UKAWA– KESHO HATUNA KAMPENI

UKAWA– KESHO HATUNA KAMPENI




Mgombea Mwenza wa Chadema, Juma Duni Haji katika moja ya kampeni zake
VYAMA vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vitasitisha kampeni zake ngazi zote kesho tarehe 20 Oktoba kutoa fursa kwa wananchi kuaga mwili wa aliyekuwa mwenyekiti mwenza, Dk. Emmanuel Makaidi.
Dk. Makaidi, aliyekuwa pia Mwenyekiti wa National League for Democracy (NLD) alichokianzisha mwaka 1992, na mgombea ubunge jimbo la Masasi mkoani Mtwara, alifariki dunia Alhamisi wiki iliyopita katika hospitali ya Nyangao, Masasi, baada ya kuugua ghafla ugonjwa wa shinikizo la damu (presha).
Ofisa Habari wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tumaini Makene, akizungumza kwa niaba ya UKAWA, leo jijini Dar es Salaam, amesema usitishaji wa kampeni umelenga kuonesha heshima ya kipekee kwa Dk. Makaidi ambaye alijitoa muhanga katika kuimarisha UKAWA kwa hali na mali.

“Kesho kuanzia saa tatu asubuhi tutakuwa viwanja vya Karimjee kwaajili ya kutoa heshima za mwisho kwa Dk. Makaidi, sambamba na hilo pia tutasitisha kampeni zetu za ngazi zote na katika shughuli hiyo viongozi wote wa kitaifa wa UKAWA pamoja mgombea Urais watakuwepo” amesema Makene.

Baada ya mwili wa Dk. Makaidi kuagwa katika viwanja vya Karimjee, shughuli ya mazishi ya mwanasiasa huyo mkongwe aliyefariki akiwa na umri wa miaka 74 itahitimishwa katika makaburi ya Sinza jijini Dar es Salaam.

Ratiba ya kampeni itaendelea Jumatano ya tarehe 21 Oktoba kwa mgombea urais wa Ukawa, Edward Lowassa kwenda mkoani Morogoro kumalizia majimbo ambayo hakufika katika awamu yake ya kwanza ya kampeni mkoani hapo.

Majimbo hayo ni pamoja na jimbo la Kilombero, Mlimba, Mikumi, Ulanga Mashariki na Ulanga Magharibi.
MWANAHALISI

Maoni