Kipindupindu chatinga Kiteto



                                    RAMANI YA MKOA WA MANYARA

Mohamed Hamad
Kiteto,Watu watatu wa maeneo tofauti wamelazwa wilayani Kiteto mkoani Manyara kutokana na ugonjwa wa kipindupindu, baada ya kugundulika vipimo vya wagonjwa hao vilivyopelekwa Dodoma

Kambi ya wagonjwa hao imefunguliwa Zahanati ya kata ya Bwagamoyo wilayani humo ambapo mgonjwa mmoja amelazwa, huku watu wengine wawili wakiwa wamelazwa katika moja ya majengo ya Hospitali ya wilaya ya Kiteto

Bwana afya wa Wilaya ya Kiteto Annicet Munga akizungumza na gazeti hili alisema kwa mujibu wa sheria za afya mtu mmoja akigundulika kuwa na ugonjwa wa kipindupindu wengine wote wenye dalili hizo wanahesabika kuwa wanaugonjwa huo

“Mgonjwa wa kwanza tulipeleka sample yake Dodoma na kugundulika kuwa anao, ambapo wengine tunaendelea na vipimo na kwa sheria ya afya lazima tuwaweke pamoja kuwapa matibabu kwa kuwa wanadalili zote”alisema Munga

Alisema jitihada zinazofanyika kukabiliana na ugonjwa huo ni kuhakikisha kunapatikana kwa madawa wakati wote ambapo Mganga mkuu wa wilaya ya Kiteto aliwasilisha jana mahitaji ya wilaya Mkoani

Wakati jitihada zikifanyika tahadhari imeanza kuchukuliwa na mabwana afya kufanya matangazo ya kuwatahadharisha wananchi juu ya ugonjwa huo huku wakizunguka kila kaya kuhamasisha wananchi kufanya usafi kwenye maeneo yao

Moja ya matatizo yaliyopo wilayani Kiteto ni pamoja na wananchi kutokuwa na utamaduni wa kuchimba vyoo kwenye kaya zao na badala yake  kaya tatu mpaka nne zinaweza kuwa na shimo moja tu la choo

“Jamii ya kifugaji wamasai ukienda huko usitegemee kuona shimo la choo, sasa hapo ndipo kwenye matatizo na wao maji wanayotumia ni yale yanayotiririka makorongoni kubwa zaidi ni kuhamasisha watu wachemshe maji na wale vyakula vya moto”alisisitiza Bwana afya Munga

Kwa upande wa wananchi wilayani humo wakizungumzia ugonjwa huo walisema hakuna asiyefahamu sheria, kila mtu anajua hivyo kwa ukubwa wa tatizo hilo mabwana afya wanatakiwa kusimamia sheria hizo ili kuokoa vifo vya watu vinavyoweza kujitokeza kwa uzembe

Kwa mujibu wa Bwana Afya huyo hakuna mtu aliyepoteza maisha kwa ugonjwa huo huku akitoa wito kila mtu kuchukua tahadhari juu ya gonjwa hilo ambalo kwa sasa limekuwa tishio pamoja na kuwemo dawa za awali

mwisho


Maoni