Shehena ya madawa ya kulevya yakamatwa Kiteto





Shehena ya madawa ya kulevya yakamatwa Kiteto

JUMLA ya kilo 185 za madawa ya kulevya aina ya mirungi zimekamatwa katika eneo la kaachini kata ya Njoro wilayani Kiteto mkoani Manyara, zikiwa zinasafirishwa kutokea Kenya kuelekea Wilaya ya Kondoa iliyopo Mkoani Dodoma.

Kukamatwa kwa shehena hiyo imekuwa ni mwendelezo wa ukamataji wa madawa hayo ambapo hivi karibuni jumla ya kilo 223 zilikamatwa na Askari Polisi wa Kibaya waliokuwa kwenye Doria wakati ikisafirishwa kutoka Maeneo ya Tanga kuja Kiteto

Taarifa za ukamataji wa shehena hiyo zimeelezwa kuwa Askari Polisi wa Kibaya ASP Mwita na Mkuu wa Trafiki Kiteto akiwa na PC 5530 Japhesi wakiwa katika doria walitilia shaka gari ndogo aina ya Toyota carina yenye namba za usajili T 436 BNK   ambao walianza kukimbia kisha kukamatwa

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Manyara Christopher Fuime alitaja majina ya watuhumiwa hao kuwa ni Sefu Amour (22) dereva wa gari hiyo na Halifa Iddy (35) wakidai kuwa walikodiishwa na mwenye mzigo huo ambaye hakuwepo walipokamatwa

Kamanda Fuime alitoa wito kwa wananchi  kufanya kazi halali za kuwapatia kipato ili kuepuka usumbufu wa kazi ambazo zinakatazwa na sheria na ambazo mtu akikamatwa sheria kali zinachukuliwa dhidi yake

Kwa mujibu wa taarifa za uhakika kutoka wilayani humo zinaeleza kuwa madawa hayo ya kulevya yana thamani kubwa inayokadiriwa kuwa Tsh mil 9,250,000,ambapo huwa yanauzwa kwa kilo moja elfu hamsini

“Mirungi hii inatoka Kenya inathamani kubwa katika maeneo haya na ndio maana kila mara hupitishwa maeneo haya pamoja na kuwa hukamatwa bado watu wanaleta na kuuza maeneo mbalimbali ya wilaya za Kiteto,Chemba na Kondoa”alisema mmoja wa mashuhuda katika kituo hicho cha polisi

Kwa mujibu wa mkuu wa Polisi wilaya ya Kiteto Bw.Geoge Katabazi alisema kila mara Polisi wilayani humo wakiwa kwenye doria hukamata watuhumiwa wa madawa hayo na kuwafikisha mahakamani ambapo mamlaka nyingine ya kisheria huchukuwa mkondo wake

Mwisho

Maoni