Wagombea Ubunge CCM Kiteto waanza kuchafuana.




Wagombea Ubunge CCM Kiteto waanza kuchafuana.
·         
          Watumia ukabila na uraia kuwagawa wanachama

NA.MOHAMED HAMAD MANYARA.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi CCM Wilayani Kiteto mkoani Manyara Abeid Maila, amewatoa hofu wanachama wa chama hicho kuwa, mjumbe wa Halmshauri kuu ya CCM Taifa Emmanuel Papian ni raia halali wa Tanzania ana haki ya kugombea Ubunge tofauti na inavyosambazwa na wahasimu wake

Akizungumza hayo kwenye mkutano wa kampeni za CCM kata ya Njoro Maila alisema, anasikitishwa na vitendo vya wagombea hao kuchafuana kwa misingi ya ubaguzi wa kikabila na uraia wakati wao ni familia ya Baba na mama mmoja  ambao wanatakiwa kupendana na kusaidiana

“Kama kuna mashaka ya uraia wa Emmanuel Papian mwende Ofisi za uhamiaji, huko… mtapata ukweli wa mambo jambo hili CCM hatuna shaka nalo, uraia wake ni halali na ndio maana akapata nafasi kubwa ndani ya chama chetu hiki mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa NEC tuache vijembe tuusaidie umma”alisema katibu huyo

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya gazeti la CHAPAKAZI kuchapishwa habari yenye kichwa kisemacho “CCM Manyara katika kashifa nzito” na kusambazwa kwenye mikutano ya kampeni hizo ili wajumbe wasimchague kwakuwa sio raia wa Tanzania

Kwa mujibu wa taarifa hizo zilielezwa kuwa Chama cha Mapinduzi CCM kimeingia kwenye kashfa ya kumpitisha Emmanuel Papiani kuwa mjumbe wa Halamshauri kuu ya CCM wakati ni raia wa Rwanda kinyume na taratibu za nchi

Wanachama wa CCM waliotajwa kutoa malalamiko hayo kupitia kwenye gazeti hilo ni Saidi Msonde wa kijiji cha Engusero na Msafiri Rashidi ambao wametajwa kuwa ni wafuasi wa mgombea mmoja wakisema chama kimepoteza imani kwa wananchi

Akizungumza kwa niaba ya Chama hicho baada ya mmoja wa wanachama aliyejitambulisha kwa jina la Amir Issa kuhoji juu ya vitendo vya wagombea hao kuchafuana kupitia vipeperushi hivyo, katibu huyo wa CCM Wilaya alisema wanachama wapuuze rafu hizo za kisiasa

“Toka mwaka 2012 nilimkuta Emmanuel Papian akiwa Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa, nafasi hii ilihojiwa sana na ukweli ukathibitika kuwa ni raia halali wa Tanzania, sasa niseme tu kwamba hizi ni kampeni chafu kuwafanya wananchi washindwe kufanya maamuzi sahihi kwa nafasi yangu nitachukua hatua”alisema Maila

Awali akizungumza na wanachama hao Emmanuel Papian alipopata nafasi ya kuomba ridhaa kwa wanachama hao aliwataka wapuuze taarifa hizo akisema zimelenga kuchafua na kuwagawa wananchi kwa itikadi za kisiasa,ukabila ambao unazidi kushika hatamu wilayani humo

Alisema Watanzania hawajafikia hatua ya kubaguana na kuwataka kutafari kwa kina juu ya kinachoendelea,hasa amani inayotoweka  siku hadi siku kwa wakulima na wafugaji kuuana huku akiwataka kufanya maamuzi sahihi ya kumpata kiongozi mwenye kujibu matatizo yao mwenye uwezo wa kuthubutu na kukemea

Alisema propaganda hizo ndizo zilizofanikisha baadhi ya viongozi wa kisiasa kuingia madarakani kwa kuweka mapandikizi ya watu kugombea na kugawa  kura kwa lengo la kujihakikishia ushindi ambao hadi leo Kiteto imeendelea kuingia kwenye rekondo mbaya ya ubaguzi wa kikabila unaosababisha mauaji

Kuhusu Wilaya kuingia kwenye rekodi mbaya ya mauaji ya wakulima na wafugaji Papiani alisema hali hiyo imetokana na kuendekezwa kwa ukabilana baadhi kwa viongozi ambao wananufaika na migogoro hiyo.

