Mwanafunzi auawa kwa kufeli mtihani


Mwanafunzi auawa kwa kufeli mtihani
·        Achapwa vipoko 12 kwa walimu kupokelezana
·        Walimu watatu mbaroni
·        CWT Kiteto wadai viboko vinafundisha
·        Familia wasusa maiti,wadai uchunguzi zaidi

NA. MOAHAMED HAMAD MANYARA
Mwanafunzi Emmanueli Mbigima (15) wa kidato ya pili shule ya Sekondari Matui iliyopo wilayani Kiteto Mkoani Manyara amepoteza maisha kwa kuchapwa viboko 12 na waalimu kwa tuhuma za kufeli mtihani wa Kiswahili

Tukio hilo limetokea majira ya saa nne baada  wanafunzi wengi wa kidato cha pili kufeli mtihani huo wa kiswahili ulioandaliwa na mwalimu wao kisha kuanza kuchapwa viboko na waalimu watatu wa shule hiyo

Kifo cha mwanafunzi huyo kinaongeza idadi ya wanafunzi watatu waliopoteza maisha ndani ya miaka minne katika maeneo tofauti wilayani Kiteto kwa madai ya kucharazwa mboko na waalimu wao wakiwa shuleni

Kamanda wa Polisi na kamishna msaidizi wa Polisi Mkoani  Manyara Christopher Fuime amewataja waalimu watatu wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za mauaji dhidi ya mwanafunzi huyo

“Jumla ya waalimu watatu akiwemo Machael Bajutta (28), Chalamilla Gereza (33) na Joyce Msiba (36) wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi baada ya madai ya kuhusika na adhabu hizo”alisema Kamanda Fuime

Alisema uchunguzi zaidi utafanyika baada ya familia ya marehemu kuja na daktari wao waliyedai kutokana na kutokuwa na imani na daktari juu ya tukio hilo ambalo wanadai kuwepo kwa mianya ya rushwa

Familia
Kwa mujibu wa Emmanuel Ngowi msemaji wa familia ya marehemu alisema wangependa kuona haki ikitendeka pande zote tofauti na mazingira ya rushwa yanayoandaliwa  baada ya kutokea tukio hilo za kutaka kutolewa taarifa za uongo

“Baada ya kwenda na mwili wa marehemu kituo cha Polisi Kibaya kauli za baadhi ya askari zinakatisha tamaa na kuona kuwa haki haiwezi kutendeka kutokana na madai yao kuwa eti marehemu alikuwa mgonjwa na alitoroka Hospitali jambo ambalo sio kweli”

Alisema marehemu hakuugua kwa siku za hivi karibuni na kupelekwa Hospitalini kulazwa, kauli hizi zinaashiria kulindana na huenda haki haitatendeka kwa kuwaachia madaktari wa Kiteto peke yao na badala yake familia tumeagiza Daktari wetu wa kushirikiana naye

Alitaja sababu zaidi za kuandaa daktari wao kuwa ni pamoja na matukio mengine ya wanafunzi wawili katika maeneo tofauti kuwa nao walipoteza maisha kwa tuhuma za kucharazwa mboko na waalimu kisha kufumbiwa macho

“Kuna mwanafunzi mmoja wa shule ya msingi Bwawani Kijiji hiki cha Matui mwaka jana na mwingine Mbeli mwaka juzi walipoteza maisha kwa tuhuma za kucharazwa viboko huku taarifa za uchunguzi zikionyesha kuwa walikuwa na matatizo ya kiafya jambo ambalo sio kweli”alisema Ngowi

Wanafunzi
Kwa upande wa wanafunzi wa shule ya sekondari matui wamezungumzia tukio hilo kuwa ni kitendo cha ukatili kilichofanywa na waalimu hao wakisema imekuwa ni mazoea kutoa adhabu za viboko wakidai kuwepo kwa kauli za baadhi ya walimu kuwa huo ndio utaratibu mzuri wa mafunzo kwa mwanafunzi wa Kitanzania

Walisema pamoja na kuwepo kwa sheria zilizowekwa katika adhabu bado waalimu wamezidi kukiuka na hata wakiripoti kwa wazazi wao huambulia kutakiwa kuvumilia na kwamba mwisho wa siku watamaliza shule na kurejea nyumbani

Kwa upande wake Khadija Mustafa wa Kiteto Sekondari kuhusu tukio hilo alilaani akisema huo ni ukatili wa hali ya juu ambao kwa sasa umepitwa na wakati kwani hakuna mafunzo yanayofanyika kuwa kupigwa bali zitafutwe njia mbadala huku akisisitiza sheria ya adhabu izingatiwe

CWT Kiteto
Chama cha waalimu wilayanin Kiteto kimesikitishwa na tukio hilo na kuomba uchunguzi zaidi ufanyike kuondoa malalamiko dhidi ya familia hiyo waliyodai waalimu wameungana pamoja kuchanga fedha kumsaidia mwalimu mwenzao atoke

Akizungumza na MTANZANIA Paulo Gwacha mwenyekiti wa chama hicho alisema haamini kuwa viboko 12 vinaweza kumuua mwanafunzi hata kama ni kwa kupokelezana kuwa waalimu hawakuwa na dhamira mbaya

“Viboko kwa mwanafunzi wa kitanzania ni muhimu vinasaidia sana kwani hata sisi tulichapwa ndio maana tuko katika nyazifa hizi sasa kilichotokea huyu mtoto taarifa za awali ni kwamba alikuwa anaumwa”alisema Gwacha

Kwa upande wake Faostine Salala Mkaguzi wa elimu Kiteto alisema suala la viboko limeundiwa utaratibu wake shuleni ambao mwanafunzi ataadhibiwa mwisho ni viboko vitatu na  taarifa ziandikwa kwenye kitabu cha shule kuhusu adhabu hiyo na sio vinginevyo

Alisema hatua hiyo imetokana na taratibu zilizopitishwa kisheria na atakayevunja sheria mkondo wake utafuata hivyo kitendo kilichofanywa na mwalimu Bajula kumchapa mwanafunzi viboko 8 kisha waalimu wengine wawili kumchapa vinne kwa wakati huo ni kosa

Mkuu wa Wilaya
Mkuu wa wilaya ya Kiteto Kanali Kimiang’ombe Nzoka na mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama akiongea ofisini kwake alisema Jeshi la polisi limetuliza mzuka wa wananchi waliokuwa wameandamana kwenda shuleni na Kituo kidogo cha polisi matui kutaka kufanya uhalifu

“Hali ya amani ni shwari na mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Wilaya ya Kiteto na bado haujafanyiwa uchunguzi mpaka ndugu wa marehemu wafike na mchana huu naenda kuongea na wananchi hao”alisema Mkuu huyo wa Wilaya

Kwa upande wa baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Matui wameitaka Serikali kufanya uchunguzi wa kina kwani matukio hayo ni ya kujirudia kwani katika eneo lao hilo hili ni tukio la pili na hakuna hatua iliyochukuliwa

“Tunashuhudia uhalifu kila mara wa aina mbalimbali ukifanyika Kiteto na baada ya muda watuhumiwa wanaachiwa huru wahalifu wakiendelea kutamba mitaani hatukubaliana na kinachofanyika”walisema wananchi hao bila kutaja majina yao wakati wakiongea na gazeti hili

Mwisho

Maoni