MAUAJI YA WAKULIMA NA WAFUGAJI KITETO NI MPAKA LINI?




Mauaji Kiteto ni mpaka lini?

NA.MOHAMED HAMAD
Mauaji ya wakulima na wafugaji Kiteto ni mpaka lini? hili ni swali ambalo si tu wananchi wa Kiteto wanajiuliza bali ni watanzania wote kwa ujumla wakitaka majibu sahihi bila mafanikio

Jibu hilo linasubiriwa kutolewa na ofisi ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambayo imedaiwa kushuhulikia suala hili toka mauaji hayo yalipoanza muda mfupi baada ya kufariki aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kiteto Benedict Loosurutya (CCM)

Kila mara taarifa zimekuwa zikitolewa na mamlaka husika kuhusu vifo vya wakulima kuuawa wakiwa mashambani na baadhi ya wafugaji kwa madai kuwa wamevamia maeneo ya mifugo na kufanyaka shuhuli za kilimo

Waungwana wanasema uhalifu huu hauvumiliki hata kidogo,na ndio maana tume kadha wa kadha ziliundwa na Waziri mkuu mzengo Pinda wilayani Kiteto kutafuta suluhu bila mafanikio

Tume ya viongozi wa dini chini ya Askofu Amos Mhagachi wa kanisa la MENONITE aliyekuwa mwenyekiti wa tume iliyoundwa na Waziri mkuu kwaajili ya kufanya suluhu ya mgogoro wa wakulima na wafugaji Kiteto ilimaliza kazi yake

Kazi ya tume hiyo ilikuwa ni kuhakikisha inakutana na makundi yote kuzungumzia amani pamoja na kupokea kero mbalimbali za wananchi juu ya mauaji hayo kwa hatua zaidi zitakazochukuliwa na Waziri Mkuu Pinda

“Nimekutana na makundi yote wakulima,wafugaji,pamoja na viongozi mbalimbali juu ya mauaji haya ambayo wameyaita kwa majina tofauti,wapo waliofananisha na mauaji ya kibari,wengine Somalia,kutokana na jinsi watu wanavyouawa”alisema Mhagachi

Alisema nafasi aliyonayo pamoja ni kuandaa taarifa  kutoka kwa wananchi kisha kuipeleka kwa aliyemteua ili naye aweze kufanya maamuzi ambayo yanaweza kusaidia wananchi wa Kiteto wasiweze kuendelea kupoteza maisha

Kwa mujibu wa mwenyekiti hiyo alisema taarifa za awali zinaonyesha mauaji hayo yamechangiwa na ukabila uliopo kwa baadhi ya viongozi,rushwa kwenye mamlaka za uongozi mbalimbali katika kutoa haki,pamoja na kukosekana kwa dhamira ya dhati kushuhulikia tatizo

“Haya mambo matatu ni muhimu sana kushuhulikiwa kwa haraka kwani yasiposhuhulikiwa watu wataendelea kufa wakigombea ardhi huku viongozi wa Wilaya wakishindwa kusimamia majukumu yao kwa hofu ya usalama wao”

Tume nyingine ni ya upimaji wa mipaka iliyoundwa na Waziri mkuu ambayo nayo ilikamilisha kazi yake na kuiachia Serikali ya kiteto kuhakikisha kuwa wanasimamia sheria ipasavyo

Zaidi ya vijiji 50 kati ya 68 vimefikiwa na tume hiyo ya upimaji wa ardhi kupimwa maeneo kwa kuweka matumizi bora ya ardhi kama vile kilimo,mifugo,makazi na maeneo ya hifadhi na kwamba kazi iliyobaki ni kulinda sheria

Kamati nyingine iliyofika Kiteto ni ile iliyoundwa na Bunge kuchunguza mauaji na kutoa taarifa Bungeni kuhusu mauaji yanayoendelea kujitokeza kila mara na kutoa taarifa ambapo iliwasilisha taarifa yao Bungeni

Mbali na wataalamu hao wa Serikali pia waliweza kufika viongozi wa mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali ya haki za binadamu LHRC kutoka Arusha kwaajili ya kuangalia ukiukwaji wa haki hizo na kutoa taarifa zao

