ARUSHA INAONGOZA KWA UMILIKI WA BUNDUKI



Arusha. Mkoa wa Arusha umetajwa kati ya mikoa ya pembezoni nchini ambayo inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu wanaomiliki silaha za moto, hasa bastola.
Katika maeneo ya burudani katika jiji la Arusha kumekuwapo na matukio ya watu kutishiana kwa bastola jambo ambalo limesababisha ulinzi kuimarishwa katika maeneo haya na baadhi ya wateja kuzuiwa kuingia ndani na silaha hizo.
Uchunguzi wa kina uliofanywa na Mwananchi umebaini kuwa idadi kubwa ya vijana katika jiji la Arusha wanamiliki bastola, baadhi kihalali na wengine kinyume cha sheria.
Kwa wanaomiliki kihalali ni wale waliofuata utaratibu za kisheria za umiliki, ambao unaanzia ngazi ya kijiji au mtaa, kujadiliwa na baadaye kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya, kamati ya mkoa na hatimaye makao makuu ya polisi.
Hata hivyo, kati ya wanaomiliki kihalali, kuna kundi ambalo linamiliki bastola hizo kihalali kupitia mawakala ambao hulipwa kati ya Sh1.5 milioni hadi Sh2 milioni.
Uchunguzi umebaini kuwa watu wengi wanaomiliki silaha hizo kinyume cha sheria ndiyo wanazitumia katika matukio ya uhalifu.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas licha ya kukiri vijana wengi kumiliki bastola katika jiji hilo, alisema wengi wanaozimiliki wamezipata kwa kufuata sheria.
Hata hivyo, katika kudhibiti silaha hizo, alisema jeshi hilo kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama limesitisha kutoa vibali vya umiliki wa bastola.
“Tumesitisha kutoa vibali vya bastola lakini tunatoa vibali vya silaha nyingine kwa mahitaji maalumu, lakini silaha zilizopo mikononi mwa watu ni zile ambazo zilitolewa kipindi kirefu cha nyuma,” alisema.
Alisema baadhi ya waliopata bastola kipindi cha nyuma ni wafanyabiashara na wachimbaji wa madini katika maeneo ya Mererani kulingana na biashara zao.
Hata hivyo, alisema silaha hizo zilitolewa kihalali lakini baadhi ya wamiliki wamekuwa si waangalifu katika utunzaji na hivyo kufanya baadhi kuwafikia watu wasio waaminifu.
“Katika matukio ya ujambazi ambayo yanatokea hapa Arusha, silaha ambazo tunakamata ni zile ambazo zilizotolewa kihalali lakini wamiliki wake waliibiwa au kupoteza,” alisema.
Alisema uhakiki wa silaha ambao umekuwa ukifanywa na jeshi hilo na kwa kiasi kikubwa umesaidia kuziondoa bastola mikononi mwa watu wasio waaminifu.
Kuuzwa kwa silaha
Mwananchi imebaini kuwa, baadhi ya wamiliki wa silaha hasa bastola wamekuwa wakiuza mitaani kutokana na hali ngumu ya maisha.
Joram Kaaya mkazi wa Ngulelo alilieleza gazeti hili kuwa kipindi cha nyuma vijana wengi wa Mirerani walinunua silaha kihalali kutokana na biashara zao lakini sasa kutokana na kuporomoka biashara ya madini ya Tanzanite wamekuwa wakiuza.
“Bastola zinauzwa kati ya Sh1,000,000 hadi 2.5 milioni kutoka kwa wamiliki lakini wanakueleza kufuata taratibu za umiliki, kwa kuandika barua ya umiliki wa silaha ngazi ya mtaa na kwenda polisi kabla ya kukabidhiwa silaha na kitabu chake,” alisema.
Mkazi mmoja wa Arusha, aliyeomba kuhifadhiwa jina, lake alikiri kuwapo kwa madalali wa silaha ambao wamekuwa wakifuata taratibu za umiliki wa silaha.
“Mimi mwenyewe nimenunua bastola yangu kwa mtu lakini kabla ya kumiliki nilifuata taratibu zote za kipolisi na kiserikali na nimekuwa nikiilipia kila mwaka,” alisema.
Hata hivyo, Kamanda Sabas alikemea utaratibu wa kununua silaha mitaani akisema ni kuvunja sheria.
“Ni makosa kisheria, kuuza na kununua silaha mitaani ambao watakamatwa watafikishwa katika vyombo vya sheria, kuna taratibu za umiliki kwa ambao wanahitaji silaha ni vyema kuzifuata,” alisema.
Silaha kutoka nje
Wakati polisi wakieleza kuwapo udhibiti mkubwa katika uingiaji wa silaha katika njia haramu, taarifa zilizolifikia Mwananchi zinaeleza kuwa wapo watu wanaziingiza kutoka nje ya nchi kupitia njia za panya.
Silaha hizo, zinaelezwa kuingizwa kwa kubadilishana na bidhaa mbalimbali kama vyakula, mifugo na fedha.
Katika Wilaya ya Ngorongoro pekee, ambayo ipo mpakani na nchi jirani na Kenya, mara kadhaa polisi, wamekuwa wakikamata silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria ambazo zinamilikiwa na makundi ya wafugaji na wakulima ambao wamekuwa wakipigana mara kwa mara kugombea ardhi.
Mwaka juzi silaha zaidi ya 80 zilikamatwa katika operesheni ya polisi katika wilaya ya Ngorongoro pekee na kumekuwapo na taarifa za wakazi wengi wa wilaya hiyo kumiliki silaha kinyemela.
Wilaya nyingine zenye wamiliki wengi wa silaha ama halali au haramu ni Arumeru na Longido huku wilaya za Monduli na Karatu zikiwa hazijaathiriwa sana na kuzagaa kwa silaha.

Maoni