KITETO HALI SI SHWARI, MAUAJI YAENDELEA


NA.MOHAMED HAMAD MANYARA
Hali ya amani wilayani Kiteto mkoani Manyara inazidi kuwa tete kutokana na mauaji ya kimyakimya yanayoendelea kujitokeza mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji pamoja na uhalifu wa kuibiana mifugo.

Pamoja na kuwepo jitihada za Serikali kukabiliana na uahalifu huo bado hali sio shwari kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za mamlaka zinazohusika kukabiliana na matatizo hayo “kudanganywa”

Toka Waziri Mkuu Mizengo Pinda aunde tume ya maridhiano ya wakulima na wafugaji zaidi ya watu watano wamepoteza maisha akiwemo Msafiri Mwama (50),Bw. Msukuma Aneti (48) na mtoto wa miaka miwili aliyepigwa risasi akinyonya na mtu asiyejulikana katika Kijiji cha Lortepes

“Tunapoeleza ukweli kwa viongozi ngazi ya Taifa juu ya yanayoendelea kutokea Kiteto tunaonekana waongo kutokana na taarifa za wilaya zinazoandaliwa kwa viongozi hao mara wanapofika”alisema Bakari Maunganya (mwananchi)

Baadhi ya viongozi wa Wilaya ya Kiteto akiwemo aliyekuwa mkuu wa Wilaya na Mbunge viti maalum (CCM) Martha Jaki Umbulla aliwahi kueleza Bunge, Kiteto ni shwari akipingana na aliyekuwa mkuu wa Polisi Wilaya Foka Dinya ambaye alisema mauaji yanaendelea

Alisema tofauti hizo ndizo zilizochangia matatizo hayo ambayo kwa sasa Serikali imetumia gharama kubwa kuunda tume na kamati mbalimbali kwaajili ya kuchunguza na hata kuandaa ripoti ya Serikali juu ya kinachoendelea Kiteto

Hivi karibuni Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliunda tume ya maridhiano ya wakulima na wafugaji ambayo inaendelea kukutanisha makundi mbalimbali ya wananchi kusaka amani hiyo ambayo inazidi kutoweka

Mbali na tume hiyo pia Bunge liliunda kamati maalumu kuchunguza migogoro hiyo na kuwasilisha taarifa Bungeni, kazi ambayo imedaiwa kuwa imetumia gharama kubwa za wananchi ambazo haikuonyesha mafanikio yake

Kuhusu uhalifu wa wizi wa mifugo kila mara matukio yameendelea kujitokeza ambapo zaidi ya ng’ombe 20 za Diwani wa kata ya Magungu (CCM) Daudi Mwedimage ziliporwa hazikuonekana hadi hii leo

Kutokana na wizi  wa mifugo unaoendelea kijitokeza watu wanne  wanashikiliwa na polisi Kiteto kwa tuhuma za wizi wa mifugo zaidi ya 70 ya familia ya Bw. Farah ambayo 43 ilipatikana baada ya mchungaji kuporwa akiwa machungajini

Mwisho

Maoni