Ziara ya viongozi wa Chama cha mapinduzi CCM ikiongozwa na Abdulrahmani Kinana katibu mwenezi Nape Nnauye nao walilaani mauaji hayo wakisema wataenda kumweleza Rais Jakaya mrisho Kikwete juu ya walichokiona Kiteto

“Nimesikitishwa sana na haya mliyoniambia wananchi wa Kiteto naona tatizo ni uroho wa madaraka ndio unaoua watu, sasa nitaenda kumwambia bwana mkubwa ili aweze kuchukua hatua ingekuwa ni mimi ningeweza kufanya hivyo lakini anapaswa yeye”alisema Kinana

Jitihada za kuwakamata wahalifu chini ya Jeshi la Polisi zimeendelea kila kukicha na wahalifu kufikishwa mahakamani lakini wamekuwa wakiachiwa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kukosa ushahidi kuthibitisha tukio hilo

Taarifa za uhakika kutoka Jeshi la polisi na waathirika zinasema kuwa vijana wa jamii ya kifugaji wamasai wamekuwa tishio la kuwaua wakulima shambani kwa kuwakata kata mapanga wakitaka waachiwe kuchunga mifugo yao shambani

Kwa mujibu wa madai ya wafugaji ni kwamba huwa wamevamiwa na wakulima katika maeneo yao, na kwamba mkakati uliopo ni kurejesha maeneo hayo kwa kufanya uhalifu huo ili wakulima waogope na wawapishe katika maeneo hayo

“Haiwezekani wakulima wakalima mpaka katika maboma yetu, unawezaje kumzuia ng’ombe asikimbilie shambani kwa kuona mahindi hayo ambayo ni majani yakiwa yamenawiri”alisema Kisioki Mesiaya (mfugaji)

Alisema mbali na tatizo hili uongozi wa wilaya ya Kiteto uliamua kuwachonganisha wakulima kwa kuchangisha fedha wafugaji ili waweze kuwaondoa wakulima katika maeneo yanayogombaniwa ya Emboley Murtangos

Kwa upande wa wakulima walisema jamii ya kifugaji masai wamekuwa wakulima wakubwa na maarufu na wanachofanya ni kuajiri watu kufyeka na kuwataka walime kwa miaka miwili kisha waondoke ili wao waendelee kulima

“Wakishafyeka wanalima kisha kuuza maeneo hayo kwa watu wengine ambao nao huendelea na kilimo huku wao wakiwa wamehamia katika maeneo mengine na kusema wamevamiwa”alisema Bakari maunganya (mkulima)

Uchunguzi uliofanywa na MAKALA hii umebaini kuwa hakuna aliyewahi kutiwa hatiani kwa mauaji ya zaidi ya watu 40 yaliyotokea mwanzoni mwa mwaka 2014 yaliyosababisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda kufika na kutoa pole kwa wahanga

Hata hivyo mauaji hayo mara nyingi wakulima hukutwa wakiwa wamekufa mashambani baada ya kukatwakatwa mapanga ama kufia hospitali na kukamatwa mifugo kisha wahusika kujitokeza na kufunguliwa kesi za mauaji

Kwa mujibu wa habari za uhakika zaidi ya wafugaji 20 wa jamii ya kimasai wanatuhumiwa kwa makosa ya mauaji mahakama ya wilaya ya Kiteto na kesi zao zinaendelea ambapo wadadisi wa mambo walisema mahakama ni chombo cha kwisho katika kutoa haki

“Ujue hakimu akitaka kukuhukuma huwa anakueleza kuwa ushahidi ni ule utakaothibitishwa bila shaka, mauaji yanayofanyika huwa mifugo inatelekezwa kisha kuokotwa sasa hakimu anatafuta aliyeona mauaji yakifanyika unamtiaje hatiani mmasai hapo”alisema mmoja wa wananchi Kiteto

Kwa sasa hakuna anayejua kuwa lini mauaji hayo yataisha pamoja na kuwepo kwa taarifa za viongozi wa Serikali akiwemo Kanali Samuel Nzoka mkuu wa Wilaya ya Kiteto kuwa atakomesha mauaji hayo na wala hatamwonea haya mhalifu


INAENDELEA WIKI IJAYO….0758 222 248 masarade1995@gmail.com

Maoni