Mafuriko ya mvua yasababisha watu 70 kukosa makazi Manyara


Mafuriko ya mvua yasababisha watu 70 kukosa makazi Manyara

NA MOHAMED HAMAD MANYARA
JUMLA ya watu 70 wamekosa makazi na kuhifadhiwa katika majengo ya shule ya msingi Magugu iliyopo mji mdogo wa Babati mkoani Manyara baada ya nyumba zao kuangushwa na mvua

Tukio hilo limetokea April 9 mwaka huu baada ya mvua kubwa kunyesha na kusababisha mafuriko kwenye makazi ya watu ambapo awali nyumba 10 ziliripotiwa  kuanguka na baadaye kuongezeka zingine na kufikia 66

Kwa mujibu wa John Jeu kwa niaba ya makamu Mkiti wa Halmashauri ya Babati alidai mafuriko hayo yamesababisha hasara kubwa kwa wananchi ambayo haijafahamika mapema na kuwataka wadau kujitokeza kusaidia janga hilo

Mkuu wa mkoa wa Manyara kupitia RAS ametoa msaada wa magodoro 48 na wadau wengine kama makampuni ya CHRISHNA SEEDS na MAGUGU FARM chini ya wakurugenzi wao Babu Atia na Atia Visa  walitoa msaada wa vyakula mbalimali katika kambi hiyo

Awali Mkurugenzi wa kampuni ya CHRISHNA SEEDS Atia Visa na MAGUGU FARM Babu Atia wakikabidhi msaada kwa Mwenyekiti wa kijiji hicho Abdallah Mbonde walisema wameguswa na maafa hayo na kusaidia wahanga waliokumbwa na tatizo hilo

“Tumetoa mifuko mia moja ya unga yenye kilo tano,mbuzi wawili,chumvi,mafuta ya kupikia lita 40,pamoja na maziwa lita 20,magunia mawili ya mahindi tukilenga kuwawezesha wakati huu ambao Serikali inaendelea kujipanga kuwasaidia”alisema Babu Atia na Atia Visa

Kwa upande wa mama Khadija Rajabu mhanga wa mafuriko hayo akizungumza na MTANZANIA aliomba Serikali kuharakisha msaada zaidi wa kibinadamu kutokana na mazingira wanayoishi kuhofia afya zao kutokana na magonjwa ya milipuko

“Tunaiomba Serikali iwe karibu, na  itusaidia zaidi tunashukuru kwa  magodoro na vyakula tulivyopata kutoka kwa wenzetu wahisani zipo changamoto nyingi kama hofu ya magongwa kulinda afya zetu, tunahofu kuwepo kwa magonjwa ya mlipuko hapa kituoni”alisema Masherebu Issa mwenyekiti wa kamati ya huduma za jamii

Kwa Upande wake Abdallah Mbonde Mwenyekiti wa kijiji cha Magugu alivishukuru vyombo vya habari ambavyo viliwahi na kuujulisha umma juu ya madhila yaliyowapata wananchi hao ambapo sasa wameanza kunufaika na misaada

“Binafsi nisema kuutoka moyoni vyombo vya habari vimekuwa msaada mkubwa kwa wahanga kwani bila ya kutangaza habari hizi leo dunia isingejua kilichotokea na kuja kutufariji hapa naomba muendelee na moyo wenu huu”alisema Mbonde wakati akiongea na vyombo vya habari

Mwisho
                                


Maoni