Askofu Mhagachi awashangaa viongozi Kiteto



Na. Mohamed Hamad Manyara
Mwenyekiti wa tume ya maridhiano ya wakulima na wafugaji wilayani Kiteto mkoani Manyara Askofu Amos Mhagachi amekerwa na viongozi wa Kiteto ambao amedai hawawajibiki na kubaki kulalamika huku wananchi nao wakilalamika

Kila kada ya uongozi ukihojiana nao kuhusu  maendeleo ya wilayani na hata migogoro ya ardhi wanalalamika huku wananchi nao wakilalamika badala ya viongozi hao kuonyesha elimu zao kuusaidia umma ambao umechanganyikiwa juu ya yanayojitokeza kila siku yakiwemo mauaji kati ya wakulima na wafugaji

Askofu Mhagachi na kamati yake ya maridhiano iliyoundwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda jana katika ukumbi wa Halamshauri ya Wilaya walikutana na viongozi wa vijiji (watendaji) maafisa Tarafa,madiwani,pamoja na wakuu wa idara kwa nyakati tofauti juu ya sakata la migogoro ya ardhi

“Elimu zetu zinahitajika sana kwa wananchi mbona kila kiongozi akisimama hapa analalamika badala ya kutafuta ufumbuzi juu ya tatizo hili,naamini elimu ndio kila kitu na nafasi zenu hamkuzipata kwa bahati mbaya zitumieni vizuri ili wananchi wanufaike nanyi”alisema Akofu Mhagachi

Aliwataka viongozi hao kutumia elimu zao kukabiliana na changamoto zinazowakabili wananchi zikiwemo migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji pamoja na mendeleo mengine ambayo yatawasaidia wananchi kusonga mbele katika kukabiliana na umaskini wa kipato

Wakichangia chanzo cha mauaji hayo baadhi ya madiwani walionekana kutumia muda mwingi kutuhumiana juu ya maamuzi waliyokwisha fanyika siku za nyuma juu ya eneo la Emboley Murtangos kuwa limepitishwa kiubabe  kwa nguvu ya chama chenye madiwani wengi CCM

“Kuna madiwani tulikataa mpango huu usipite lakini kwa uchache wetu tulionekana wasaliti na hata viongozi wa CCM ngazi ya mkoa walitumika kufanya vikao vya kimila  kuchangisha fedha kwa jamii moja ya wafugaji ili wafukuzwe wakulima wao wanufaike”alisema diwani Kidawa Othmani CHADEMA

Kwa upande wao watendaji wa vijiji walikiri kuwa miongoni mwao wanatumika vibaya katika nyazifa zao kumilikisha watu ardhi zaidi ya ekari zisizotakiwa kutolewa na kijiji ili hali wakijua kuwa ni kosa jambo abalo limechangia migogoro hiyo huku wengine wajishindwa kusimamia sheria ipasavyo

Nao wakuu wa idara katika mahojiano hayo walidai kuwa chanzo cha migogoro hiyo ni uvamizi wa wananchi kutoka wilaya na mikoa ya jirani kwa shuhuli za kilimo zilizochangia uharibifu mkubwa wa mazingira

Katika Hatua hiyo Askofu Mhagachi na makundi hayo alisema dhana ya uwajibikaji kwa kila mtu wilayani humo imetoweka hivyo ili kuijenga upya Kiteto isiyo na migogoro kila mtu anatakiwa kuwajibika katika nafasi yake mwisho wa siku wananchi wanufaike

“Wajibikeni viongozi ili wananchi waone uwepo wenu kuwa una manufaa kinyume chake mtaonekana sawa na wale wananchi ambao hawajasoma hata darasa moja jambo ambalo ni hatari sana”alisema Mhagachi

Mwisho

Maoni