KIDATO CHA NNE KUANZA MITIHANI YA KUHITIMU KESHO NOVEMBER 2


Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa.

WATAHINIWA 448,358 wa shule na wa kujitegemea, wanatarajiwa kufanya mtihani wa kumaliza kidato cha nne, kuanzia kesho hadi Novemba 27 mwaka huu. Idadi hiyo ni ongezeko la watahiniwa 150,870 ikilinganishwa na watahiniwa 297,488 waliosajiliwa mwaka 2014.

Aidha, Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Dk Charles Msonde alisema jana kwamba baraza lake halijapokea taarifa ya kuwapo hali itakayoathiri ufanyaji wa mitihani Zanzibar.

Alipoulizwa kama hali ya kisiasa Zanzibar itawaruhusu wanafunzi kufanya mitihani yao, Dk Msonde alisema “Mpaka sasa baraza halijapokea taarifa ya kuwapo hali itakayoathiri ufanywaji wa mitihani.

Hivyo wanafunzi wote watafanya mitihani yao kuanzia Jumatatu kama ilivyopangwa.” Akizungumzia mitihani hiyo, Dk Msonde alisema watahiniwa 394,243 kati ya 448,858 walisajiliwa kufanya mitihani yao ni wa shule na wanafunzi 54,115 ni wa kujitegemea.

Alisema kati ya watahiniwa wa shule 394,243 waliosajiliwa,wavulana ni 193,082 ambao ni asilimia 48.97 na wasichana ni 201,161 sawa na asilimia 51.03. “Watahiniwa 67 kati ya hao ni wasioona na watahiniwa wenye uoni hafifu ni 278 ambao maandishi ya kataratasi zao za mitihani hukuzwa,” alisema.

Dk Msonde alisema kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea waliosajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2015, wanaume ni 26,051 sawa na asilimia 48.14 na wasichana ni 28,064 sawa na asilimia 51.86. Watahiniwa wa kujitegemea wasioona ni wawili ambao wote ni wanaume.

Kwa upande wa Mitihani wa Maarifa (QT), Dk Msonde alisema watahiniwa 19,547 wamesajiliwa kufanya mtihani mwaka huu, wanaume wakiwa 7,225 ambao ni asilimia 26.96 na wanawake ni 12,322 ambao ni asilimia 63.03. Mwaka 2014 walikuwa watahiniwa wa Maarifa walikuwa 14,723.

“Maandalizi yote kwa ajili ya mtihani huo yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa mtihani, vijitabu vya kujibia na nyaraka zote muhimu zinazohusu mtihani huo katika mikoa yote Tanzania Bara na Zanzibar,” alisema Dk Msonde.

Maoni