Katika hatua hiyo alisema mgogoro wa ardhi Kiteto haujaisha akikidai unaibuka mara kwa mara huku watu wakiendelea kupoteza maisha akisema, atakapoingia madarakani kazi atakayoanza  ni kuhubiri amani kwa kukutanisha makundi yote

Kwa upande wake Hajjat Amina Saidi Mrisho wakati akijinadi alisema kuwa hakuna anayemtumia kama inavyotafsiriwa bali amesukumwa na uzalendo wake kuona wananchi wa Kiteto wanaendelea kupoteza maisha kwa kugombea ardhi

Kama kamishna wa sense Taifa sikuweza kusema chochote wakati wakulima na wafugaji wanauana kwakuwa mimi ni mtumishi maadili hayaniruhusu kufanya hivyo lakini sasa nimeomba ruhusa nimekuja mnipe ridhaa ni malize matatizo haya alisema baada ya kuulizwa swali la siku zote alikuwa wakati watu wanakufa

Naye Benedict Ole Nangoro akijibu maswali aliyoulizwa na wanachama kuhusu mauaji ya Kiteto alisema, ongezeko la watu pamoja na uhaba wa maji umechangia tatizo hilo, “Serikali ilifanya kazi yake hivyo sikuona sababu ya kuwa mstari wa mbele kwa kuwa nchi hii inatawaliwa kwa utawala wa sheri na kuheshimu mihimili iliyopo

“Tuna mihimili mitatu Mahakama, Serikali, na Bunge kwa nafasi yangu kama Mbunge, sikuona sababu ya kuingilia mhimili mwingine, kwani wahalifu walikamatwa na sheria imefuata mkondo wake, kuhusu nafasi ya Uwaziri sikufukuzwa kwa misingi ya Ufisadi bali niliwajibika kisiasa kutokana na zoezi la (TOKOMEZA)”alisema Nangoro

Kwa upande wake Ally Juma Lugendo alisema akipata nafasi ya kuongoza Jimbo la Kiteto atarejesha fadhila kwa wananchi kwa kuwatumikia baada ya kupata elimu kwa kodi za wananchi na kwenda nchi mbalimbali duniani kujifunza

Alisema anauwezo mkubwa na elimu aliyoipata kutoka nchi mbalimbali hapa Duniani hivyo anatamani siku moja kupewa djamana hiyo ili arudishe fadhila za wananchi wa Kiteto kwa kuwatumikia

Joseph Mwaleba Afisa Maendeleo ya Wilaya ya Kiteto akiomba ridha wanachama hao alisema amekerwa na hali ya maisha ya wananchi wa Jimbo hilo lenye rasilima nyingi kushindwa kutumika kuwasaidia wananchi na kubaki kugombea ardhi

Alisema asilimia 10% za vijana amezitumia kwa kuzigawa kwa walengwa lakini hazina tija kutokana na muda mwingi kutumika kutatua migogoro kuliko kufanya shuhuli zingine za maendeleo hivyo wananchi kuishi kwa wasiwasi kuhofia kuuawa na wenzao (wafugaji)

Kwa mujibu wa Katibu huyo wa CCM Bw. Maila alisema jumla ya makada watano wa chama cha mapinduzi CCM wamejitokeza kuwania Jimbo la Kiteto ambalo kwa sasa linachangamoto kubwa ambapo kila mkutano suala la mgogoro lazima liulizwe

Mwisho

Maoni