katika hatua hiyo alidai mwanaume huyo alipata adhabu ya kifungo cha miaka saba jela ambapo alitumikia kisha kutoka kwa msamaha wa Rais na kudai anataka kumalizia kiporo chake kutaka kumuua kama alivyokuwa amekusudia

“Nilienda Kituo kidogo cha Polisi Mgugu kulalamika lakini sikutiliwa maanani dhidi ya kutakiwa nirejee kwenye uongozi wa kitongoji na kijiji ambako walidai watanisaidia juu ya tukio hilo ambalo naamini kuwa mwisho wa siku nitauawa”alisema

Akizungumzia tukio hilo mkuu wa kituo cha Polisi Babati alisema atalivalia njuga kuhakikisha sheria inafuata mkondo wake na kwa waliosababisha kupoteza haki ya mwanamke huyo watachukuliwa hatua juu ya kilichotokea

Kwa upande wake Emmanuel Mgalla kutoka CELG ambao wanashuhulika na ukatili wa kijinsia aliwataka Polisi kuwajibila katika nafasi zao kuepuka kupoteza haki za watu akisema Taifa linahitaji uzalendo wa wananchi na viongozi wao kunusuri maisha ya watu

Mwisho

Maoni