Kiteto waomba kanda maalum ya kipolisi


Kiteto waomba kanda maalum ya kipolisi

NA.MOHAMED HAMAD MANYARA.
Wananchi wilayani Kiteto mkoani Manyara wamependekeza waundiwe kanda maalumu ya Kipolisi kudhibiti uhalifu unaoendelea kujitokeza wilayani humo ukiwemo mauaji ya wakulima na wafugaji kwa wakigombea ardhi. 

Wakiwasilisha malalamiko yao mbele ya Tume ya maridhiano iliyoundwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda mjini Kibaya jana walisema mauaji hayo yamekuwa yakijirudia huku kukiwa hakuna jitihada za dhati kukabiliana nayo

“Tumeshuhudia wakulima na wafugaji wakiendelea kupoteza maisha kuanzia miaka mitano iliyopita wakati awali tulisaidiana katika mfumo wote wa maisha yetu lakini kutokana na mabadiliko ya utawala tumeingia kwenye matatizo makubwa”alisema Ibrahimu Msindo (mwananchi)

Alisema pamoja na kuwepo tume ya maridhiano na kamati ya upimaji wa ardhi kama moja ya njia ya kutatua tatizo kama hapatakuwa na ulinzi katika maeneo yanayogombaniwa ya Emboley Murtangos bado watu wataendelea kuuana kwasababu wamegonganishwa kwa misingi ya kisiasa na ukabila


Alidai katika maeneo hayo kuna wanaoruhusiwa kuwepo na wasioruhusiwa jambo ambalo ni ubaguzi mkubwa na wala halitavumilika kundi moja kunufaika na ardhi huku wengine wakiitwa wavamizi halikubaliki alisema Msindo

Akiwashauri wananchi hao kuachana na wazo hilo la kuundiwa tume Askofu Amos Mhagachi mwenyekiti wa kamati ya maridhiano ya wakulima na wafugaji Kiteto alisema kanda za kipolisi zina madhara makubwa kwa wananchi yakiwemo kukosa uhuru

“Mngefahamu madhara ya kanda maalumu ya Kipolisi  msingeomba ulizeni, wenzenu mimi nimetoka Tarime kule wanasachiwa mpaka kwenye soksi masuala ya ulinzi hayo…sasa mnataka kusachiwa mpaka kwenye soksi” alihoji Askofu Mhagachi

Kauli za Askofu mhagachi juu ya pendekezo hili zikawafanya wananchi hao kusinyaa na kupata hofu kubwa juu ya pendekezo lao la kuingizwa kwenye kanda ya Kipolisi huku wakiendelea kunungunika chinichini kutaka ushauri zaidi juu ya namna ya kukomesha mauaji

Katika hatua hiyo wananchi hao walipendekeza kamati hiyo ya maridhiano iwakamate viongozi wa Kisiasa wote wakiwemo madiwani pamoja na Mbunge wao kwa kudaiwa kuchochea mgogoro uliochangia mauaji kati ya wakulima na wafugaji

Akijibu hoja hiyo mwenyekiti huyo wa kamati alisema kamwe hawawezi kujiiingiza kwenye kazi isiyowahusu ya kukamata watu akidai kuwa ni ya polisi huku akiwalaumu wananchi kwa kushindwa kufanya maamuzi ya busara ya kuwapata viongozi wao

Mwisho


Maoni