ASKOFU MHAGACHI NA MKAKATI WA KUIJENGA UPYA KITETO

Askofu Mhagachi na mkakati wa kuijenga upya Kiteto

Na. Mohamed Hamad Manyara
Kwa miaka mitano mfululizo wilaya ya Kiteto imeaandamwa na migogoro ya ardhi iliyoweka historia ya aina yake kati ya wakulima na wafugaji iliyotokana na vitendo vya ubaguzi wa kikabila, Rushwa pamoja viongozi kutowajibika

Hali hiyo ilisababisha uhasama mkubwa ndani ya makundi hayo kisha kutokuwa na imani na Serikali yao ambapo baadhi ya viongozi waliwagawa wananchi kwa misingi ya kikabila kutaka kuongoza

Madhara makubwa yalianza kujitokeza kwa wakulima na wafugaji kugawanywa kwa misingi ya ukabila na kujikuta wakiuana kwa madai ya kugombea ardhi iliyodaiwa kutumiwa kujipatia kipato kwa makundi hayo

Wakulima waliitumia ardhi hiyo kwa shuhuli za kilimo wakati wafugaji nao wakiitumia kwa kuchunga mifugo yao ambapo kwa uhitaji huo ulisababisha ugomvi wa kuvamiana na kuuana

Mapema mwaka jana wilaya iliweka historia zaidi ya watu kumi kuuawa katika maeneo ya pori kwa pori,kwa mtanzania na kalikala na baadaye saba katika vijiji vya matui na chekanao kwa kukatwa na vitu vyenye ncha kali shingoni,kupigwa risasi,pamoja na kuchomwa mikuki

Mauaji hayo yametokana na kile kilichodaiwa kuvamiwa  wakulima mashambani na kuuawa na wengine kujeruhiwa kisha baadaye wakulima nao kuungana na kulipiza kisasi kwa kuwafuata wafugaji kuwachomea makazi yao moto na hata kuwaua watoto na wanawake

Tafiti zinaonyesha chokochoko hizo zilianza kujitokeza miaka mitano iliyopita baada ya mabadiliko mbalimbali ya kiutawala ambapo kila kiongozi alikuja na mfumo wake wa kutawala ili aweze kukubalika kwa wananchi

Baada ya Serikali kuona hali hiyo iliweza kufanya mabadiliko makubwa kila mara hasa katika ngazi za juu za uongozi wa Wilaya lakini hali ilizidi kuwa tofauti na matarajio ya viongozi hao dhidi ya wananchi

Katika kuhakikisha amani inarejea kama Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyewasili kushuhudia mauaji hayo na kutembelea eneo la kwa Mtanzania feb mwaka jana na kuwaahidi wananchi kuunda tume ya kuchunguza mauaji na kutoa agizo la kukamatwa wauaji hao

Watu 16 walikamatwa na kufunguliwa mashitaka ya tuhuma za mauaji ambapo baadaye waliachiliwa kwa madai kuwa hakuna ushahidi wa wazi kuwa wamehusika na mauaji hayo ya watu kumi katika maeneo ya kalikala,olpopong,na kwamtanzania

Mwezi Aug mwaka jana mauaji tena yaliibuka katika vijiji vya matui na chekanao ambapo watu saba walipoteza maisha akiwemo mwanamke mmoja kutokana na ghasia hizo ambapo Serikali ilijitokeza na kukamata watu 16 kisha kuwafungulia mashitaka ya mauaji

Mbali na hatua hiyo tume kadha ziliudwa na Waziri Mkuu kwaajili ya kuchunguza matukio hayo ikiwemo tume ya viongozi wa dini ikiongozwa na Askofu wa Kanisa la Mennonite Tanzania Amos Mhagachi kwa lengo la kukabiliana na tatizo hilo

Kwa mujibu wa Askofu Mhagachi akizungumza na vyombo vya habari aliwahakikishia umma kuwa migogoro hiyo itamalizika endapo pande hizo zitakubali maridhiano sambamba na kukataa kutumika kisiasa na kikabila

Alisema kuna kikundi kidogo cha watu wanaonufaika na migogoro hiyo na kukitaka waache mara moja kwani serikali imegundua na sheria itaanza kufuata mkondo wake ili kunusuru maisha ya watu wasio na hatia 

Alisema katika kukabiliana matatizo hayo baada ya kuteuliwa na Waziri Mkuu walikutana na viongozi mbalimbali wa wilaya kufanya mahojiano na kisha kuanza kuzungumza na wananchi vijijini na sasa wamerejea tena kuzungumza na makundi mengine ya viongozi

“Tupo hapa sote tuna wajibu wa kuhakikisha tunarejesha amani ya wananchi wa Kiteto iliyotoweka kwa maslahi ya baadhi ya wenzetu wachache, tusikubali hata kidogo kuona amani ikitoweka kwani kuirejesha ni kazi” alisema Askofu Mhagachi

Alisema kazi ya kamati yake ya viongozi wa dini na wataalamu mbalimbali sio kuhukumu wakosaji bali ni kuhakikisha amani inarejea kwa wakulima na wafugaji iliyotoweka na kusababisha makundi hayo kushindwa kufanya kazi za maendeleo

“Pamoja na kubaini kuwepo kwa ukabila na kutowajibika kwa baadhi  ya viongozi baada ya kufanya mahojiano nao pamoja na wananchi wao tutakuwa na taarifa moja tutakayoiwasilisha hivi karibuni kwa Waziri Mkuu”alisema  Askofu Mhagachi

“Nilichokuta kwa wananchi wao wanasema awali waliweza kuishi pamoja wakisaidiana na kufanya kazi za kiuchumi kati ya wakulima na wafugaji na baadaye siku za karibuni makundi hayo yaligombanishwa na wajanja wachache kwa maslahi yao” alisema

Alidai kwa mazungumza aliyoyafanya kwa kukutanisha pande hizo na kukubali kuongea watarejea katika hali yao ya kawaida kwa kuaminiana huku akiwataka wasikubali kugombanishwa kwa maslahi ya kisiasa na kikabila

ITAENDELEA WIKI IJAYO…..

MWISHO

Maoni