MJUMBE WA HALMASHAURI KUU YA CCM TAIFA LIVINGSTONE LUSINDE AKIMNADI EMANUEL PAPIAN JIMBO LA KITETO






Lusinde amshukia mgombea Urais wa Ukawa

  • ·                    Amtaka authibitishie umma afya yake

  • ·                   Asema ana mashaka ya uelewa wa Sumaye

  • ·                  Adai hata Kikwete akiondoka, CCM itashinda

  • ·                 Wagombea wa Ukawa wote ni Ma-TX

Na. Mohamed Hamad 
MJUMBE wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa na mgombea Ubunge kwa tiketi ya chama cha mapinduzi CCM Jimbo la Mtera Livingstone Lusinde (Kibajaji), amemshukia mgombea Urais wa Ukawa Edward Lowassa na Fredrick Sumaye kuwa hawana fadhila

Akizungumza na mamia ya wananchi kwenye uzinduzi wa kampeni za CCM Kiwilaya zilifanyikia kata ya Matui Wilayani Kiteto mkoani Manyara Lusinde alisema, Serikali ya CCM iliwapa dhamana kubwa viongozi hao kama walishindwa , watawezaje kuwatumikia hivi sasa kupitia Ukawa

“Tatizo lililopo kwa viongozi wengi hapa nchini, ni kukosa uvumilivu wa kisiasa, mtu akiambiwa apumzike ili mwingine naye aongoze inakuwa nongwa, atabubujikwa na maneno mengi na hata kuzua maneno kuwachanganya wananchi ili washindwe kugundua ukweli”alisema Lusinde

“Wananchi mtafakari viongozi waliohama CCM na kujiunga na Ukawa, kule wamepewa nafasi za kugombea waulizeni walifanya nini awali hao ni Ma-TX hawana jipya Edward ametoka CCM,Chadema wamemwazima mgombea mwenza wa urais kutoka  CUF sio muumini wao”alisema Lusinde

Alisema katika miaka ya uchaguzi ambayo CCM itashinda kwa rahisi ni mwaka huu wa 2015 kwani wagombea wote ni wa CCM, tunafahamiana, Watanzania tendeni haki katika kuamua wenu nani anafaa kuongoza alisisitiza Lusinde

Katika hatua hiyo alisema Waziri Mkuu mstaafu Fredirck Sumaye hajaeleweka kwa watanzania, kwani kati ya viongozi walionufaika na chama kwa miaka mingi ikiwemo ile ya uwaziri mkuu ni yeye kilichomkimbiza CCM ni nini?alihoji Lusinde

Wamasai kujiunga na Ukawa
Kuhusu jamii ya kifugaji wamasai kujiunga na Lowassa aliyehamia CHADEMA  alisema, Hakuna ukweli wowote, akidai  wakati akiwa kiongozi mkuu wa Serikali aliwasaidia nini, mbona mpaka sasa baadhi yao wameendelea kulinda makufuli mijini (walizi) alisema Lusinde

Alisema kama hoja hiyo ina ukweli, wagombea wanaotokana na jamii ya kifugaji masai ambao wako CCM watapigiwa kura na nani ikiwa wote watahamia CHADEMA kwa Lowassa, alisema kwa hisia kali

JK akihama, CCM itashinda tu
Akiaminisha wana-CCM Lusinde alisema, hata kama Jakaya Mrisho Kikwete ataihama, CCM itaendelea kuongoza na kushinda chaguzi mbalimbali tena kwa kishindo dhidi ya vyama vya upinzani

Alisema CCM ni chama imara ambacho kimetandaa nchi nzima tofauti na vyama vingine vya siasa ambavyo toka kuanzishwa mfumo wa vyama vingi hapa nchini mwaka 2002, havijaweza kuingia kwenye maeneo waliko CCM

Kuhusu mkoa wa Arusha kuwa na bahati ya pekee kutoa mawaziri wakuu watatu, Lusinde alisema hiyo ni bahati ya pekee ambayo mikoa mingine hapa nchini haikupata fursa hiyo, hivyo iko haja kwa viongozi hao kushukuru kupata nafasi hiyo

“Tazama Marehemu Sokoine alitoka Arusha,Sumaye huko huko na Edward naye pia, sasa mnataka nini tena wananchi wa kanda hiyo, hebu tuangalie na haki itendeke”alisisitiza Lusinde huku ummati mkubwa wa wananchi ukizizima kumshangilia

Akimnadi mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM na mgombea Ubunge wa Jimbo la Kiteto Emmanuel Papian Lusinde alisema Kiteto ina uongo mwingi ambao ulifanya jina hilo kucheleweshwa mara baada ya kura za maoni, lakini baada ya uchunguzi imeonekana kuwa anafaa

“Sikilizeni wananchi wa Kiteto, mimi ni mwanaume… kule Jimboni kwangu wananifahamu, hata wajumbe wenzangu wa NEC wananielewa, kazi ngumu ilikuwa ni maamuzi tuliyofanya Dodoma kubakiza majina matatu, wananifahamu Lusinde ni nani …mimi ni mwanaume bwana usisikie”alisikika Lusinde akisema hivyo

Alisema mgombea huyo alionekana kuletewa maneno mengi kuwa hafai hali ambayo yeye alishauri uchaguzi urudiwe lakini aliambiwa na wakubwa zao kuwa atulie..na kuundwa tume maalumu kuchunguza na kubaini anayefaa kuwa ni yeye

Akizungumza na wananchi hao Emmanuel Papian aliwashukuru kwa kumteua ndani ya chama chake na kuwaomba nguvu hiyo ya umma itumike kumthibitisha ili aweze kutatua matatizo na kero mbalimbali za wananchi zinazowakabili kwa muda mrefu bila ufumbuzi

“Ndugu zangu wananchi,baada ya shukurani zangu za dhati kwenu kunipitisha kuwa mgombea nipeni sasa ridhaa na mnithibitishe ili nianze kuchapa kazi, najua nini mahitaji ya wanakiteto kwani hata mimi ninayaishi hapa”alisema Papian

Alisema cha kwanza atakachoanza nacho ni kurejesha amani iliyokwisha kutoweka miongoni mwa wanaKiteto kutokana na mgogoro wa ardhi,ataimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja na vikundi kwa kutumia taasisi za kifedha

Lingine ni kusimamia upatikanaji wa huduma za jamii bora na kwa wakati kwa kushirikiana na Serikali na mashirika ya umma kuhakikisha kuwa wananchi wananufaika na fursa hizo ambazo kwa muda mwingi zimekuwa adimu

Aliwataka wananchi hao kukichagua chama cha mapinduzi CCM kuanzia nafasi ya udiwani,Ubunge na Urais kuwa itakuwa rahisi kufikia malengo ya wananchi kwa kuzungumza kwa kuelewana tofauti na kuwa na mchanganyiko wa viongozi mbalimbali toka vyama vingine

Kwa upande wake Mbabire Oleikurukuru kiongozi wa mila wa jamii ya kifugaji masai aliyefuatana na viongozi wenzake katika uzinduzi huo wa kampeni za CCM alisema sasa jamii hiyo imepata mwelekeo kuwa nani watampigia kura

“Tumeamua kuipa CCM kura, kura za wafugaji wamasai zimenyooka, wale waliosema kuwa tumehamia CHADEMA hapana tupo na CCM mpaka mwisho hatuja wahi kuihama CCM”alisema huku akishangiliwa na wanananchi hao

Mwisho



Maoni