CHADEMA CHAFANYA UCHAGUZI KUWAPATA WAGOMBEA UBUNGE




GEKULI:Tusiposhika Dola mwaka huu hatutaweza tena

NA. MOHAMED HAMAD MANYARA
Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA) Mkoa wa Manyara Paulina Gekul amesema, kama CHADEMA hakitashika Dola mwaka huu uwezekano wa kushika hautakuwepo tena baada ya miaka 50 ijayo

Akizungumza leo (jana) kwenye mkutano mkuu wa chama hicho wilayani Kiteto Gekul alisema, nafasi ya UKAWA kushika dola mwaka huu ni kubwa kwani wananchi wamejitambua tofauti na miaka iliyopita kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo vitisho vya utawala wa CCM

“Kuna viashiria vingi sana vinavyo onyesha UKAWA kushika Dola naamini CCM watakimbilia mahakamani baada ya kuangushwa, kwani walitegemea kuona wananchi wakibaki mbumbumbu badala yake kila mmoja sasa ameamka na anajitambua”

“Bila shaka mnafahamu kilichofanyika Bungeni, wabunge tumepambana vya kutosha mmeona hali halisi ya nchi yetu imefilisiwa na mafisadi hapa ilipofika kila eneo hali imekuwa ngumu si kwa vijana wala wazee twendeni pamoja safari yetu tufike salama, tujiunge na jeshi la ukombozi kuwaadhibu CCM mwaka huu”alisisitiza Gekul

Aliwataka wanachama hao kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kuanzia ngazi ya chini  mpaka juu akisema wasiachie hata moja, kwani ikiachwa wazi inawapa kiburi CCM kujiona kuwa bado wana haki wa kuendelea kuwa madarakani

Hata hivyo mkutano huo ulilenga kuchagua mwanachama mmoja atakayepeperusha bendera ya CHADEMA katika nafasi ya Ubunge, pamoja na Ubunge Viti maalum ambao majina yao yatawasilishwa Taifa kwaajili ya uteuzi zaidi

Waliojitokeza kuwania nafasi ya ubunge wa Jimbo ni Pascal William Chibala na Kidawa Othman Kidawa, huku viti maalum Ubunge wakiwania wanachma watatu Sisca Seuta Seuta,Angela Raphael Laiza na Mery Thomas Temba

Akizungumzia nafasi ya viti maalum Mwenyekiti huyo alisema kwa waliojitokeza wana nafasi kubwa kwani walitakiwa wawe kumi badala yake wamejitokeza watatu na baada ya uchaguzi huo majina yao yatawasilishwa Taifani kwa uteuzi

Kuhusu wagombea wa Jimbo alisema nafasi inayotakiwa ni moja hivyo wajumbe wanatakiwa kuwa makini kumpata atakayejibu matatizo ya wananchi na anayekubalika kwa wote ili iwe rahisi kunadiwa kwani kwa wilaya ya Kiteto ni rahisi kutokana na changamoto zilizojitokeza

“Kiteto kuna mauaji ya kila mara,huduma duni za afya,elimu,maji nakadhali sasa mnataka nini CCM wataeleza nini yao ngumu mwaka huu, hatuwezi kucheka na nyani tutaendelea kuvuna mabua”alisisitiza Mwenyekiti huyo

Kwa upande wa wanachama hao walisema matarajio ya UKAWA kuchukua Jimbo ni makubwa kutokana na mauaji yaliyotokea chini ya utawala wa CCM, huku kukiwa hakuna jitihada zozote zilizochukuliwa nna utawala huo

Akizungumza kwa hisia kali Salmu Ramadhani Mambo (mjumbe) kutoka kata  ya Kijungu alisema tume kadhaa ziliundwa na Serikali baada ya kujitokeza mauaji ya wakulim ana wafugaji lakini hazijazaa matunda kutokana na kukosekana kwa ufuatiliaji wa kina

Huwezi kuwa na kiongozi bubu ambaye hasemi, tulitegemea Mbunge wetu Benedict Nangoro awe mstari wa mbele katika kuelezea hili na kuonyesha hata dhamira ya kushuhulikia lakini imekuwa kinyume chake watu wamezidi kuuana mpaka sasa hatujui hatma yake

Akizungumza hivi karibuni kwenye mikutano ya CCM kuomba ridhaa wananchi kumteua tena kugombea jimbo la Kiteto Benedict Ole Nangoro alisema hakuwa na chakusema katika mgogoro huo kwani hatua zaidi zilikwisha kuchukuliwa na mamlaka husika ambazo ni Serikali

“Sikuweza kuingilia kwani tuliona Serikali imechukua hatua,watu wamekamatwa na kufikishwa mahakamani hapo mbunge kusema ni sawa na kuingilia mahakama kazi yake hjambo ambalo ni kosa kubwa”alisikika akisema huku akizomewa na wananchi wa kata ya Njoro kwa kauli hiyo

MWISHO

Maoni